Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi ya kununua ardhi kisheria

Muktasari:

Leo tutajikita katika ununuzi, ardhi ni mali ambayo kila siku inapanda thamani na watu wanaweza kujipatia ardhi kwa njia ya kununua kisheria.

Uwanjani leo tutajikita kwenye kupata ardhi kwa njia ya kununua (by purchase) , wiki iliyopita tuliangalia upatikanaji wa ardhi kwa njia ya kugawiwa na Serikali ( by allocation).

Leo tutajikita katika ununuzi, ardhi ni mali ambayo kila siku inapanda thamani na watu wanaweza kujipatia ardhi kwa njia ya kununua kisheria.

Mauzo ya ardhi yanasimamiwa na sheria mbalimbali, kama mauzo yanahusiana na ardhi ya kijiji basi Sheria ya Ardhi ya Vijiji Itatumika, lakini kama mauzo hayo hayahusiani na ardhi ya kijiji basi sheria ya Ardhi Sura ya 113 itatumika.

Kwa kuwa ununuzi wa ardhi ni njia mojawapo ya kupata ardhi basi sheria iliweka misingi ili mauzo na ununuzi wa ardhi uwe halali na wewe uwe umejipatia ardhi ikiwa huru ( Free from encumbrances ).

Sheria ya Ardhi Sura ya 113 kifungu cha 64 (1) kinaeleza kuwa ununuzi wa ardhi au mikopo inayohusiana na ardhi lazima ziwe katika maandishi na lazima mkataba huo uwe na sifa kimkataba zinazokubalika kisheria.

Watu wengi wamekuwa wakitumia fedha nyingi kununua ardhi ambazo zina matatizo, zenye mikopo, zinazomilikiwa na wanandoa au wauzaji wasiokuwa na uwezo wa kisheria wa kuuza.

Mkataba wa ununuzi wa ardhi, lazima uwe halali kisheria, ushuhudiwe na wakili, lakini watu wamezoea kutoa asilimia kumi kwa wenyekiti wa serikali za mitaa wakijua basi hapo itakuwa ni mwisho wa matatizo, lakini kuna matapeli wengi wanachonga mihuri na kujifanya wenyeviti wa Serikali za Mitaa.

Hata hivyo, mawakili wana nafasi zao, mwenyekiti wa mtaa leo anaweza kuwa huyu, kesho akachaguliwa mwingine, lakini wakili kama ofisa wa mahakama ni shahidi namba moja. Ardhi ni mali unapaswa kuitunza na kuilinda, lakini katika kupata ardhi kwa njia ya kununua mtu hufuata hatua zifuatazo.

Kwanza mtu anapaswa kufanya uchunguzi wa kina wa eneo ikiwa ni pamoja na kufanya upekuzi kwa msajili wa hati, kwenye ofisi za manispaa, kwa majirani na kwa kutembelea eneo husika.

Hatua ya pili ya mauzo ni kukubaliana juu ya bei na mambo mengine ya msingi, na ndipo mwanasheria huwaandikia mkataba mzuri unaokidhi matakwa ya kisheria, hata ikitokea mmedhulumiana wakili atakuwa shahidi namba moja, atathibitisha kuwa kilichoandikwa mle ni kweli.

Hatua ya tatu watu husainishana mkataba mbele ya wakili, na kufanya malipo husika ya eneo, hapo mauzo yatakuwa yamekamilika,

Nne, hatua hii humfanya mtu kubadili umiliki kutokwa kwa wauzaji au muuzaji kwenda kwa jina la mnunuzi (conveyance), hii ni hatua ndefu kidogo ambayo mtu hupaswa kuzifuata ili kubadili umiliki kutoka kwa jina la muuzaji kwenda kwenye jina la mnunuzi hapa lazima kupata ridhaa kutoka kwa kamishna wa ardhi.

Hata hivyo, endapo mauzo yatakamilika lakini baadaye kamishna akashindwa kutoa ridhaa haimaanishi mauzo hayo ni batili, hiyo ilielezwa na mahakama ya rufaa kwenye kesi ya Abualy Alibhai Azizi v. Bhatia Bros (2000 TLR 288 C.A).

Ili kuepuka migogoro unapaswa kufanya uchunguza wa kina kabla ya kununua ardhi yoyote ile, eneo lolote. Wengi wamekuwa wakiteseka mara nyingine hata mwezi haujaisha tangu ununue unakuta migogoro kibao eneo hilo, ukiangalia karatasi uliyonayo kisheria siyo mkataba kabisa.

Ununuzi wa ardhi unapaswa kufanywa kwa umakini. Wiki ijayo tutaangalia kupata ardhi kwa njia ya kukaa kwenye eneo kwa muda mrefu ( by adverse possession).

Mwandishi ni wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya Law Guards Advocates ya Dar es Salaam.