Uwezo wa kifedha wa mtu unavyoakisi uchumi wa familia
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalumu wa Benki ya Stanbic,Beatrice Kisoka.
Katika mazingira mengi duniani, uwezo wa kifedha mara nyingi huonekana kama mafanikio ya mtu binafsi. Hupimwa kwa mali alizonazo mtu, kiwango cha mapato yake, au ukubwa wa uwekezaji alioufanya.
Lakini nchini Tanzania, picha ni tofauti kidogo. Hapa, uwezo wa kifedha mara nyingi hauishii kwa mhusika mmoja. Huendana na mafanikio ya familia yake, hujenga maisha ya wengine, na hubeba wajibu unaovuka kizazi kimoja.
Hili ndilo linalofanya mjadala wa uwezo wa kifedha nchini kuwa wa kipekee. Kadri uchumi wa Tanzania unavyoendelea kukua na fursa za biashara, uwekezaji na ajira zinavyozidi kupanuka, ndivyo pia kizazi kipya cha wafanyabiashara, wataalamu na wawekezaji kinavyoendelea kujenga mali na thamani kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, uchumi wa nchi yetu umeendelea kuonyesha uthabiti katika ukuaji katika miaka ya hivi karibuni, ukichochewa na uwekezaji endelevu na shughuli za sekta binafsi.
Hali hii imefungua nafasi mpya za kujenga uwezo wa kifedha, hasa kupitia biashara zinazo milikiwa na familia na uwekezaji wa muda mrefu. Lakini kadri uwezo huo unavyoongezeka, ndipo pia maswali muhimu yanavyoanza kuibuka.
Kwa Watanzania wengi, mafanikio hayapimwi tu kwa kile mtu alichojikusanyia. Mara nyingi huonekana kupitia watoto wanaosomeshwa, ndugu wanaosaidiwa, biashara zinazowapa wengine ajira, na uthabiti wa kifedha unaosaidia familia pana kusimama. Kwa lugha nyepesi, uwezo wa kifedha hapa huja na uwajibikaji.
Kwa miaka mingi, nguvu kubwa imewekwa kwenye kujenga. Kujenga biashara, kujenga kipato, kujenga usalama wa kifedha. Lakini sasa, swali kubwa zaidi si tena namna ya kuongeza uwezo huo, bali namna ya kuupangilia, kuuhifadhi, na kuurithisha kwa namna inayodumu.
Na hapa ndipo changamoto halisi ilipo. Biashara nyingi bado zinategemea sana mwanzilishi mmoja. Maamuzi mengi hubaki kwa mtu mmoja, mifumo ya kifedha huendelea kuwa ya kawaida au isiyo rasmi, na mipango ya urithi mara nyingi haipewi kipaumbele au kutokuwepo kabisa.
Hali hii huenda ikaonekana ya kawaida wakati biashara bado ipo katika hatua za mwanzo, lakini kadri biashara inavyokua na familia inavyopanuka, mazingira hayo huanza kuwa dhaifu zaidi.
Hatari kubwa si kutokuwepo kwa uwezo wa kifedha.
Hatari kubwa ni kutokuwepo kwa mwendelezo wake. Katika nchi nyingi barani Afrika, biashara nyingi za kifamilia zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya kuvuka salama kutoka kizazi cha kwanza kwenda kingine.
Sababu zake zinajulikana, ukosefu wa maandalizi ya mapema, mifumo dhaifu ya uongozi na umiliki, pamoja na kutokuandaliwa ipasavyo kwa kizazi kijacho kubeba wajibu huo.
Tanzania nayo haiko nje ya uhalisia huo. Wakati huo huo, kizazi kijacho tayari kipo mezani. Vijana wa familia nyingi za wafanyabiashara leo ni wasomi zaidi, wana mtazamo mpana zaidi wa dunia, na kwa kiasi kikubwa wanaanza kushiriki katika maamuzi ya biashara na uwekezaji.
