Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafula Chebukati afariki dunia akiwa na miaka 63

Muktasari:

  • Kipindi chake cha uongozi kama Mwenyekiti wa IEBC, kilianza Januari 2017 baada ya kuondolewa kwa Ahmed Issack Hassan na makamishna wenzake.

Nairobi. Wafula Chebukati, aliyesimamia uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 uliobatilishwa na Mahakama ya Juu na pia uchaguzi wa mwaka 2022 uliosababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 63.

Kipindi chake cha uongozi kama Mwenyekiti wa IEBC, kilianza Januari 2017 baada ya kuondolewa kwa Ahmed Issack Hassan na makamishna wenzake.

Akiwa mwanasheria wa hadhi ya chini kisiasa, alichukua ofisi hiyo wakati wa mvutano mkubwa wa kisiasa, ambapo kiongozi wa upinzani, Raila Odinga alikabiliana na Rais Uhuru Kenyatta aliyekuwa akitafuta kuchaguliwa kwa muhula wa pili.

Aliingia madarakani chini ya miezi saba kabla ya uchaguzi, ambapo yeye na timu yake walihitajika kusimamia mojawapo ya chaguzi zenye ushindani mkubwa zaidi nchini Kenya.

Hata hivyo, jaribio lake la kwanza la kusimamia uchaguzi mkuu halikufanikiwa, kwani matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 yalibatilishwa na Mahakama ya Juu katika uamuzi wa kihistoria.

Katika uamuzi wake, Mahakama hiyo, chini ya Uenyekiti wa Jaji Mkuu, David Maraga, iligundua kuwa uchaguzi uliompa ushindi Kenyatta dhidi ya Odinga ulikumbwa na kasoro na ukiukwaji wa sheria uliofanywa na IEBC.

Mahakama ya Juu iliagiza uchaguzi mpya wa urais kufanyika ndani ya siku 60.

Hata hivyo, Odinga alisusia uchaguzi huo wa marudio, akidai kuwa hangeweza kushiriki katika uchaguzi unaosimamiwa na Tume ileile iliyoharibu uchaguzi wa awali.


Alikuwa mtu wa misimamo

Akiwa mtu aliyesimamia chaguzi mbili zilizobishaniwa, Chebukati mara kwa mara alijikuta akikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa lakini alikataa wito wa kujiuzulu.

Uchaguzi wa urais wa mwaka 2022 haukuwa tofauti, kwani upinzani ulidai kuwa mgombea wao, Odinga, alinyimwa ushindi kwa manufaa ya William Ruto.

Upinzani, ambao ulipinga matokeo ya uchaguzi huo katika Mahakama ya Juu bila mafanikio, ulidai kuwa kulikuwa na upatikanaji usio halali wa mifumo ya IEBC, jambo lililowawezesha baadhi ya watu kudukua matokeo ya mwisho kwa faida ya Dk Ruto.

Hata hivyo, Mahakama ya Juu ilitupilia mbali madai hayo na kuthibitisha ushindi wa Dk Ruto, ikitaja baadhi ya madai yaliyowasilishwa kuwa “ya kipuuzi”, na hivyo kufungua njia kwa kuapishwa kwake kama Rais wa tano wa Kenya.


Mgawanyiko ndani ya IEBC

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa Agosti 2022, hasa wakati wa kuhesabu kura, mgawanyiko mkali uliibuka ndani ya Tume, hali iliyosababisha mgawanyiko mkubwa kati ya makamishna kuhusu usimamizi wa shughuli za uchaguzi.

Makamishna hao saba waligawanyika katika makundi mawili: moja likiongozwa na Chebukati, Boya Molu, na Abdi Guliye, huku lingine likijumuisha Makamu Mwenyekiti, Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya.

Dalili za mzozo wa ndani zilianza kuonekana wakati vifaa vya uchaguzi vilipowasili nchini, ambapo baadhi ya makamishna walidai kutofahamu kilichokuwa kikiwasilishwa.

Mivutano hii ilizidi kudhihirika kupitia mikutano ya waandishi wa habari iliyofanyika Bomas ya Kenya. Wakati fulani, mwandishi mmoja alimuuliza mwenyekiti ikiwa taarifa aliyokuwa akitoa ilikuwa na uungwaji mkono wa makamishna wote.

“Je, kuna yeyote anayepinga? Kuna mtu yeyote? Chebukati alijibu kwa mshangao, huku akiwatazama makamishna waliokuwa wameketi naye kwenye mkutano huo.

Mvutano huo hatimaye ulifikia kilele wakati makamishna wanne walipokataa matokeo ya uchaguzi wa urais hadharani.


Makundi hasimu IEBC

Makamishna hao—Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit, na Justus Nyang’aya—walijitenga na matokeo yaliyokuwa yakitangazwa na Chebukati, wakidai kuwa hayakuwa yamehakikiwa na makamishna wote kama ilivyokubaliwa awali.

Makamishna hao wanne, baadaye walipewa jina la “Cherera Four”, walitoka nje ya ukumbi wa Bomas na kuitisha mkutano na wanahabari katika Hoteli ya Serena, ambapo walikataa matokeo ya urais yaliyokuwa yakitangazwa na Tume.

Miongoni mwa madai yao ilikuwa ni kwamba asilimia za kura za wagombea wa urais zilikuwa zimezidi asilimia 100, hali iliyotia shaka usahihi wa matokeo hayo.

Pia, walimshtumu Chebukati kwa kupuuza mapendekezo yao, wakisema kuwa alikuwa amejifanya kuwa ofisa msimamizi wa uchaguzi wa urais kinyume cha sheria.

Hata hivyo, mwishowe, Chebukati ndiye aliyeshinda mzozo huo, kwani hatimaye kundi lililompinga liliondoka IEBC, huku mmoja wao, Irene Masit, akiondolewa rasmi baada ya kuundwa kwa jopo la kumchunguza.


Taswira ya Chebukati kwa umma

Wengine walimuona Chebukati kama kiongozi aliyekataa kusikiliza maoni ya wengine, huku baadhi wakimwona kama mtu thabiti na mwenye msimamo, ambaye hakuweza kushawishiwa na shinikizo la nje.

Baada ya kuondoka ofisini mwishoni mwa kipindi chake cha miaka sita, Chebukati alijitenga na siasa kwa kiasi kikubwa huku ripoti zikidai kuwa afya yake ilikuwa ikidhoofika.


Maisha na kazi yake

Chebukati alizaliwa Desemba 19, 1961, alikuwa mhitimu wa shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na shahada ya uzamili ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta.

Kabla ya kujiunga na IEBC, alikuwa mwanasiasa na mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ambacho alikihama kabla ya kuomba nafasi ya Uenyekiti wa IEBC.

Mwaka 2007, aligombea ubunge katika jimbo la Saboti lakini akashindwa uchaguzi huo, akishika nafasi ya pili.