Mafisadi wawajibishwe, siyo kukemewa pekee
Picha na Akili Unde.
Kwa mara nyingine tena, Zanzibar zimesikika kauli za kusikitisha za mafisadi kutumia nyadhifa na mamlaka zao walizopewa katika serikali kujinufaisha kwa kudhulumu watu, wengi wao wakiwa wanyonge.
Kilio cha sasa ni cha baadhi ya watumishi wa serikali kudaiwa kuchota fedha za malipo ya fidia kwa nyumba, mashamba na miti ili kuwezesha utekelezaji wa miradi inayoendelea sehemu mbali za Zanzibar.
Miradi hii ni pamoja na ujenzi wa barabara, hospitali, vituo vya afya, shule, nyumba za makazi ya kwa wafanyakazi wa taaasisi mbalimbali.
Tumeelezwa kwamba baadhi ya maofisa na wafanyakazi waliokabidhiwa mamlaka ya kulipa fedha za fidia wamejichota kwa raha zao kama vile ni mali waliyorithishwa na wazazi wao.
Baada ya kusikika malalamiko ya baadhi ya watu kutolipwa na wengine kupata kidogo kuliko walichostahili, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliunda tume iliyochunguza na kufanya tathmini ya fidia iliostahili kulipwa kwa watu waliopisha ujenzi wa miradi na ripoti yake tayari ameshakabidhiwa.
Hii ni hatua ya kupongezwa kwa vile ndicho kinachostahili kufanywa na Serikali iliuyoahidi utawala bora, wa haki na wenye kufuata sheria.
Lakini hatua inayofaa kufuata ni kwa hiyo ripoti kuwekwa wazi ili wananchi wajue nini hasa kilitendeka, nani walihusika na huu ufisadi na hatua gani za kisheria zilifuata.
Hii ni muhimu kwa sababu katika siku siku 100 za kwanza za uongozi wake baada ya kuingia madarakani Novemba 2020, Rais Mwinyi alifanya ziara za kushitukiza sehemu mbalimbali na kugundua ufisadi ambao maelezo yake yalishangaza na kushitua.
Katika orodha ya madudu yaliyogunduliwa ni kuwepo kwa mamia ya wafanyakazi hewa katika taasisi za Serikali na hasa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Mengine yaliyogundulika katika kile kilichoelezwa kama uoza wa rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali ni uwepo wa bwawa la kufugia vifaranga vya samaki liliogharimu mamilioni ya shilingi ambalo lilikuwa na vifaranga vilivyohesabika vidoleni na majongoo matatu ya pwani.
Vilevile, aligundua fedha za kununulia magari ya kusombea taka zilitumika kununua magari ya kifahari ya viongozi.
Hii ilisababisha kuundwa tume kama aliyoiunda karibuni na kuwasilisha ripoti, lakini kwa bahati mbaya kilichokuwemo ndani hakijulikani vema. Baada ya kutolewa kwa ripoti ile wapo viongozi waliowekwa pembeni ili kupisha uchunguzi.
Sasa yameibuka mengine kama yale, lakini hili limewagusa zaidi baadhi ya wananchi moja kwa sababu fedha za fidia ambazo zingewasaidia kujenga nyumba nyingine au kufanya matengenezo hawakupewa.
Lakini tumesikia kuwa wapo watu ambao walipewa hizi fedha wakati hawakupoteza hata bustani ya nyanya wala bamia. Kama hili lilifanyika, basi ni wizi na ufisadi.
Katika kuendesha shughuli za serikali, Rais Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kuwepo uwazi na kueleza kwamba hatakuwa na muhali na kiongozi yeyote atayeficha habari na yule atakayefanya hivyo aelewe kuwa kazi imemshinda na atamuweka pembeni.
Alisema bila ya kutafuna maneno kuwa ni haki ya wananchi kujua kinachofanyika katika serikali yao na kuwataka viongozi wavione vyombo vya habari sio madui, bali washirika wa maendeleo.
Kwa bahati mbaya, vikao hivi havifanyiki na unapoitishwa mkutano wa waandishi wa habari, basi huwa wa wateule maalumu na sio wote.
Ni vizuri hata Rais Mwinyi akafikiria kurejesha utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari aliokuwa akifanya kila mwezi na kama itaonekana tabu, basi angalau kila baada ya miezi mitatu. Vikao hivi vinasaidia kuibua yaliyojificha au yanayofunikwa kawa.
Ni vizuri uwazi aliousisitiza Rais Mwinyi ukaongezwa kasi na hili la fedha za malipo ya fidia kutumika vibaya linapswa kushughulikiwa vema ili umma uone sheria inafuata mkondo wake na hakuna aliyekuwa juu ya sheria.
Kwa kufanya hivyo, umma utazidi kuwa na imani na serikali na kuona hakuna mwenye haki ya kudhulumu au kutumia vibaya fedha za umma.
Hii pia itahakikisha kwamba Mahakama zetu hazikuwekwa kwa wizi wa nazi na maandazi tu, bali hata viongozi wanaotumia vibaya madaraka na mamlaka waliyokuwa nayo.
Hili halifai kufanyiwa mzaha kwani muhali unaotokana na kujuana na tabia ya kulindana kwa maovu na sio kwa mema, utaendelea kuiathiri Zanzibar na watu wake kama tutafumbia macho maovu kutokana na muhali tuliokuwa nao.
Tuwalinde kwa nguvu zote viongozi waadilifu na tusiwakumbatie wale amabao wanatumia vibaya madaraka kudhulumu watu na kufisidi uchumi wa nchi yetu.
Mjenga nchi ni mwananchi mwenye kuipenda nchi yake na anayeifisadi nchi ni mwananchi aliyeweka mbele rushwa na ufisadi.