La ‘plea bargain’ ni tone la maji baharini

Muktasari:

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kicheere anaendelea kuzikagua fedha zilizotokana na adhabu ya plea bargain ambayo inawaruhusu washitakiwa kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kukiri makosa waliyonayo ili walipe faini.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kicheere anaendelea kuzikagua fedha zilizotokana na adhabu ya plea bargain ambayo inawaruhusu washitakiwa kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kukiri makosa waliyonayo ili walipe faini.

CAG Kichere amenukuliwa na kituo cha runinga cha Azam akisema mpaka Machi mwakani, atamkabidhi Rais ripoti ya uchunguzi wa bakaa ya fedha zilizokusanywa kwa utaratibu huo ambazo ni zaidi ya Sh51 bilioni.

Kuikamilisha taarifa hiyo, CAG amesema anawahoji watu waliotajwa kuhusishwa katika sakata hilo kuanzia ngazi ya kata, huku kukiwa na madai ya baadhi ya fedha zilizokusanywa kutoingizwa serikalini.

Binafsi ningetamani tusiishie na anachokifanya CAG kwenye akaunti hiyo, tungeenda mbali zaidi kwa kuunda Tume ya Ukweli na Upatanishi ili kila aliyemtendea Mtanzania ndivyo sivyo, atubu makosa yake hadharani.

Ninasema hivi kwa sababu tukipanua wigo kwa njia hii walahi nawaambia hiki tunachokisikia kwenye hii akaunti ya plea bargain inaweza kuwa ni tone la maji ya mvua kwenye bahari, kwani kuna watu wamepitia maumivu.

Mathalan, tunaambiwa wapo wafanyabiashara waliodaiwa kodi na kikosi kazi kilichowajumuisha maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lakini kabla hawajatafakari cha kufanya akaunti zao zilifungwa.

Ukitazama na kuwasikiliza baadhi ya wafanyabiashara waliopitia hali hii, utagundua kulikuwa na mchezo wa kuwapa makadirio makubwa ya kodi ili ‘warudi kukaa mezani’ na wale waliogoma walikomolewa.

Hili wala si la siri kwa sababu hata wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha hotuba ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23, alilizungumzia hili na kuwaonya watumishi wa aina hii.

Waziri Nchemba alisema kuna mapato ya Serikali yanaingia kwenye mifuko ya watu binafsi na hii inafanyika kwa kukadiria viwango vya juu vya kodi, nami namuunga mkono kwa kuwa mkweli na muwazi.

Dk Mwigulu alisema baadhi ya maofisa wa TRA wanatengeneza mazingira hayo ili kulazimisha majadiliano kisha kupunguza kiasi ya kile kinachostahili na kilichopunguzwa kinaingia kwenye mifuko binafsi.

Hilo ni eneo moja, hebu turudishe kumbukumbu ya operesheni ya vyombo vya dola iliyofanyika katika maduka ya kubadilisha fedha (bureau de change), ambako wamiliki walivamiwa, wakaporwa fedha zao, magari yao na hati zao za nyumba.

Wengine wala hawakuwahi kuwa na madai yoyote ya kodi, licha ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa zamani, Hamad Masauni kulieleza Bunge mwaka jana kuwa mengi yalifungwa kwa kuendesha biashara bila kuzingatia sheria.

Hatukatai, kama kweli walikuwa wanaendesha biashara hiyo bila kufuata sheria na kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), adhabu yake ilikuwa ni kuporwa fedha, vitendea kazi na mali zao, au kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria za nchi?

Hadi mwaka 2019, biashara 16,252 zilifungwa nchini, hili wala si la kumtafuta mchawi, bali ukweli ni kuwa kulikuwa na mazingira magumu ya kufanya biashara na ukifuatilia, wengi walifunga maduka yao kwa sababu ya makadirio ya kodi yasiyo na uhalisia.

Ninaamini kama tunataka kuliponya Taifa na majeraha yanayovuja damu hadi leo, tusiishie kuchunguza kilichotokea katika akaunti ya plea bargain, tuunde tume ya ukweli na upatanishi ili watu wafunguke madhila yaliyowakuta kutoka kwa watumishi walioaminiwa kuwatumikia Watanzania kwa haki.

Ni kupitia tume hiyo tutawafahamu Watanzania waliotendewa ndivyo sivyo, tutawajua wawekezaji waliotendewa ndivyo sivyo na tutawajua raia walioumizwa na uamuzi mbaya wa baadhi ya watendaji wa Serikali walipokuwa wanatekeleza wajibu wao kinyume na utaratibu.

Tukifanya hivyo tutawajua walioumizwa na kuonewa na mfumo kwa sababu za kisiasa au nyingine zozote na waliofanya haya tuwajue na kiwango cha ushiriki wao ili tuamue kama Taifa kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa kizalendo utakaosaidia kuujenga uchumi wa nchi yetu.

Ndiyo maana nimetangulia kusema hili la akaunti ya plea bargain linaweza kuwa ni tone la maji ya mvua lililodondoka baharini lakini tukienda mbali zaidi na kupanua wigo wa uchunguzi, tutaweza kutibu majeraha mengi yanayoendelea kuvuja damu mtaani, kwani zipo familia ambazo hazijainuka mpaka leo.

Tusipofanya hivyo itakuwa kama Waswahili wanavyosema usipoziba ufa utajenga ukuta, hivyo hivyo tusipotibu majeraha haya tuliyopitia na kuondoa mioyo ya chuki na visasi, tutakuja kukumbuka shuka kukiwa kumepambazuka.

Mjema ni mwandishi wa gazeti hili mkoani Kilimanjaro. Kwa maoni na ushauri: 0656 600 900.