Mema ya mwezi mtukufu wa Ramadhani yadumishwe

Muktasari:
- Katika mwezi huu, kama ilivyokuwa miaka iliopita watu wengi wa visiwani walionekana kubadili mwenendo wao wa maisha na tabia.
Baada ya siku chache mwezi mtukufu wa Ramadhani utamaliza safari yake na ukiacha kumbukumbu zilizobadilisha maisha ya kawaida ya watu wa Zanzibar.
Katika mwezi huu, kama ilivyokuwa miaka iliopita watu wengi wa visiwani walionekana kubadili mwenendo wao wa maisha na tabia.
Mtu ambaye alikuwa ndio kwanza amefika Zanzibar katika mwezi huu angeshangazwa kwa kuona upole, ukarimu, wema na ihsani ya watu wa visiwani hapa kwa namna wanavyopendana na kusaidiana.
Watu wengi wenye uwezo mzuri wa maisha walijitolea kwa hali na mali kusaidia wenye maisha magumu.
Katika mwezi huu watu walibadilishana sahani za vyakula na wengine kutoa misaada ya chakula, mavazi na pesa kuwapa wanyonge mitaani, madukani, katika nyumba za ibada na hata vijiweni.
Hakuna wakati ambapo watu wenye mazingira magumu ya maisha, mahitaji maalumu, mayatima, vizuka (wajane) na watu wenye ulemavu ambapo walipata msaada mkubwa kama katika mwezi huu.
Ndio maana watu wenye maisha magumu husubiri kwa hamu mwezi wa Ramadhani ufike kwani huwa ni wakati wa kupata faraja.
Taasisi nyingi za Serikali na za watu binafsi waliwafanyia futari zilizowakutanisha walionacho na wale hohehahe na hapo kutolewa misaada kwa maskini.
Mwenendo huu uliwapunguzia unyonge watu maskini na wengine kuonja vyakula ambavyo katika miezi yote iliyopita kabla ya mwezi wa Ramadhani waliviona tu na kuvisikia na sio kufurahia ladha yake.
Hata matumizi ya lugha chafu na maneno yaliokosa staha na busara kwenye masoko, vijiwe na mitaani yalipungua sana.
Lakini uzoefu umeonyesha mara tu unapomalizika mwezi huu watu wengi wenye hali ngumu wamejikuta tena kuwa na shida ya kupata msaada kama tulivyoshuhudia wakati wa mwezi wa Ramadhani.
Ni vizuri watu wa Zanzibar wakatafakari juu ya umuhimu wa ukarimu na kusaidiana kuendelezwa, ijapokuwa itakuwa kidogo taabu kama walivyofanya katika huu mwezi unaoitwa wa ibada na misaada.
Mwenendo wa kupitia nyumba za wazee, watu ambao ni wajane walioachiwa mzigo wa kulea watoto katika hali ngumu na kuwasaidia mayatima kupata chakula na elimu unapaswa kuendelezwa.
Mahitaji ya watu wanaoishi katika mazingira magumu ni ya kila siku na sio ya msimu kama wa mavuno ya mpunga au karafuu.
Ni vizuri kwa watu wenye kipato kizuri ambao walitoa futari katika maeneo mbalimbali wakaendeleza mwenendo wa kusaidia wenye shida.
Wapo ambao wanahangaika kupata visaidizi vya kutembelea, kama vigari na juhudi zao za muda mrefu zimegonga ukuta na wengine wanahitaji matibabu, lakini hawana pesa za kuwasaidia kuzipata huduma wanazozihitaji.
Hawa wanahitaji msaada na nguvu za pamoja za watu wenye uwezo mzuri wa kimaisha utawasaidia kutokana na unyonge waliokuwa nao.
Ni kweli ni taabu kuyamaliza matatizo yote ya watu waliomo katika makundi haya, lakini kuuendeleza mfumo wa maisha tuliouona mwezi wa Ramadhani utasaidia kupunguza na idadi ya watu waliolazimika kuwa ombaomba Visiwani.
Kama watu na taasisi zilijitolea kwa hali na mali kutoa misaada katika mwezi wa Ramadhani wataendelea kutupia jicho la huruma kwa watu hawa, badala ya kungojea mwezi huo mtukufu wa mwakani kutoa misaada, maisha ya watu wanaoishi katika mazingira magumu Zanzibar yatabadilika.
Kwa bahati mbaya watu wengi wamejenga dhana kuwasaidia watu wenye shida ni kama kufanya wema, lakini maamrisho ya dini zote yanamtaka kila mwenye uwezo kufanya hivyo.
Tusingojee kuombwa na kubembelezwa kuwasaidia wazee wasiojiweza, mayatima, wajane, vizuka na watu wenye ulemavu.
Kuwasaidia watu wenye shida ni wajibu wa kila mwenye uwezo kwani hali ngumu ya maisha waliokuwa nayo watu hawa sio ya kujitakia bali ni majaaliwa.
Ni vizuri kuona kuwasaidia maskini na wasiojiweza ni wajibu wa kila alichokuwa nacho kutoa japo kidogo ili na wao wajione wanafurahia maisha kama watu wengine. Huu sio mzigo wa Serikali, bali wa kila mwanajamii.
Mazingira ya wema na ukarimu tuliyoyaona mwezi wa Ramadhani Zanzibar ambayo yaliwapa wanyonge furaha na faraja yanapaswa kuwa endelevu ili kuipa Zanzibar sura nzuri.
Dini zote zinaelekeza aliyekuwa nacho kumsaidia aliyekuwa hana. Tutekeleze wajibu huo kuanzia wakati wa sherehe za Idd el Fitr baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhani.