Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri zinazovutia mikutano ya kimataifa kufanyika Tanzania

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na marais wa nchi za Afrika waliohudhuria mkutano wa nishati unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Miongoni mwa sifa zinazotajwa za utawala wa hayati Rais John Magufuli ni kujifungia, kwa maana kuwa nchi ilikuwa haijichanganyi sana kidiplomasia. Mkuu wa nchi hakupenda safari za nje, lakini pia alipokea wageni wachache.

Katika kipindi hicho, mkutano mkubwa uliofanyika ulikuwa mkutano mkuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019, ambapo Tanzania ilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

Hata hivyo, hali ilibadilika tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Machi 19, 2021, ambapo Tanzania imefunguka na kufanikiwa kuandaa mikutano mingi ya kimataifa, ikiwemo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, na inayohusisha masuala ya ulinzi na usalama.

Kidiplomasia, hii imekuwa heshima kubwa kwa Tanzania, hasa kwa kutembelewa na viongozi wakubwa wa mataifa mbalimbali, akiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, aliyetembelea nchini Machi 29, 2023.

Tangu aingie madarakani Machi 19, 2021, Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuhimiza na kuimarisha diplomasia, akisema Tanzania inahitaji kuchangamana na mataifa mengine kukuza ushirikiano.

Kutokana na hilo, tumeshuhudia safari za hapa na pale za ndani na nje ya Bara la Afrika zenye lengo la kukuza ushirikiano na kuitangaza Tanzania duniani ili kuchochea utalii na kuita wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali. Kadhalika, imeshuhudiwa mikutano mingi ya kimataifa hapa nchini.

Miongoni mwa mikutano hiyo ni pamoja na mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa barani Afrika (The 3rd G25 Africa Coffee Summit) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Februari 22, 2025.

Mbali na hilo, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Energy Connect Conference & Exhibition na mkutano wa tisa wa Africa Energy Market Place (AEMP) uliofanyika Oktoba 2024.

Januari mwaka huu, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Afrika (Mission 300). Mkutano huo ulijikita katika kushughulikia changamoto za nishati barani Afrika, ambapo Tanzania iliahidi kuongeza uwezo wake wa kuzalisha nishati kufikia megawati 4,000 ifikapo mwisho wa mwaka.

Kuanzia Machi 4 hadi 7, Tanzania iliandaa mkutano wa 11 wa Mafuta na Gesi wa Afrika Mashariki (EAPCE’25), uliofanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Januari 28, mwaka huu, wakuu wa nchi 21 kutoka mataifa ya Afrika walikutana jijini Dar es Salaam kuhitimisha mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati. Mkutano huo ulivunja rekodi ya kuwa tukio lililohudhuriwa na marais wengi zaidi kwa wakati mmoja.

Mingine ni pamoja na mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania, uliofanyika kati ya Novemba 19 hadi 21, 2024, jijini Dar es Salaam.

Mkutano wa tathmini ya muda wa kati wa mzunguko wa Benki ya Dunia ulifanyika mwaka 2023 Zanzibar, ukihusisha wajumbe 2,590 kutoka nchi 100 duniani.

Pia, mkutano wa jukwaa la mifumo ya chakula Afrika (AFSF), ulioangazia kujadili na kuboresha mifumo ya chakula barani Afrika, uliofanyika mwaka 2023.

Sambamba na hilo, kulikuwepo mkutano wa wakuu wa nchi wastaafu, jijini Arusha, ukihusisha viongozi wastaafu kujadili masuala muhimu ya bara la Afrika mwaka 2023.

Kadhalika kulifanyika mkutano wa wanawake na vijana katika biashara kwenye eneo huru la biashara barani Afrika (AfCFTA) uliofanyika kati ya Septemba 12 hadi 14, 2022, JNICC, Dar es Salaam.

Pia, kulifanyika mkutano wa nne wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini, uliofanyika mwaka 2022 jijini Dar es Salaam, ukihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.

Novemba 31, 2021, kulifanyika kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza lililolenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.


Sababu za mikutano kufanyika Tanzania

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo, anasema Tanzania imejitangaza kupitia filamu ya Royal Tour, iliyorekodiwa kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji unaopatikana nchini.

Jambo lingine ni kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Maliasili na Utalii, ambazo zimeweza kutangaza ajenda ya diplomasia ya mikutano ya utalii.

“Diplomasia ya mikutano inakuja wakati wewe (kiongozi wa nchi) umeweza kusafiri nje ya nchi pamoja na ujumbe wako, unaojumuisha wafanyabiashara. Rais Samia amekwenda nchi za Ulaya, Amerika, Asia na nchi za Bara la Afrika,” anasema Shoo.

“Hii yote ameifungua nchi zaidi na kuongeza idadi ya balozi zetu, ikiwemo balozi ndogo zilizowezesha nchi kutambulika na watu kuifahamu zaidi Tanzania, inayozidi kujitangaza na kujipambanua kwamba kuna amani na usalama wa kutosha.”

Shoo anasema wageni wakija katika Taifa lako, ni rahisi nawe kwenda kwao, ndivyo alivyofanya Rais Samia. Mbali na hilo, Rais Samia ameonyesha utawala bora katika kipindi cha miaka minne, akifungua ubalozi mpya na kuthibitisha kuwa Tanzania si kisiwa.

Anasema tangu Rais Samia aingie madarakani, kuna mambo aliyoyabadilisha na kuyaleta upya, tofauti na mtangulizi wake, ambaye sera zake hazikuendana na diplomasia inayotaka kuungana na mataifa mengine.

“Sasa Tanzania si kisiwa, lazima uungane na wenzako kila kona duniani ili kuendeleza zana nzima ya uhusiano wa kimataifa. Kwa mfano, mtangulizi wake hakuwa mtu wa kusafiri sana kwenda mataifa ya nje, badala yake alituma wasaidizi wake,” anasema Shoo.

Shoo anasema, kwa mujibu wa utaratibu au itifaki, kadiri unavyotuma mtu wa chini, basi akifika Taifa fulani anapokelewa hivyo na mtu wa chini wa taifa husika.

“Hatakutana na kiongozi wa ngazi ya juu, lakini pia uamuzi mkubwa unafanywa na viongozi wa juu, siyo wawakilishi,” anasema Shoo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus, anasema mabalozi wa Tanzania wamekuwa na hadidu za rejea za kuitangaza Tanzania nje ya nchi na hivyo kuvutia mashirika na taasisi nyingi kufanya mikutano nchini.

“Suala la amani, utulivu, na ukarimu wa Watanzania kwa wageni ni turufu mojawapo inayozishawishi nchi na taasisi za kimataifa kuja kufanyia mikutano Tanzania.

“Rais Samia, katika ziara zake za nje, amekuwa mstari wa mbele kuitangaza Tanzania na kuwashawishi marais wenzake katika ajenda zake anazozisimamia, hivyo kupata nafasi ya kuwavutia wenzake na kumuunga mkono,” anasema.