Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa nini Tanzania inahitaji biashara imara za kilimo?

Kwa muda mrefu kilimo kimekuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania. Mamilioni ya Watanzania wanategemea sekta hii kwa ajira, kipato na chakula. Aidha, mazao ya kilimo yameendelea kuwa sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya nchi, yakichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Taifa.

Hata hivyo, sekta ya kilimo ipo katika kipindi muhimu cha mabadiliko. Mazingira ya biashara inabadilika kwa kasi, na ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa unaongezeka.

Ili Tanzania iweze kunufaika kikamilifu na fursa hizi, ni muhimu kuanza kuangalia kilimo kwa mtazamo mpana zaidi ya uzalishaji pekee.

Leo hii mjadala hauishii tena kwenye kuongeza uzalishaji wa mazao shambani. Kinachozungumzwa zaidi ni namna gani tunaweza kujenga biashara za kilimo zilizo imara, zinazoongeza thamani ya mazao, na zinazoweza kushindana katika masoko makubwa zaidi.

Kuongeza thamani katika kilimo ni hatua muhimu katika safari ya maendeleo ya uchumi. Mazao yanapochakatwa hapa nchini badala ya kuuzwa ghafi, thamani yake huongezeka, ajira huongezeka, na uchumi wa maeneo ya vijijini huimarika.

Aidha, hatua hii husaidia Tanzania kujenga sekta ya kilimo inayochangia zaidi katika maendeleo ya viwanda na biashara.

Katika kipindi hiki, mahitaji ya bidhaa za kilimo zilizochakatwa yanaongezeka katika soko la Afrika Mashariki na hata nje ya bara. Hii ni fursa kubwa kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli zao na kufikia masoko mapya.

Hata hivyo, kufikia hatua hii kunahitaji maandalizi ya kimkakati. Biashara za kilimo zinahitaji miundombinu bora, mifumo madhubuti ya usimamizi, na upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji.

Bila uwekezaji katika maeneo kama uhifadhi wa mazao, usafirishaji, uchakataji na teknolojia za uzalishaji, itakuwa vigumu kwa biashara nyingi za kilimo kufikia kiwango cha ushindani kinachohitajika katika masoko makubwa.

Hapa ndipo taasisi za kifedha zinapokuwa na nafasi muhimu. Benki na taasisi nyingine za fedha zinaweza kusaidia wakulima, wasindikaji na wauzaji wa mazao kujenga mifumo ya biashara inayokidhi vigezo vya kupata mitaji ya kukuza shughuli zao.

Katika mazingira haya, taasisi za kifedha pia zina jukumu la kusaidia biashara za kilimo kujenga misingi imara ya ukuaji. Kupitia uzoefu wake katika sekta ya kilimo, Benki ya Stanbic imeendelea kufanya kazi kwa karibu na wakulima, wasindikaji na wafanyabiashara wa mazao katika mnyororo mzima wa thamani ili kuwasaidia kuimarisha mifumo ya biashara na kupata mitaji ya kukuza shughuli zao.

Kwa mfano, mikopo ya mtaji wa biashara inaweza kusaidia wafanyabiashara kununua mazao wakati wa mavuno na kuyaandaa kwa ajili ya masoko ya ndani na ya nje. Vilevile, ufadhili unaotegemea bidhaa zilizopo ghalani unaweza kusaidia wauzaji wa mazao kupata fedha wakati wakisubiri kuuza bidhaa zao katika masoko ya kimataifa.

Uwekezaji katika mitambo, maghala na miundombinu ya usafirishaji pia ni sehemu muhimu ya kujenga mnyororo wa thamani wa kilimo ulio imara.

Kwa upande mwingine, mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuleta changamoto mpya katika sekta ya kilimo. Mabadiliko ya mifumo ya mvua na ongezeko la hatari za uzalishaji vinahitaji uwekezaji katika mifumo ya umwagiliaji, uhifadhi bora wa mazao na matumizi ya nishati mbadala katika shughuli za uchakataji.

Hatua hizi husaidia kupunguza hasara za baada ya mavuno, kuimarisha uzalishaji na kuongeza uthabiti wa biashara za kilimo katika kipindi cha muda mrefu.

Ni muhimu pia kwa biashara za kilimo kujiandaa vizuri ili kupata ufadhili. Biashara zilizo na kumbukumbu sahihi za kifedha, mikataba ya masoko na mifumo thabiti ya uendeshaji huwa na nafasi kubwa zaidi ya kupata mitaji kutoka kwa taasisi za fedha na wawekezaji.

Tanzania ina rasilimali nyingi zinazoweza kuifanya kuwa nguvu kubwa katika uzalishaji wa kilimo barani Afrika.

Ardhi yenye rutuba, nguvu kazi kubwa na upatikanaji wa masoko ya kikanda ni baadhi ya faida ambazo nchi inazo. Iwapo uwekezaji katika miundombinu, teknolojia na mifumo ya biashara utaendelea kuimarishwa, sekta ya kilimo inaweza kuwa kichocheo kikubwa zaidi cha ukuaji wa uchumi wa taifa.

Hatua inayofuata katika maendeleo ya kilimo nchini ni kujenga biashara za kilimo zilizoandaliwa vizuri, zenye uwezo wa kuvutia uwekezaji na kushindana katika masoko ya kimataifa.

Kilimo kikiwa na muundo huo, hakitabaki tu kuwa nguzo ya uchumi wa Tanzania, bali kitakuwa pia chanzo kikubwa cha ajira, biashara na ustawi wa muda mrefu kwa taifa letu.

_*Na Benefrida Tarimo - Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara, Stanbic Bank Tanzania.*_