Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Almasi ya Tanzania ni adimu duniani isichezewe ovyo ovyo

Muktasari:

  • Hazina yote hii ya madini inamilikiwa na Serikali, hivyo shughuli za utafutaji na uchimbaji wake huweza kufanywa na wananchi au kampuni baada ya kupewa leseni zinazotolewa na wizara husika.

Tanzania imebarikiwa kuwa na hazina kubwa ya rasilimali ya madini. Dhahabu, almasi, nikeli, urani, makaa ya mawe, jasi, chumvi na mengineyo yanapatikana nchini.

Hazina yote hii ya madini inamilikiwa na Serikali, hivyo shughuli za utafutaji na uchimbaji wake huweza kufanywa na wananchi au kampuni baada ya kupewa leseni zinazotolewa na wizara husika.

Almasi ni moja ya madini adimu yenye mvuto kwa wavaaji wa vito tangu zama za kale.

Inachukuliwa kama kielelezo cha ufahari kwa wafalme, watawala, makuhani au wengine wenye mamlaka.

Ni kielelezo cha utajiri na nguvu ya fedha kwa watumiaji wengine pia.

Kwa asili yake, madini ya almasi hayana rangi, hata hivyo kasoro katika uumbaji wake husababisha iwe na rangi mbalimbali.

Uwapo wa rangi unaweza kuongeza au kupunguza thamani ya almasi kulingana na mahitaji ya soko.

Rangi zinazoongeza thamani ya almasi ni nyekundu na ni adimu kuliko rangi zote, bluu na pinki.

Nyingine ni njano, nyeusi, kijani na kahawia.

Tanzania, mgodi pekee wenye historia kubwa ya uzalishaji almasi ni Williamson Diamonds Limited (WDL) uliopo Kishapu huko Shinyanga.

Mgodi huu ambao unaitwa ‘Mwadui’ kwa heshima ya chifu wa eneo hilo, uligunduliwa na Dk John Williamson mwaka 1940.

WDL ilisajiliwa mwaka 1942 na Serikali ya kikoloni ikiwa na hisa 400 zenye thamani ya Paundi 500 kila moja, hivyo kuufanya mtaji wake kuwa ni pauni 200,000.

Mgodi huu unasifika duniani kwa mambo mengi na ni miongoni mwa wazalishaji wachache wa almasi ya pinki (rangi adimu na inayopendwa zaidi duniani).

Mgodi maarufu kwa uzalishaji almasi za pinki ni ule wa Agyle uliopo Australia Magharibi unaotoa asilimia 90 ya almasi yote inayopatikana duniani.

Licha ya Mwadui, Tanzania pia inachimba almasi katika mgodi unaoendeshwa na Kampuni ya El Hilal Minerals iliyopo jirani na WDL huko Kishapu mkoani Shinyanga.

Wachimbaji wadogo huko Maganzo, Kishapu na Mabuki mkoani Mwanza nao pia wanachimba almasi.

Almasi ya pinki hupatikana katika migodi michache sana duniani na uadimu wake huifanya itafutwe zaidi.

Tanzania inasifika kwa kutoa almasi hii kwa Afrika. Ukiwa nayo, unakuwa miongoni mwa watu maarufu au matajiri.

Madini haya huuzwa na kununuliwa kulingana na soko kwa vigezo vya uzito, usafi wa jiwe, mkato na rangi yake maarufu kama 4Cs.

Septemba 2015, Mwadui ilibahatika kupata jiwe kubwa la almasi ya pinki lenye uzito wa karati 23.16.

Almasi hii imeweka rekodi kwa Mwadui kwani iliuzwa kwa Dola 10.05 milioni za Marekani huko Antwerp nchini Ubelgiji.

Hii ni rekodi mpya kuwahi kupatikana na kuuzwa kwa mgodi wa nchini.

Mbali na jiwe la pinki, nyingine kubwa kuwahi kupatikana Mwadui ilikuwa na uzito wa karati 54.5 ambayo Dk Williamson alimzawadia Malkia wa pili wa Uingereza, 1947 kwenye harusi yake.

Jiwe hilo halikuwahi kuuzwa au kuingizwa sokoni lakini linadhaniwa kuwa ni almasi bora ya pinki kuwahi kupatikana duniani.

Pinki hiyo iliyotolewa kama zawadi kwa Malkia baadaye ilikatwa na kutoa jiwe la karati 23.6 lililowekwa katika mfano wa ua (Williamson pink brooch).

Hili ni miongoni mwa mapambo adimu yanayopendwa kuvaliwa na mtawala huyo wa Uingereza.

Takwimu za 2013 za Mgodi wa Mwadui zinaonyesha kuwa mgodi huo unashikilia rekodi ya dunia ya kuwa wa pekee uliochimbwa mfululizo kwa miaka 70.

Ndiyo mgodi mkubwa zaidi duniani unaochimbwa kwa stahili ya shimo la wazi (open cast) ukiwa na akiba ya almasi inayokadiriwa kuwa karati milioni 40.

Vilevile, unakadiriwa kuwa na uhai wa miaka 18 na uwezekano wa kuendelea kuzalisha almasi kwa miaka mingine 50 ijayo.

Kumbe Tanzania tuna madini ya kila aina na yenye thamani kubwa, yenye ubora wa juu.

Ni vema madini yote yanayopatikana Tanzania yafuatiliwe kwa karibu ili wananchi wote wafaidike na Serikali ikusanye mapato yake na kusaidia kupaisha uchumi wa nchi.

Wachimbaji wote wakubwa kwa wadogo wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini, ni vema wakatoe ushirikiano kwa Serikali katika ulipaji wa kodi mbalimbali ili Tanzania na wananchi wake wafaidike na madini yao.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya uchumi na jamii. Anapatikana kwa namba 0756638393