Prime
Mwenezi Bawacha asimulia chanzo kupigwa na mlinzi Chadema

Katibu Mwenezi Baraza la Wanawake Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Sigrada Mligo (34) akiwa amepumzika katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Njombe (Kibena) iliyopo Mkoani Njombe.
Muktasari:
- Simulizi ya Katibu Mwenezi wa Bawacha kabla ya kushambuliwa na kujeruhiwa na mtu anayedaiwa kuwa mlinzi. Heche akiri kuamuru atolewe ukumbini.
Njombe. Katibu Mwenezi Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Sigrada Mligo (34) ameeleza kuwa sababu ya kushambuliwa na mlinzi ni baada ya kunyimwa nafasi ya kujitetea juu ya tuhuma alizopewa, kwenye kikao cha ndani cha chama hicho kilichofanyika mkoani Njombe.
Amesema miongoni wa tuhuma dhidi yake ambazo ziliwasilishwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche aliyeongoza kikao cha ndani, ni kuendesha vikao bila kufuata utaratibu wa chama.
Mligo amesema hayo leo Machi 27, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hospitali ya Kibena, Njombe ambako amelazwa akiendelea na matibabu.
Amesema ndani ya kikao hicho muda ulipofika wa yeye kuzungumza alikatishwa na alipomweleza Heche ampe nafasi ya kuzungumza, aliambiwa akae chini.
Mligo amesema alimwambia Heche: "Utakuwa hutendi haki nisikilize, naomba unipe muda nikusimulie vizuri hili jambo, kwa sababu unatakiwa ulijue kiundani, lakini yeye akaniambia nikae chini, nikasema sawa mwenyekiti, lakini tunaonewa, naomba utusikilize. Akasema toka nje, nikasema sawa bosi wangu," amedai Mligo.
Mligo amesema alipotoka nje aliamua kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa Heche akiomba aruhusiwe kurudi kwenye mkutano, lakini Heche hakujibu.
Amedai akiwa bado nje, kuna watu walimfuata wakamweleza aingie ukumbini kuendelea na kikao, ili kumalizia hoja yake.
Mligo amedai wakati akienda kuingia ukumbini, ghafla alitokea mtu wa ulinzi na usalama wa chama hicho na kumshambulia.
Amedai mtu huyo alimpiga ngumi kichwani na kudondoka sakafuni.
Mligo amedai aliokolewa na polisi waliokuwa kwenye doria na kumpeleka nyumbani kwake, na siku iliyofuata aliamka na maumivu yaliyosababisha alazwe hospitali kwa matibabu.
"Tukaenda polisi tukachukua PF3 ndiyo tukaja hospitalini kama mnavyoona naendelea na matibabu, lakini maumivu ni makali sana, nazidi kuchoka nimegundua niliumia sana baada ya kudondoka pale chini," amesema Mligo.
Hata hivyo, licha ya Heche kukiri kutoa agizo la kumtoa nje katibu huyo wa uenezi, amesema chama chao ni cha demokrasia, hivyo watu wanashindana kwa hoja na sivyo vinginevyo.
Amesema kuhusu tukio la kushambuliwa kwa katibu mwenezi huyo mamlaka husika ndiyo inatakiwa kushughulika na mhusika ambaye amefanya shambolio hilo, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
"Chama chetu sisi ni cha demokrasia na watu wanashindana kwa hoja na kuhusu mtu aliyemshambulia, mamlaka zipo zishughulike naye," amesema Heche.
Tukio hilo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, lilitokea Jumanne Machi 25, 2025 wakati viongozi wa Taifa wa Chadema walipokuwa kwenye kikao cha ndani.
Kwa mujibu wa Kamanda Banga miongoni mwa mambo waliyoyajadili ni pamoja na taarifa zilizodai katibu huyo mwenezi alifanya mikutano kinyume na utaratibu wa chama hicho.
Kutokana na hilio, Kamanda Banga alisema kuliibuka taharuki iliyosababisha Mligo kutolewa nje kumpunguza munkari huku wajumbe wengine wakiendelea na kikao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe (Kibena), Ayoub Mtulo amesema walimpokea Mligo akiwa na majeraha madogo madogo, walimtibu na kumlaza.
"Tatizo kubwa lililokuwa linamkabili ni maumivu tu kutokana na kadhia ambayo amekutana nayo, lakini anaendelea vizuri" amesema Mtulo.
Pia, Mkuu wa Mafunzo na Hamasa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Ngerime amesema anachelea kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa limefanyika kinyume na utaratibu wa chama hicho kinachoongozwa na kanuni na misingi iliyowekwa.
“Mimi jukumu langu pale ilikuwa kuhakikisha kuna usalama…inawezekana Katibu huyo Mwenezi wa Bawacha walikosana na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche.
"Mimi nilikuwa nje nilipoingia ndani niliuliza katibu mwenezi yuko wapi wakasema wamemtoa kwa sababu kulikuwa na kutofautiana maneno na mwenyekiti wake, basi tukasubiria," amesema Ngerime.
Amesema baadaye inaonekana kuna mtu mwenye busara alimwambia Heche amwite Mligo na wakati anaenda kuitwa kuna mtu mmoja alipiga kelele nje kuwa haiwezekani Mligo kuingia kwenye mkutano, kisha akampiga ngumi.
Amemwomba Heche kukemea jambo hilo na kuchukua hatua ya kumpeleka mtuhumiwa polisi, ili akaadhibiwe na sheria kutokana na kufanya kosa la jinai la kumpiga kiongozi wa kitaifa hadharani.
Mweka hazina wa Baraza la Wanawake Chadema Mkoa wa Njombe, Faraja Mgimba amesema yeye pia alikuwa mmoja ya wajumbe wa kikao hicho kilicholenga usuluhishi wa mambo mbalimbali katika chama hicho.
"Wakati hatua zote zikiendelea za kuhoji wanachama na vitu ambavyo vimetokea, mkanganyiko mkubwa uliojitokeza baada ya mwenezi taifa kuelezea namna ambavyo amekuwa akipigwa vita katika kuandaa mikutano yake, hasa katika Jimbo la Makambako," amesema Mgimba.
Amesema alipokuwa akieleza jambo hilo ilihitajika vithibitisho, lakini baadaye ilionekana alifuata utaratibu ila alikosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa jimbo hilo.
Amesema baada ya mkanganyiko kuwa mkubwa, aliombwa kutoka nje kwa sababu alishindwa kuhimili mambo ambayo yalikuwa yanaendelea kwenye kikao hicho kwa kukosekana kwa masikilizano.
"Lakini, akiwa nje na yeye alijaribu kutaka kujua kinachoendelea ndani ya kikao kwa sababu yeye pia ni mwanachama, lakini walinzi waliokuwa nje walikuwa wanamzuia na sisi tuliokuwa ndani tulikuwa tunasikia kelele za kuzuiliwa kwake," ameongeza Mgimba.