Prime
UCHAMBUZI WA MAYALA: Aibu ya kusimuliwa na wageni
Moja ya picha ya matukio ya Oktoba 29 2025. Picha na Mtandao
Miaka michache iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan aliposhiriki katika utayarishaji wa filamu ya Royal Tour, nilikuwa miongoni mwa walioipongeza Serikali kwa ubunifu huo wa kuitangaza Tanzania kupitia utalii.
Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo, nilitoa ushauri mmoja muhimu; kwamba tusijivunie kufanyiwa kila jambo na wageni wakati tuna wataalamu, kampuni na wabunifu wa kutosha ndani ya nchi.
Nilipendekeza uwezo wa ndani ujengwe ili siku zijazo kampuni za Kitanzania ziweze kuandaa filamu za kiwango hicho. Zaidi, nilitamani kuona filamu kama hiyo ikitengenezwa kwa Kiswahili ili ihamasishe utalii wa ndani na kuwafikia Watanzania wengi zaidi. Hilo halikutokea.
Baadaye, wakati nchi ikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, niliandika tena nikizitaka mamlaka kuiwezesha sekta ya habari kuandaa vipindi vya elimu ya mpigakura na mijadala ya wagombea. Lengo langu lilikuwa kuwapa Watanzania fursa ya kuwafahamu kwa kina wagombea wote waliokuwa wakishiriki uchaguzi ili wapige kura kwa uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, badala ya mazoea au ushabiki wa kisiasa.
Wiki iliyopita nilipata mwaliko kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhudhuria uzinduzi wa filamu ya kumbukumbu inayochambua matukio yaliyotokea Tanzania Oktoba 29, 2025. Miongoni mwa wahusika wakuu wa filamu hiyo alikuwa Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.
Makala hii si tu ya kupongeza kwa uzalendo wake katika kusimulia kile kilichoonekana kuwa ukweli wa kilichotokea siku hiyo, bali pia ni nafasi ya kujihoji sisi wenyewe kama tasnia ya habari.
Inawezekanaje tukio kubwa lililotokea nchini mwetu likasimuliwa kwa kina zaidi na mwandishi kutoka nje ya Tanzania wakati vyombo vyetu vya habari na waandishi wetu walikuwapo?
Hapo ndipo ninapoona aibu yetu ilipo. Filamu hiyo imeandaliwa na mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka Nigeria, David Hundeyin, ambaye kwa sasa anafanya kazi zake nchini Ghana. Kupitia kazi yake yenye kichwa cha habari ‘What Happened on October 29?’ alijaribu kutoa simulizi tofauti na ile iliyotolewa na sehemu kubwa ya vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu matukio hayo.
Katika uchunguzi wake, Hundeyin alimtumia Balile kama chanzo muhimu cha taarifa. Kwa maoni yangu, Balile aliutendea haki wajibu huo kwa kueleza kwa kina mtazamo wake kuhusu chanzo na mazingira ya vurugu zilizotokea.
Hundeyin mwenyewe anasema simulizi iliyowasilishwa kwa ulimwengu ilikuwa rahisi mno ukilinganisha na uhalisia wa matukio hayo. Kwa mujibu wake, kulikuwa na wahusika wengine, maslahi mengine na mazingira mapana zaidi yaliyohitaji kufafanuliwa ili kuelewa kilichotokea.
Huo ndio msingi wa uandishi wa habari za uchunguzi; kutafuta yale ambayo hayakuonekana juu juu.
Lakini pamoja na kuthamini mchango wa Hundeyin, nilijikuta nikijiuliza swali moja kubwa. Kwa nini kazi hii imefanywa na mwandishi kutoka nje ya Tanzania?
Tunao waandishi wa habari za uchunguzi. Tunavyo vyombo vya habari. Tunazo kampuni za kutengeneza makala na filamu za kumbukumbu. Tunazo taasisi za habari zenye uzoefu wa kutosha. Kwa nini basi simulizi ya tukio kubwa la Tanzania liandikwe na kurekodiwa na mtu aliyelazimika kusafiri kutoka nchi nyingine kuja kutueleza sisi kilichotokea kwetu?
Katika mjadala uliofuatia onyesho la filamu hiyo, nilisema wazi kuwa sisi waandishi wa habari wa Tanzania tunapaswa kujisikia aibu. Sio kwa sababu mgeni ameandika habari kuhusu Tanzania, bali kwa sababu aliandika habari ambayo sisi tulipaswa kuwa wa kwanza kuiandika.
Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba vyombo vya habari navyo ni sehemu ya sababu zilizoruhusu baadhi ya mambo kutokea jinsi yalivyotokea. Kama tungetimiza wajibu wetu kikamilifu wa kutoa elimu kwa umma, kuchochea mijadala ya sera, kuuliza maswali magumu na kuwapa wananchi taarifa za kutosha, huenda baadhi ya matukio yangekuwa na sura tofauti.
Cha kusikitisha zaidi ni kwamba hata baada ya matukio hayo kutokea, bado hatujaonyesha ari ya kutosha kuyachunguza kwa kina na kuyaeleza kwa dunia kwa mtazamo wetu wenyewe.
Miongoni mwa wageni walioandamana na Hundeyin alikuwa Profesa, Joshua Maponga wa Zimbabwe, mmoja wa watetezi wa falsafa ya Pan-Africanism. Katika mazungumzo yake, alisisitiza umuhimu wa Waafrika kutafuta suluhisho la matatizo yao kwa kutumia maarifa, historia na mifumo yao wenyewe.
Ninakubaliana naye kwa kiwango kikubwa. Baadhi ya changamoto zinazolikabili bara la Afrika zinatokana na kuendelea kutegemea mifumo ya kiutawala tuliyorithi kutoka kwa wakoloni bila kujiuliza kama inakidhi mazingira yetu ya sasa.
Lakini somo kubwa nililoondoka nalo siku hiyo halikuwa la siasa wala la historia. Lilikuwa somo la wajibu.
Kama tunataka dunia iisikie Tanzania kwa sauti ya Watanzania, basi ni lazima sisi wenyewe tuwe tayari kusimulia hadithi zetu. Tusisubiri wageni waje kutueleza tulichokiona, tulichokipitia na tunachokifahamu.
Mungu ibariki Tanzania.