Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tujiandae na athari za mzozo wa Iran, Israel

Mvutano kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, licha ya kuonekana mbali na Bara la Afrika, unaanza kuleta athari za kiuchumi ikiwamo kupanda kwa bei ya mafuta na gesi ya kupikia, hali inayoweza kuathiri maisha ya wananchi na uchumi wa nchi nyingi zinazoagiza nishati hiyo, ikiwamo Tanzania.

Tayari dalili za mabadiliko hayo zinaanza kuonekana katika soko la dunia, ambapo bei ya mafuta imepanda kutoka karibu dola 70 hadi kufikia takribani dola 100 kwa pipa, huku kukiwa na hofu kwamba inaweza kufikia dola 120 endapo hali ya vita itaendelea au kuongezeka.

Hofu hiyo inachangiwa zaidi na hatari ya kuvurugika kwa usafirishaji wa mafuta kupitia Lango la Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta yanayosambazwa duniani.

Tanzania, ambayo hutegemea uagizaji wa mafuta kutoka nje, hali hiyo inapaswa kuchukuliwa kama tahadhari kwa kudhibiti moja kwa moja bei ya mafuta katika soko la dunia kwa kuwa haizalishi nishati hiyo.

Hata hivyo, athari zake huingia kwa kasi katika uchumi wa ndani kupitia kupanda kwa gharama za usafiri, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa.

Ni ukweli usiopingika kwamba mafuta yanapopanda bei, gharama za maisha pia hupanda. Sekta ya usafirishaji huwa ya kwanza kuathirika kwa sababu magari ya abiria na mizigo hutegemea nishati hiyo. Pia, nauli za mabasi, daladala na usafiri wa mizigo hupanda, hali inayoongeza gharama za kupeleka bidhaa sokoni.

Athari kubwa zaidi hujitokeza katika bei za vyakula, hususan katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Mazao yanayotoka katika maeneo ya uzalishaji husafirishwa kwa magari yanayotumia mafuta. Gharama za usafiri zinapoongezeka, bei za vyakula pia hupanda. Hali hiyo inaweza kuathiri hata maeneo ya pembezoni ambako baadhi ya mahitaji ya msingi hayazalishwi na hulazimika kuletwa kutoka mbali.

Hivyo, ni muhimu kwa Serikali na wananchi kuanza kujipanga kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza. Kwa upande wa Serikali, mojawapo ya hatua zinazoweza kusaidia ni kuangalia uwezekano wa kupunguza baadhi ya kodi na tozo zinazotozwa kwenye mafuta ili kupunguza mzigo kwa walaji.

Aidha, Serikali inaweza kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku kwa muda katika mafuta au gesi ya kupikia, hasa katika kipindi ambacho soko la dunia linakuwa na msukosuko mkubwa.

Hatua kama hizo ziliwahi kuchukuliwa nchini Tanzania mwaka 2022, wakati Serikali ilitoa ruzuku ya zaidi ya Sh100 bilioni kupunguza makali ya kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia msukosuko wa soko la dunia uliosababishwa na Vita vya Urusi na Ukraine. Ruzuku hiyo ilisaidia kupunguza bei ya petroli na dizeli na kupunguza athari kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wa wananchi, ni muhimu kuanza kuzingatia matumizi ya nishati kwa uangalifu zaidi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Kutokana na hali ilivyo, juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama gesi asilia na vyanzo vingine vya ndani zinapaswa kupewa kipaumbele.

Kwa jumla, kupanda kwa bei ya mafuta kuna athari pana katika uchumi, hivyo tahadhari na maandalizi ya mapema ni muhimu kulinda uchumi na ustawi wa wananchi.