Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahoua, Dube wanavyozibeba Simba, Yanga

Muktasari:

  • Amefunga 12 na asisti 6. Hao ndiyo wachezaji waliohusika kwenye mabao mengi hadi sasa kwenye ligi wakifuatiwa na Feisal Salum mwenye mchango wa mabao 16, akifunga 4 na asisti 12 akiitumikia Azam.

Unapoiangalia Yanga pale kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 58, basi tambua kuna mchango wa mshambuliaji wao, Prince Dube ambaye amehusika kwenye mabao 17 kati ya 58 yaliyofungwa na timu hiyo. Mchango wake huo unatokana na kufunga mabao 10 na asisti 7.

Upande wa pili kwa maana ya Simba yenye pointi 57, Jean Charles Ahoua naye amehusika kwa mabao mengi kikosini hapo ambayo ni 18 kati ya 52. Amefunga 12 na asisti 6. Hao ndiyo wachezaji waliohusika kwenye mabao mengi hadi sasa kwenye ligi wakifuatiwa na Feisal Salum mwenye mchango wa mabao 16, akifunga 4 na asisti 12 akiitumikia Azam.

Wachezaji hao wawili ni wapya kwenye timu zao kwa maana wametua msimu huu wa 2024-2025 ulipoanza. Hata hivyo, Dube si mgeni kwenye Ligi Kuu Bara kwani yupo tangu Agosti 2020 alipotua kwa mara ya kwanza kuichezea Azam akitokea The Highlanders ya kwao Zimbabwe. Huu ni msimu wa tano Bongo.

Ndani ya kikosi cha Azam FC, Dube alikuwa na kiwango cha kupanda na kushuka huku msimu wake bora zaidi ukiwa ni ule wa kwanza 2020/2021 alipofunga mabao 14 katika Ligi Kuu Bara huku akifuatiwa na msimu mbovu zaidi 2021/2022 akifunga bao moja pekee. Katika misimu yake minne iliyopita akiwa Azam, Dube raia wa Zimbabwe amefunga mabao 34 kwenye Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji huyo msimu huu alianza taratibu kwani hakufunga katika mechi 10 za kwanza kabla ya kuibukia ya 11 alipopiga hat trick ikiwa ni ya kwanza kwake msimu huu na kwa Ligi Kuu Bara ambapo hadi sasa zimefungwa tatu. Zingine kupitia Aziz Ki wa Yanga na Steven Mukwala wa Simba.

Katika mechi hizo 10 za kwanza ambazo Dube alicheza bila ya kufunga, alikuwa na asisti moja pekee huku akitumika kwa dakika 446. Baada ya hapo akafunga mfululizo dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji.

Dube alikuja kucheka tena na nyavu Februari 5, 2025 alipopiga mawili dhidi ya KenGold, akashindwa kufunga dhidi ya JKT Tanzania, akaendeleza moto kuzifunga KMC, Singida Black Stars na Mashujaa ambapo hapo alifunga mechi tatu mfululizo.

Tunapomuangalia Dube hivi sasa wakati ligi imesimama kupisha Kalenda ya Fifa, mshambuliaji huyo amecheza mechi 19 kati ya 22 za Yanga kwa dakika 1162.

Kwa upande wa Ahoua aliyetua Simba akitokea Stella Club d’Adjamé ya nchini kwao Ivory Coast, moto alianza kuuwasha mapema tu kwani mechi ya kwanza alitoa asisti, kisha ya pili akafunga bao moja na kutoa asisti mbili.

Ahoua anafukuzia rekodi yake ya msimu uliopita 2023-2024 aliyoiweka nchini Ivory Coast ambapo aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu (MVP) huku akifunga mabao 12 na kutoa asisti tisa. Tayari amefunga mabao 12, huku akidaiwa asisti tatu kuzifikia za msimu uliopita. Ili kuvunja rekodi, anahitaji bao moja na asisti nne katika mechi nane zilizobaki.


MABAO YAO

Dube mabao yake 10 aliyofunga hakuna la penalti, huku pia akiwa na hat trick moja, wakati Ahoua ana mabao matano ya penalti, sita ya kawaida na lingine faulo ya moja kwa moja kitu kinachomfanya kiungo huyo kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga kupitia mipira ya kutenga na kawaida.

Jambo linalowafanya nyota hao kufanana katika kufunga mabao yao hadi sasa, asilimia kubwa wameyafunga ndani ya boksi, lakini Ahoua ana moja pekee nje ya boksi lile dhidi ya Kagera Sugar kwa njia ya faulo wakati Simba ikishinda 2-5 ugenini.

Dube ubora wake zaidi upo katika kutumia mipira ya vichwa kwani ana mabao sita aliyofunga kwa mtindo huo huku matano akitumia mguu.

Yanga na Simba ndiyo timu zilizocheza mechi chache kulinganisha na zingine katika Ligi Kuu Bara ambapo klabu hizo kongwe zimeshuka dimbani mara 22 kila moja huku mechi yao ya Machi 8 ikiota mbawa baada ya kuahirishwa huku ikitarajiwa kupangiwa tarehe nyingine.

Vita ya wakongwe hao katika kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, ni kama wameachiwa wenyewe kufuatia Azam kuachwa mbali kwa pointi tisa hadi kumi ikibakiwa na mechi saba, ili kuzipiku inahitaji kushinda mechi zake na kuziombea mabaya Simba na Yanga ziteleze.

Hata hivyo, ushindani uliopo kwa Yanga na Simba huku mastaa wake wakiendelea kupambana kujitoa kwa nguvu zote, inatoa nafasi ndogo kwa Azam kusogelea nafasi hizo mbili za juu zaidi ya kupambania kubaki ya tatu ili kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Ubabe wa Simba na Yanga umekuwepo kwa muda mrefu huku timu hizo zikitawala zaidi ligi kuanzia mwaka 2001 hadi sasa ambapo kuanzia kipindi hicho hadi sasa, ni mara moja pekee Azam imewatibulia msimu wa 2013-2014 ilipobeba ubingwa, huku misimu mingine 23 utawala ukibaki kwao. Yanga ikichukua ubingwa mara 13 huku Simba ikibeba mara 10 ndani ya kipindi hicho.

Kwa jumla, Yanga ina mataji 30 ya Ligi Kuu huku Simba ikiwa nayo 22 tangu kuanza kwa michuano hiyo mwaka 1965.


MISIMU MITANO YA DUBE BONGO

MSIMU: 2020-2021 (MABAO: 14)

MSIMU: 2021-2022 (MABAO: 01)

MSIMU: 2022-2023 (MABAO: 12)

MSIMU: 2023-2024 (MABAO: 07)

MSIMU: 2024-2025 (MABAO: 10)


TAKWIMU ZA JEAN CHARLES AHOUA

MECHI: 21

DAKIKA: 1457

KUANZA: 17

KUTOKEA BENCHI: 04

MABAO: 12

ASISTI: 06

PENALTI: 05

HAT-TRICK: 00


PRINCE DUBE

MECHI: 19

DAKIKA: 1162

KUANZA: 14

KUTOKEA BENCHI: 05

MABAO: 10

ASISTI: 07

PENALTI: 00

HAT-TRICK: 01

TIMU ALIZOZIFUNGA AHOUA

Fountain Gate (1)

Dodoma Jiji (3)

Namungo (3)

KMC (2)

Kagera Sugar (1)

JKT Tanzania (1)

Tanzania Prisons (1)

TIMU ALIZOZIFUNGA DUBE

Mashujaa (4)

Tanzania Prisons (1)

Dodoma Jiji (1)

KenGold (2)

KMC (1)

Singida Black Stars (1)