Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SALUM MWALIMU: Rais wa masela, asema ikulu ni mwendo wa tisheti na jinzi

Muktasari:

  • Mwaka 2014, jumuiya ya wanahabari na wale wa ulimwengu wa biashara kubwa kitaasisi, waliingiwa na mshangao.

Mwaka 2014, jumuiya ya wanahabari na wale wa ulimwengu wa biashara kubwa kitaasisi, waliingiwa na mshangao.

Mtu aliyekuwa na wasifu bora kwenye maeneo hayo mawili, aliyefanikiwa bila shaka, aliingia kwenye siasa.

Jina lake ni Salum Mwalimu Juma. Mguu wa Salum kwenye siasa ulijielekeza moja kwa moja Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Salum akateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Chadema, Zanzibar.

Muongo mzima wa kwanza karne ya 21, aliutumia kujenga barabara ya wasifu wake kama mwanahabari na msoma taarifa ya habari mahiri na nyota.

Kila mtu aliheshimu ubora wa Salum akiwa mwanahabari, kisha aliajiriwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Vodacom kwa nafasi ya Meneja Uhusiano wa Nje.

Ulikuwa mwanzo wa Salum kujenga wasifu wake kwenye jumuiya za mitandao ya simu, vilevile kutengeneza haiba ya utumishi katika mashirika makubwa.

Wasifu wa Salum kuanzia kwenye taaluma ya habari mpaka Vodacom, unajenga taswira na tafsiri ya moja kwa moja kuwa, aliingia kwenye siasa akiwa na kusudi alilokuwa analielekea. Haikuwa kufuata fursa za kimaisha, maana tayari alishajenga wasifu bora wa kumfanya kuishi akiwa mwanahabari.

Maisha ya Salum baada ya kutinga Chadema yamekuwa sehemu ya harakati za mageuzi, akitumika zaidi kujenga taasisi hiyo kisiasa.

Ni rahisi kutambua jinsi uzoefu wa Salum wa kufanya kazi kitaasisi ulivyokuwa na manufaa Chadema.

Nyakati zote akiwa Chadema, Salum alihesabika kuwa mtiifu wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye ndiye alimshawishi kujiunga na harakati za mageuzi, hivyo kuacha ajira yake Vodacom na kuingia kwenye hekaheka za siasa.

Miaka 11 akiwa Chadema, kisha akajiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Kutoka Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, sasa Katibu Mkuu. Haitoshi, Chaumma wameyaweka matumaini yote ya chama kwa Salum.

Agosti 7, 2025, wajumbe wa Mkutano Mkuu Chaumma, walimpigia kura nyingi Salum kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo, kwa sasa Salum yupo kwenye mapambano akiizunguka, nchi, akiomba Watanzania wamwamini, wamchague kuwa Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu.


Maisha ya Salum

Novemba 24, 1979, familia ya askari wa zamani wa Jeshi la Majini, Mwalimu Juma Mwalimu na mkewe, Fauziyat Ismail Aboud, walipata mtoto, wakamwita Salum.

 Mama wa Salum ni mwanahabari aliyewika zaidi akiwa mtangazaji wa kituo cha televisheni cha ITV.

Salum kuwa mtangazaji mahiri ni matokeo ya maji kufuata mkondo. Fauziyat alianza kuwa mtangazaji mahiri wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), kisha akaweka rekodi kuwa msoma taarifa ya habari wa kwanza alipojiunga na ITV. Inaleta tafsiri kuwa Salum alikuzwa vema kitaaluma, kutoka vyuoni hadi ndani ya familia.

Katika maisha yake, Salum amekuwa akihama kutoka mkoa mmoja hadi mwingine, visiwani mpaka bara, hiyo imesababisha elimu yake iwe ya kuhama shule kwa shule.

Inaakisi pia umaridhawa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Unaweza kuishi, kusoma au kufanya shughuli zako popote ndani ya mipaka bila bughudha, mradi wewe ni Mtanzania.

Elimu ya msingi, Salum alisoma kwenye shule mbili tofauti, alianza na Mkunazini, iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi, katika Jiji la Zanzibar.

Mwaka 1995, alihitimu Shule ya Msingi Mlimwa, iliyopo ndani ya Wilaya ya Dodoma, mkoani wa Dodoma.

Mwaka 1996, Salum alijiunga na elimu ya sekondari. Ilimchukua shule tatu kuhitimu kidato cha nne. Alianza na Shule ya Sekondari Dodoma, halafu akasoma Shule ya Sekondari Umbwe, iliyopo Moshi Vijijini, Kilimanjaro, kabla ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 1996, akiwa Shule ya Sekondari Kibaha, Pwani.

Mwaka 2000 mpaka 2002, Salum alisoma na kuhitimu Shule ya Juu ya Shy Com. Alipomaliza kidato cha sita, Shule ya Juu ya Shy Com, moja kwa moja Salum aliingia kwenye maisha ya ajira.

Alijiunga na Televisheni ya Channel 10. Alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 23, kipindi anaanza kujenga wasifu wake kwenye tasnia ya habari.

