Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAAMULI HURU: ‘No reforms’ ya Chadema ni mpango wa Mungu au shetani?

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alivyowasili Ndanda mkoani Mtwara Aprili 5, 2025 kuendelea na operesheni No Reforms, No Election.

Leo nitajadili kitu kinachoitwa kwa Kiingereza ‘holistic approach’, kwa kutumia dhana dhanifu ya imani kuwa Mungu ndiye muumba wa mbingu na nchi na vyote vilivyomo ndani yake, wakiwemo viumbe wote na sisi binadamu na kila kinachotokea duniani.

Jambo lolote ni ama ni mpango wa Mungu ama wa Shetani. Japo nchi yetu haina dini na Serikali yetu haina dini, lakini wananchi wake wana dini zao, ndio maana viongozi wetu tukiwachagua, tunawaapisha kwa mujibu wa imani za dini zao.

Mpango wa Mungu katika kumuumba binadamu ni ili amche Mungu na kutenda yalio mema, mambo yote mema na mazuri ya neema ya kheri ni rehema za Mwenyezi Mungu, hivyo tunaita ni mpango wa Mungu na mambo yote mabaya, maovu yakiwemo majanga na dhambi zozote ni mpango wa shetani.

Mungu ndiye huweka Serikali za Mataifa, hivyo viongozi wote wa nchi ni mpango wa Mungu wanapaswa kuwaza kusema na kutenda mema, viongozi wanapotenda maovu kwa nchi na wananchi wak, wanageuka mawakala wa shetani.

Kuna wakati Mungu anamruhusu shetani kutenda mambo mabaya, kuleta majanga hadi vifo ambayo tunaita ni mapito, majaribu na mitihani ya Mwenyezi Mungu ili kukupima umesimamaje.

Anakupitisha kwenye tanuru la moto kukuimarisha kukuandaa kwa majukumu makubwa zaidi, hivyo jambo lolote zuri au baya likitokea, japo linasababishwa na shetani, tunatakiwa kushukuru Mungu kwa yote kwa sababu Mungu ndiye Alfa na Omega, ameruhusu hayo yatokee.

No reforms, no election

Inawezekana ajenda ya Chadema ya No reform, no election ni mpango wa Mungu kwa Tanzania kuzirejesha zile haki mbili kuu za msingi za kikatiba, haki ya kuchagua na haki ya kuchaguliwa zilizoporwa kwenye Katiba yetu, au ni mpango wa shetani kukisambaratisha Chadema kwa kutaka kuzuia uchaguzi mkuu.

Kwa kutumia mtindo wa “kukinukisha”, kitu ambacho hakiwezekani, Chadema inakusudia kuzuia uchaguzi mkuu, na ikifanya hivyo itakosa ruzuku na kujifia kifo cha kawaida.

Mwasisi wa No reforms, no election ni mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe na aliiasisi ajenda hiyo kufuatia kuvunjika kwa mazungumzo ya maridhiano na CCM, akasema bila mabadiliko, uchaguzi hautafanyika.

Baada ya Mbowe kushindwa kwenye uchaguzi wa ndani na Tundu Lissu kushika usukani, aliibeba ajenda hiyo ya Chadema kwa ahadi ya kufanya maandamano nchi nzima siku ya uchaguzi ili kuzuia uchaguzi usifanyike kwa mtindo wa kukinukisha.

Kauli za Lissu zimetisha na kutingisha, na kusababisha kujibiwa na viongozi waandamizi wa CCM, alianza Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, akafuatia Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, Rais Samia akatoa hakikisho la milango ya majadiliano iko wazi, na juzi Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akasisitiza kwamba ruksa Chadema kugomea uchaguzi, wasilazimishwe lakini wasiwazuie wengine kushiriki.

Masikini viongozi wa CCM hawajui kuwa kila wanapolizungumzia hili, ndio wanachochea moto na kulipa umaarufu, sasa linarindima, kama wangelipuuzia, wala lisingevuma kiasi hiki.

Kulikoni Lissu?

Lissu ni mpango wa Mungu kwa Tanzania ndio maana akapona kimiujiza kwenye lile shambulizi la risasi 16, hivyo ameponywa kwa makusudi fulani ili Mungu kumtumia kuonyesha utukufu wake kwa binadamu?

Hata ushindi wa Lissu dhidi ya Mbowe kwenye uchaguzi wa ndani wa Chadema ni mpango Mungu, hivyo Chadema pia ni chama mpango wa Mungu? Kupitia kwake, inawezekana Mungu anakwenda kufanya jambo kwa Tanzania, kwa kulifanya lile jiwe walilolikataa waashi, litafanywa kuwa jiwe kuu la pembeni? Au Lissu ni agenti wa shetani anayetumiwa kukisambatisha Chadema bila kujijua?

Unaweza kususa kushiriki uchaguzi kwa sababu huko huru kushiriki uchaguzi au usishiriki,lakini huwezi kuwazuia wengine kushiriki uchaguzi, ni madness lakini kitendo cha kusema utazuia uchaguzi usifanyike kwa kukinukisha huku ni kumtumikia shetani na kuwa ajenti wa shetani.

Inawezekana No reforms, no election ni mpango wa Mungu kwa Tanzania anaoletwa kwa mtindo wa baraka ili mabadiliko hayo yaondoe ule ushetani uliofanywa kwenye katiba yetu, hivyo Chadema ni mpango wa Mungu na Lissu ni mpango wa Mungu kuwakomboa Watanzania kurejeshewa haki zao zilizoporwa?

Kipimo cha mwisho cha No reforms, no election na Lissu kama ni mpango wa Mungu au wa shetani, tutakipima kwa matokeo ya mwisho, kama ni mpango wa Mungu, basi Mungu atatenda kuwezesha mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu na Tanzania itafanya uchaguzi mkuu huru, wa kweli na haki.

Kama uchaguzi utafanyika, basi kwa Lissu, Chadema na wafuasi wao hawatakuwa mpango wa Mungu kwa kuwa uchaguzi utafanyika na wananchi watashiriki kikamilifu kuchagua viongozi wao katika ngazi zote.

Kama ni mpango wa shetani, hakutafanyika mabadiliko yoyote, na uchaguzi utafanyika kama kawaida, huo mpango wa kuzuia uchaguzi mkuu utashindikana na mipango ya maajenti wa shetani, washindwe na walegee. Mungu Ibariki Tanzania.