Huu ndio umaarufu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi

Muktasari:
Vilevile hifadhi hii ipo kwenye safu za milima ya Malundwe ambayo ni sehemu ya safu za milima ya tao la mashariki hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi kutokana na wanyama mbalimbali kuonekana kirahisi na kwa wingi.
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ni maarufu nchini na duniani kwa ujumla kutokana na vivutio mbalimbali ilivyonavyo likiwamo Bonde la Mto Mkata linalosifika kwa mkusanyiko wa wanyamapori hasa tembo, nyati, simba, chui, twiga na ndege wa aina tofauti zaidi ya 400.
Vilevile hifadhi hii ipo kwenye safu za milima ya Malundwe ambayo ni sehemu ya safu za milima ya tao la mashariki hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi kutokana na wanyama mbalimbali kuonekana kirahisi na kwa wingi.
Katika Hifadhi ya Mikumi wanapatikana simba, tembo, nyati na twiga kati ya wanyama watano maarufu zaidi duniani wajulikanao kama the big five.
Mikumi wanapatikana mbwa mwitu pia ambao kwa sasa wapo hatarini kutoweka. Ni hifadhi rahisi kifikika kwa njia zote za usafiri.
Ikiwa na ukubwa la kilomita za mraba 3,230, Mikumi ni ya tano kwa ukubwa nyuma ya hifadhi nyingine za Taifa ambazo ni Serengeti, Ruaha, Katavi na Mkomazi.
Licha ya kupatikana kwa wanyama adimu kama chui na ndege wenye uwezo wa kusafiri bara moja hadi jingine na makundi makubwa ya nyumbu wanaosafiri umbali mrefu, hifadhi hii ina miti maarufu kama mpingo unaochanwa mbao na mti wenye matunda yanayotengeneza pombe aina ya Amarula ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii hasa wa nje.
Pamoja na kuwepo kwa wanyama mbalimbali, Mikumi kuna bwawa lenye viboko na mamba ambao licha ya hatari yao kwa watu na mifugo isiyo makini, ni moja ya vivutio.
Umaarufu wa hifadhi hii iliyopo ndani ya Wilaya za Kilosa, Morogoro Vijijini na Mvomero unatokana na ujirani mwema baina ya hifadhi na vijiji 19 vinavyoizunguka.
Kutokana na umaarufu wake, idadi ya watalii wa ndani na nje imekuwa ikiongezeka kadri siku zinavyokwenda.
Hali ya usalama imeimarishwa kwa kufanya doria hasa katika misitu na maeneo ya barabara kuu inayokatisha ndani ya hifadhi. Kilomita 50 za barabara itokayo Dar es Salaam kwenda Mbeya inapita katika hifadhi hii.
Kuimarisha zaidi ulinzi wa wanyama na usalama wa wageni wanaitembelea hifadhi hiyo, kuna mkakati wa kufunga vifaa vya kisasa vya kudhibiti uhalifu na zikiwamo kamera za ulinzi za CCTV katika lango kuu la kuingilia na maeneo yanayotumiwa zaidi na watalii.
Kupitia kitengo chake cha ikolojia, hifadhi imeendelea kuhakikisha mazingira yanasimamiwa kikamilifu utunzaji wa maliasili kwa kuzuia uchafuzi wa aina yoyote.
Kila siku, Hifadhi ya Taifa Mikumi imekuwa ikikusanya taka zaidi ya kilo 130 kando ya barabara kuu inayokatiza katika katika eneo lake hivyo kuyafanya mazingira kuwa safi wakati wote na kuvutia zaidi.
Kwa kutumia watalaamu afya za wanyamapori, magonjwa ya mlipuko yanayoweza kusambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu au miongoni mwa wanyama wenyewe, umekingwa.
Licha ya barabara, hifadhi hii pia imepitiwa na miundombinu mbalimbali likiwemo Bomba la Mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia (Tazama), nguzo za umeme mkubwa wa gridi ya Taifa na mkongo wa mawasilino na reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).
Ndani ya hifadhi hii pia kipo kiwanja cha ndege ambacho uhudumia ndege ndogo zinazokodiwa na baadhi ya wageni na inapakana na Mji Mdogo wa Mikumi ambao ni wa kibiashara.
Pamoja na hifadhi hii kuwa maarufu, bado kuna Watanzania wengi hawafahamu vivutio vilivyopo wala hawahamasiki kuitembelea wakidhani kuwa utalii upo kwa ajili ya wageni tu.
Umaarufu wa hifadhi hii unaweza kuuona kwa kiasi kidogo hasa pale unapopita kwenye barabara kuu inayokatiza katikati yake na kujionea baadhi ya wanyama wakiwamo swala, tembo, twiga na pundamilia.
Muda mfupi wa wanaotumia wasafiri kukatiza katika hifadhi hii hautoshi kuelezea vizuri vivutio vilivyopo Mikumi hivyo Watanzania wanapaswa kutenga muda na kuwa tayari kulipia gharama ndogo inayotozwa kuitembelea.
Ni burudani kuitembelea hifadhi hii pamoja na nyingine ziolizopo maeneo tofauti nchini. Vivutio hivi vya utalii hutoa fursa ya wananchi kujifunza mambo mengi ambayo hayapatikani mjini na maeneo mengine tukoishi na kuendesha shughuli za kila siku.
Nitoe wito kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau wengine kuendelea kutoa elimu ili kuwahamasisha wananchi wengi zaidi kutambua umuhimu wa kufanya utalii wa ndani.
Wazazi wanapaswa kuvifahamu vivutio hivi ili iwe rahisi kwao kuwahamasisha watoto wao.
Hamida Shafiff ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Morogoro. Anapatikana kwa namba 0715681287.