Wanaleta mawazo mapya na mitazamo mipya, lakini pia wanahitaji mwongozo wa kuelewa kwamba, kusimamia uwezo wa kifedha ni jambo tofauti kabisa na kuutengeneza.
Kujenga mali kunahitaji bidii na uthubutu. Lakini kuisimamia, kuilinda na kuiendesha kwa mafanikio kunahitaji nidhamu, mpangilio, na mtazamo wa muda mrefu.
Ndiyo maana taasisi za kifedha nazo zinapaswa kubadilika kulingana na uhalisia huu. Huduma za kifedha za leo haziwezi tena kuishia kwenye miamala na bidhaa pekee. Zinapaswa kwenda mbele zaidi, kusaidia wateja kupanga uwezo wao kwa mtazamo mpana unaohusisha uendelevu wa mali, urathi, uandaaji wa kizazi kijacho, na ulinzi wa kile kilichojengwa kwa miaka mingi.
Katika mwelekeo huo, huduma za Stanbic Private Banking zimeendelea kujipanga kwa namna inayojibu mahitaji mapya ya wateja, si kwa kuangalia tu namna ya kukuza mali, bali pia namna ya kuipangilia, kuilinda na kuiwezesha kudumu kwa vizazi vijavyo.
Huduma za private banking mara nyingi hufikiriwa kama eneo linalohusu uwekezaji pekee au watu wachache wenye mali kubwa. Lakini kwa uhalisia, nafasi yake ni pana zaidi. Ni huduma inayosaidia wateja kukabiliana na changamoto zinazokuja kadri uwezo wa kifedha unavyokua.
Ni kuhusu kupanga umiliki, kuelewa wajibu wa familia, kuandaa warithi, na kuhakikisha kuwa mali haiwi mwisho wa safari bali mwanzo wa mfumo endelevu.
Na nchini Tanzania, mazungumzo haya yanaanza kuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Wateja wa leo hawaulizi tena tu namna ya kuongeza uwezo wao wa kifedha. Wanauliza pia namna ya kuudumisha. Hawaulizi tu wapi wawekeze, bali pia namna ya kupanga umiliki, kugawa majukumu, na kuhakikisha kuwa kile walichojenga hakipotei pindi kizazi kinapobadilika. Haya si maswali ya kawaida ya kifedha.
Ni maswali ya kina, ya kifamilia, na mara nyingi ya muda mrefu. Kuyajibu kunahitaji zaidi ya huduma za kifedha. Kunahitaji mazungumzo ya wazi, ushauri wa karibu, uaminifu, na mahusiano ya muda mrefu. Pia kunahitajika mabadiliko ya namna tunavyoutazama uwezo wa kifedha.
Uwezo wa kifedha haupaswi kuonekana kama mwisho wa safari, bali kama mfumo wa thamani. Mfumo unaosaidia familia kusimama, unaowezesha biashara kudumu, na unaochangia uthabiti mpana wa kiuchumi katika jamii.
Unapopangwa vizuri, utajiri huweza kufungua milango ya fursa kwa vizazi vingi. Usipopangwa, unaweza kupotea kwa haraka kuliko ulivyotengenezwa.
Baada ya kupokea tuzo tatu hivi karibuni zinazoitambua Stanbic Private Banking kama benki bora nchini katika kuhudumia wateja maalum, tunatambua kuwa mafanikio haya yanatokana si tu na ubora wa huduma za kifedha tunazotoa, bali pia na uwezo wetu wa kujibu mahitaji halisi ya wateja katika safari yao ya kujenga, kulinda na kuendeleza uwezo wao wa kifedha.
Huo ndio mwelekeo unaozidi kuwa muhimu Tanzania, ambapo uwezo wa kweli haujengwi kwa mtu mmoja tu, bali hubeba familia, huunganisha vizazi, na hujenga kesho ya wengi.
Beatrice Kisoka ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Maalumu wa Benki ya Stanbic.