Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Ukimchunguza bata hutamla asilani

Kuna mwanamuziki nguli kutoka kule kunakovutwa bangi hadi zikaota vichwani alihojiwa na chombo cha habari cha kimataifa. Akasema ati alikataa kusoma sana kwa kuogopa kugeuka mjinga! Kila mmoja akajua hapa haongei mtu ila bangi. Wenzake wanakimbilia elimu ya juu ili kuongeza uwezo, halafu yeye anaikataa kwa madai ati zitamtoa ufahamu. Lakini yeye alilipigia mstari hilo.

Swahiba wangu mmoja kutoka chama hilohilo la ganja alimtetea kwa kutoa mifano, akasema mtu aliyesoma sana anapunguza uwezo wake wa ubunifu. Kwenye masomo yake atakuta kwamba biashara haiwezi kufanyika bila mtaji, bima, usafiri, ghala, matangazo na akiba ya dharura. Hatajua namna ya kujiongeza. Lakini asiyesoma atachukua maamuzi magumu kuliko kujinyonga. Ataingiza hadi senti yake ya mwisho kuagiza lori la nyanya bila kuwaza ajali.

Aliongeza kuwa ukiumwa sikio, atakudondoshea tone la “mjani” na utapona papo hapo. Lakini daktari bingwa atapoteza mwezi mzima kulichunguza sikio. Mwisho wa siku atagundua kuwa sikio zima lina matatizo, atakupeleka kwenye upasuaji na sasa utakuwa mgonjwa wa ukweli. Mambo gani haya ya kupasuana na kushonana kama nguo! Kwa mbali nilimsoma, ingawaje sikutaka kumkubalia kwa sababu zinazoeleweka.

Nilivuta kumbukumbu siku niliyotembelewa na mtoto wa tajiri mmoja mwenye elimu yake. Tajiri huyu alimleta mwanaye kwangu baada ya kumfanyia kazi aliyoishindwa mwanaye pamoja na kuisomea. Huyu mtoto wake alikuwa ameshapanda vidato vyote ndani na nje ya nchi, lakini bado aliendelea kusoma kwa kina zaidi. Yote kwa yote ilibidi aletwe kwa Mlevi kufundishwa mautundu.

Mzee aliniambia atampitia akitoka kazini saa kumi, hivyo saa nane mida ya lanchi nikaenda kubonyea naye kwa mama ntilie. Dogo hakuamini mazaga aliyoyaona pale; machopchop, mahanjumati, mavitoga kama yote! Alikula hadi akaramba sahani. Akashushia na kombe la maji ya kisima na kusema hakuna siku aliyokula mseto mzito kama huo. Baada ya misosi tukarudi zetu golini na somo likaendelea.

Mzee alirudi pale saa kumi kama alivyoahidi. Lakini kabla ya yote alimuuliza mwanaye alikula wapi. Dogo akaelekeza niulizwe mimi maana yeye hapajui. Nilimwambia mzee kuwa ninaye mama lishe mtundu sana kwa vyakula vya kihindi pale bondeni. Dakika hiyohiyo nikamwona mzee akichanganyikiwa. Haraka akamtia dogo garini na kumkimbiza mjini akachekiwe na daktari! Ama kweli gari jipya haliwekwi oili ya kale.

Utagundua kuwa gari la fundi huwa bovu pale linapokosa mafuta tu. Vinginevyo litapuyanga hata kama halina breki na plagi zinatema cheche. Hata ununue gari mpya leo, ukienda kuifanyia vipimo utagundua halipo sawa. Au nenda wewe mwenyewe Hospitali wakucheki, utashangaa ulikuwa unatembeaje wakati mwili wako wote ni mbovu. Utakutwa na shinikizo la damu, sukari, malaria, UTI na mambo kadha wa kadha.

Unajua kwa nini watu wote wana maradhi yanayofanana? Mimi nadhani kwa kiasi fulani mtindo wa maisha ya kileo unafanana kwa wote; masikini na matajiri. Sote tunavuta hewa iliyochafuliwa na pilika za kibinadamu, tunakula mazao ya mbegu zisizo za asili, mafuta yenye lehemu, kuku, nyama na mboga zinazokuzwa kwa madawa. Tusiongopeane kuwa yupo anayepikia mafuta ya ufuta au alizeti kutoka shamba.

Wasomi wa vyakula wametufundisha ulaji mzuri, lakini sasa nao wanatuchanganya. Mara wanatuambia tunywe maji mengi kadiri tunavyoweza, hapohapo tunaambiwa unywaji wa maji mengi ni hatari. Walituachisha maji ya kisima kwa kudai yana bakteria wasiokufa hata maji yanapochemshwa, kisha wakasema maji ya viwandani yanaacha kemikali za madawa miilini mwetu. Tufanyeje sasa? Tukinywa maji ya dafu watatuambia nayo yakizidi ni noma.

Walituambia tule milo kamili mitatu kwa afya bora. Lakini sasa wanasema ikiwezekana tule mlo mmoja na usiwe na protini, mafuta wala wanga. Ina maana ugali kuku, nyama, samaki au hata wali rosti sasa usikie redioni tu. Sasa tule nini? Tukila maembe na mapapai yatachunguzwa na kuonekana yana wadudu.

Kama ni kweli, hivi wazee wetu si wangelikufa wangali vijana? Watoto wa mjini tunasema ugali hauna fomula, ukishapakuliwa ndio mboga inafikiriwa. Kadhalika wazee wetu walienda shamba na jembe bila jiko. Hukohuko ndiko kulipatikana chakula kama ni muhogo mbichi, maembe au kinginecho. Sasa hao wadudu hawakuwepo? Tena wazee hawakuwa na muda wa kutafuta maji ya kuoshea hivyo vyakula.

Wakati mwingine ubovu ni sehemu ya maumbile. Huwezi kula muwa bila kukuta fundo kwa maana pingili ni sehemu ya muwa huo. Siku moja niliperuzi mtandaoni nikakuta maelekezo bora ya kuandaa chakula. Wanasema ukikata nyanya zisikae dakika mbili kabla ya kuingizwa jikoni. Lakini mara tu utakapomaliza kuzikata, ukioshe kisu chako vizuri kabla ya kukata kitunguu kisije kuambukizwa wadudu!

Daktari mmoja anasema tuogope juisi za chupa kama homa ya nyani, lakini huyohuyo akatuonya kunywa juisi ya kukamua kwani inabeba vijidudu visivyoonekana. Lakini wataalamu wanakiri kuwa ni lazima mtu awe na minyoo kwa ajili ya kumeng’enya chakula. Hakuna mtu anayekosa sukari mwilini mwake, sema ikizidi au kupungua ndio unakuwa ugonjwa. Nimuunge mkono kwa kusisitiza kila kinachozidi au kupungua mwilini huleta madhara.