Mbowe: Kuwa Chadema sio suala jepesi

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe wakati akizungumza na wananchi katika moja ya mikutano ya hadhara ya chama hicho. Picha na Mtandao

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe amesema mtu kuwa chama cha upinzani inahitaji ujasiri.

Mbowe ameyasema hayo leo Jumatatu Julai Mosi, 2024 alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Kabuku mkoani Tanga, ikiwa ni mwendelezo wa operesheni +255 inayoendelea katika mikoa ya kaskazini.

Mbowe amesema kuwa mwana- Chadema au mpinzani,  si jambo jepesi bali linahitaji ujasiri wa namna ya pekee.

Amesema viongozi wengi wa upinzani na Watanzania wazalendo wa nchi hii, wanapitia nyakati ngumu kutokana na uoga wa Serikali ya CCM.

"Marehemu Mzee Lowassa alithubutu kuingia Chadema, japo baada ya muda alirudi CCM tunatambua ujasiri wa uamuzi yake. Kitu pekee kitakachoiokoa Tanzania kutoka kwenye mikono ya watawala ni ujasiri na uthubutu wa mwananchi,”amesema Mbowe.

Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya awamu ya nne kabla ya kujiuzulu mwaka 2008 kufuatia kashfa ya Richmond, alijiengua CCM Julai 28, mwaka 2015 ikiwa ni siku chache baada ya jina lake kuchujwa pamoja na wagombea wengine 33 waliotia nia ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Hata hivyo, baadaye alipitishwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Mei Mosi, 2019 alitangaza kurudi tena CCM.

Kauli ya Mbowe inakuja ikiwa ni siku moja imepita baada ya Mchungaji Peter Msigwa, kuhamia CCM.

Msigwa aliwahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa wa chama hicho.

 “Chama hiki sio cha Mbowe, nimejenga chama chenu kimekuwa nchi nzima, msikiangalie kwa sura ya Mbowe kiangalieni kwa mambo kinayoyasimamia. Kwanza kinasimamia misingi minne ikiwemo haki, uhuru wa watu, misingi ya kuamini na maendeleo ya watu na sio maendeleo ya vitu,” amesema Mbowe.

Akizungumzia hali ya maisha kwa Mkoa wa Tanga, Mbowe amesema yamepanda sana na hali hiyo si mapenzi ya Mungu bali ni ya Serikali iliyopo madarakani aliyodai kuwa inapandisha kodi na kusababisha wananchi kuumia.

 “Fikiria Serikali inatenga zaidi ya Sh900 bilioni kununua magari ya Serikali, bado inaendeshwa kwa kodi zenu mnaendelea kuwa maskini kwa kuwa gharama za maisha ziko juu,” amesema na kuongeza;

  “Tunachowaomba watu wa Kabuku mjipange mkiacha chama kimoja kitawale peke yake kinalala usingizi kinasahau wananchi, ili chama chochote kiweze kujenga upinzani ni lazima kupata chama kingine chenye nguvu.”

Aidha, Mbowe amesema Chadema kinapopigia kelele upatikanaji wa Katiba mpya ni kutokana na mambo aliyoyaita kuwa ya ovyo yanayofanyika nchini.

“Tunataka wakati wowote unapokuwa kiongozi uamuzi utakaofanyika uwe sahihi na haki. Kwa sababu tumekubali maisha ni siasa na siasa ni maisha,  lazima mkate shauri mnasimama na Chama cha Mapinduzi (CCM) au mmnasimama na Chadema au mnaamua kukaa kimya mkubali fimbo na dhulma,” amesema.

Awali, akihutubia katika mkutano huo Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini Godbless Lema,  amesema dhambi kubwa kuliko zote duniani ni uoga, kwani kuna mtu akisikia mwananchi ana shida anaacha kila kitu kwa ajili ya kusikiliza watu.

 “Hakuna adhabu kubwa kabisa au jambo kubwa kabisa duniani linalomsibu binadamu kama  mauti, kwa sababu mauti inametengeneza binadamu na ardhi,”

 “Kama mtasubiri mikutano ya hadhara ndio mtoke kutoa taarifa za kuuawa kwa watu kesho ni zamu yako dhambi yoyote au ubaya wowote unaofanyika mbele ya macho yako halafu unafumba macho kuna siku atafanyiwa mtoto wako nao watafumba macho,”amesema.

Lema amesema anafahamu sana masuala ya mauaji kwa kuwa amewahi kuwa naibu waziri kivuli  wa mambo ya ndani ya nchi kwa miaka kumi akiwa mbunge.

Akizungumzia hali ya maisha ya watu wa Tanga Lema amesema mkoa huo una ardhi kubwa isiyokuwa na mazao yoyote,  licha ya kuwa na mawaziri na manaibu mawaziri

Amesema watu wa Tanga wamejaaliwa ardhi lakini hawalimi, vijana wamekuwa wakijipanga baabarani wakiuza vitu mbalimbali, huku akidai umasikini wao umesababishwa na watawala.