Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tufanye haya kukuza umilisi wa Kiingereza shuleni



Dar es Salaam. Katika dunia ya leo iliyounganishwa kwa kasi na teknolojia, lugha ya Kiingereza imekuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano, elimu, biashara na ubunifu. 

Ni lugha inayotumika katika kazi nyingi za kitafiti na za kisayansi, majukwaa ya kimataifa na mifumo ya elimu katika nchi nyingi, ikiwemo Tanzania. 

Hata hivyo, pamoja na umuhimu wake mkubwa, ukweli unaobaki ni kwamba wanafunzi wengi katika ngazi mbalimbali za elimu wanapata changamoto kubwa kuimudu lugha hii.

Kwa muda mrefu, wanafunzi wamekuwa wakisoma Kiingereza kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu. Lakini bado idadi kubwa ya wahitimu hushindwa kuwasiliana kwa ufasaha, kuelewa maandiko ya kitaaluma, au hata kujieleza kwa ujasiri katika mazingira ya kawaida. Hali hii inaonyesha kuwa kuna tatizo la msingi katika namna lugha hii inavyofundishwa na ujifunzaji wake.


Changamoto iliyopo

Kwa wanafunzi wengi, Kiingereza si tu somo gumu bali ni kikwazo kinachowazuia kufikia mafanikio yao ya kielimu. 

Lugha hii huanza kuwapiga chenga tangu wakiwa shule za msingi, ambapo msingi wa kujifunza haujengwi ipasavyo. Wanafunzi hukariri maneno na sheria za sarufi bila kuelewa matumizi halisi ya lugha katika maisha ya kila siku.

Wanapoendelea na elimu ya sekondari, changamoto huongezeka. Masomo mengi huanza kufundishwa kwa Kiingereza, hali inayowafanya  kushindwa kuelewa maudhui ya masomo si kwa sababu ni magumu, bali kwa sababu ya lugha inayotumika. Mwanafunzi anaweza kuwa na uwezo mzuri wa kufikiri lakini akashindwa kuonyesha uwezo huo kwa sababu ya ukosefu wa umilisi wa lugha.

Katika ngazi ya elimu ya juu, hali hii huwa dhahiri zaidi. Wanafunzi wengi hushindwa kuandika ripoti za utafiti, kuwasilisha hoja zao darasani, au kushiriki mijadala ya kitaaluma kwa ufanisi. Hii si kwa sababu hawana maarifa, bali kwa sababu lugha imekuwa kizuizi.

Athari za hali hii ni kubwa. Wanafunzi hupoteza kujiamini, hushindwa kushindana katika soko la ajira, na mara nyingi hukosa fursa muhimu za maendeleo.

 Aidha, taifa hupoteza rasilimali watu wenye uwezo ambao ungeweza kutumika kuleta maendeleo endapo tu wangewezeshwa kumudu lugha ya Kiingereza.


Umuhimu wa Kiingereza 

Ni muhimu kutambua kuwa Kiingereza si tu lugha ya darasani bali ni lugha ya kimataifa inayofungua milango ya fursa. Inatumika katika biashara za kimataifa, teknolojia, sayansi, utalii, na hata diplomasia. 

Mtu anayemudu Kiingereza ana nafasi kubwa zaidi ya kupata taarifa, kushirikiana na watu kutoka mataifa mbalimbali, na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia.

Kwa mfano, tafiti nyingi za kisayansi huandikwa kwa Kiingereza. Hivyo, mwanafunzi au mtafiti asiyeimudu lugha hii hukosa fursa ya kupata maarifa mapya au kuchangia katika uzalishaji wa maarifa hayo. 

Vilevile, kampuni nyingi za kimataifa hutumia Kiingereza kama lugha ya kazi, jambo linalomaanisha kuwa umilisi wa lugha hii ni sifa muhimu katika ajira nyingi.

Katika zama za kidijitali, ambapo mawasiliano hufanyika kupitia mitandao na majukwaa mbalimbali, Kiingereza kinazidi kuwa muhimu zaidi.

 Kuimudu lugha hii kunamwezesha mtu kujifunza kwa kujitegemea, kufuatilia maendeleo ya dunia, na kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na teknolojia.


Njia za kukuza umilisi wa Kiingereza

Ili kukabiliana na changamoto hizi, ni lazima kubadili namna tunavyofundisha na kujifunza Kiingereza. 

Mfumo uliopo kwa kiasi kikubwa umejikita katika kufundisha sarufi na miundo ya lugha kwa nadharia zaidi kuliko matumizi halisi ya lugha. 

Hii imewafanya wanafunzi wengi kujua sheria za lugha lakini washindwe kuitumia katika mawasiliano ya kila siku.

Ni muhimu kuhamia katika mbinu za kimawasiliano zaidi. Hii ina maana kuwa wanafunzi wanapaswa kupewa nafasi ya kuzungumza, kusikiliza, kusoma na kuandika kwa vitendo. 

Mazingira ya darasani yanapaswa kuhamasisha matumizi ya lugha badala ya kukariri kanuni zake.

Walimu wanapaswa kubuni mbinu shirikishi za kufundisha, kama vile mijadala, mawasilisho, michezo ya kuigiza, na kazi za vikundi.

 Mbinu hizi huwasaidia wanafunzi kutumia lugha katika muktadha halisi na hivyo kujijenga kwa ufanisi zaidi. Aidha, matumizi ya teknolojia kama video, sauti na programu za kujifunzia lugha yanaweza kuongeza ufanisi wa ujifunzaji.

Pia, ni muhimu wanafunzi kuhamasishwa kujifunza nje ya darasa. Kusoma vitabu, kuangalia vipindi vya televisheni, kusikiliza redio au podikasti kwa Kiingereza kunaweza kusaidia sana kukuza umilisi wa lugha. 

Kadri mwanafunzi anavyokutana na lugha katika mazingira tofauti, ndivyo anavyoizoea na kuimudu zaidi.

Zaidi ya yote, tunapaswa kubadili mtazamo kuhusu kujifunza Kiingereza. Badala ya kuona kama somo la kufaulu mtihani, tunapaswa kukiona kama chombo cha mawasiliano na maendeleo. Hii itawasaidia wanafunzi kujifunza kwa motisha ya ndani badala ya kulazimishwa na mfumo wa mitihani.

Kwa ujumla, changamoto ya umilisi wa Kiingereza si tatizo la wanafunzi pekee bali ni matokeo ya mfumo mzima wa elimu. Ili kuleta mabadiliko ya kweli, ni lazima tubadili mbinu za ufundishaji, tuweke mkazo katika mawasiliano, na tutumie teknolojia kwa ubunifu. Tukifanya hivyo, tutawawezesha wanafunzi wetu si tu kufaulu mitihani bali pia kutumia Kiingereza kwa ufanisi katika maisha yao ya kila siku na katika dunia inayozidi kuwa ya kimataifa.