Salum ni mpambanaji wa elimu. Pamoja na kuwa kazini, mwaka 2004, alijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam, aliposomea Shahada ya Juu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

 Baada ya hapo, alidahiliwa kwenye Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC – UDSM).

Kupitia SJMC – UDSM, Salum alisoma shahada ya uzamili ya Mawasiliano ya Umma. Shahada hiyo ya uzamili ambayo alihitimu mwaka 2007, ilikuwa mradi wa pamoja kati ya SJMC – UDSM na Taasisi ya Kimataifa ya Masomo ya Biashara (IIBS), ya Bangalore, India.

Mwaka 2012, Salum alijiunga IFM, aliposomea Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara za Kimataifa, aliyohitimu mwaka 2014. Hiyo ina maana kuwa Salum ana shahada mbili za uzamili na stashahada ya juu moja.


Ajira na siasa

Mwaka 2003, Salum alijiunga na Kampuni ya Africa Media Group Limited (AMGL), kama mtangazaji.

Alipata umaarufu mkubwa akiwa mtangazaji wa Televisheni ya Channel 10, hasa eneo la usomaji wa taarifa ya habari.

Ajira ya Salum AMGL au Channel 10, ilidumu kwa miaka minane. Mwaka 2011, alijiunga na Kampuni ya Vodacom Tanzania Public Limited, kama Meneja Uhusiano wa Nje. Maisha ya miaka mitatu akiwa ‘corporate’ ilimtosha kuhama uwanja wa mapambano ya maisha.

Septemba 15, 2014, Salum aliidhinishwa na Baraza Kuu Chadema kuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho, Zanzibar. Cheo hicho, alikitumikia kwa miaka 11, hadi Januari 22, 2025, Tundu Lissu, akiwa mwenyekiti mpya Chadema, alipotangaza safu mpya na kumweka kando Salum.

Mei 2025, Salum alijiunga na Chaumma na muda mfupi baada ya kukabidhiwa kadi, alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa chama hicho. Nafasi hiyo anaendelea kuishikilia akiwa anaendelea na mapambano ya urais.

Tangu ameingia kwenye siasa, Salum amekuwa kwenye harakati bila kukoma. Mwaka 2015, alisimama kama mgombea ubunge, kwa tiketi ya Chadema, jimbo la Kikwajuni, Zanzibar. Hakuweza kushinda.

Mwaka 2017, Salum aliteuliwa na chama chake wakati huo, Chadema, kuwa mgombea ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA). Hakuchaguliwa. Februari 17, 2018, jina la Salum lilikuwa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge, Kinondoni.

Desemba 2017, aliyekuwa mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maulid Mtulia alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM.

Uchaguzi mdogo uliitishwa, Chadema walimteua Salum kuwa mgombea lakini hakushinda.

Alijikuta akiingia kwenye mgogoro mzito wa kisheria, akiwa na viongozi wengine wa Chadema. Salum aliunganishwa kwenye kesi ya kufanya mkusanyiko na maandamano batili, hatua ambayo ilisababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia  Chama cha Ukombozi wa Umma Chaumma, Salum Mwalim akimwaga sera kwa wananchi katika mkutano wa kampeni za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa Bunda Mjini, mkoani Mara.

Salum alikuwa mmoja wa viongozi wa Chadema waliohukumiwa kifungo jela miezi mitano au faini ambayo jumla yake ilikuwa Sh350 milioni, kisha Watanzania nchi nzima waliungana kutoa michango, iliyorahisha faini kupatikana na wakaachiwa huru.

Hapa ni nyongeza kuwa mapambano na polisi, kukamatwa, kuwekwa mahabusu na hata kuhukumiwa kifungo, kama moja ya wasifu wa wanasiasa wa upinzani Afrika, basi Salum naye anao. Anajua joto la kupambana akiwa mwanasiasa wa upinzani.

Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Salum aliteuliwa na kilichokuwa chama chake, Chadema, kuwa mgombea mwenza wa urais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipopeperusha bendera na Lissu, Mwenyekiti wa sasa Chadema.


Rais wa masela

Utambulisho wa kisiasa nyakati za uchaguzi huwa ubunifu mzuri.

Mwaka 2020, Chaumma, kupitia aliyekuwa mgombea urais wake, Hashim Rungwe, walitembea na ajenda ya chakula, waliyoianza kama ahadi ya kuwalisha wanafunzi shuleni, kisha ikawa fasheni.

Salum akiibeba Chaumma, utambulisho wake ni kuwa Rais wa vijana, yaani masela.

Salum anasema, akiwa Rais wa Tanzania, mavazi yake yatakuwa fulana (tisheti) na suruali za jinzi. Aina hiyo ya mavazi ndiyo hutumiwa zaidi na vijana.

Anaahidi kuwa Rais wa mitaa kuliko ofisini. Na ndani ya ofisi ya Rais, Ikulu, atakuwa anavaa tisheti na jinzi, kama wanavyovaa masela wa mtaani.