Namungo FC yapania kufanya makubwa Ligi Kuu

Muktasari:
KOCHA Mkuu wa Namungo FC, Hitimana Thierry amesema ligi ya msimu ujao itakuwa ngumu kutokana na usajili mzuri uliofanywa na timu nyingi hivyo kama hatajipanga atapata tabu sana.
KOCHA Mkuu wa Namungo FC, Hitimana Thierry amesema ligi ya msimu ujao itakuwa ngumu kutokana na usajili mzuri uliofanywa na timu nyingi hivyo kama hatajipanga atapata tabu sana.
Hitimana ambaye pia aliwahi kuinoa Biashara United mwanzoni mwa msimu uliopita ameiwezesha Namungo FC kupanda daraja na kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao kwa mara ya kwanza.
Kocha huyo Mrundi amekiri safari hii timu nyingi zimefanya usajili wa maana hasa kwa kuchukua wachezaji wazoefu hivyo lazima wajipange vilivyo ili kuhakikisha wanatisha kwenye ligi.
"Tunaendelea na maandalizi kuhakikisha msimu ujao tunafanya vizuri. Sisi ni wageni kwenye ligi hivyo lazima tujipange sana kumudu mikikimikiki ya Ligi Kuu.
"Natarajia ligi ngumu na yenye ushindani kwani timu nyingi zimeonekana kufanya usajili mzuri na zimechukua wachezaji wazoefu hivyo bila kujipanga vizuri unaweza ukajikuta unapata wakati mgumu," amesema Hitimana.
Namungo FC itafungua pazia la Ligi Kuu Bara kwa kuikaribisha Ndanda Agosti 24, mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi.