Lisu asema hana ubavu kuwania ubunge, Kingu atia neno

Muktasari:
- Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Oktoba 2025 wa udiwani, ubunge na urais.
Singida. Wakati harakati za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zikiendelea maeneo mbalimbali nchini, mmoja wa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Hamis Lisu wa Wilaya ha Ikungi mkoani Singida amesema hana nia tena ya kuwania ubunge wa Singida Magharibi.
Lisu ambaye mwaka 2020 alikuwa miongoni mwa makada wa chama hicho waliojitosa kwenye kura za maoni, alishindwa na Elibariki Kingu ambaye aliibuka kidedea kwenye kura hizo na uchaguzi mkuu.
Uamuzi wa kutojitosa tena kwenye kinyang'anyiro hicho amesema unatokana na mbunge aliyepo sasa (Kingu) ametekeleza vyema Ilani ya uchaguzi ya chama hicho kwa ufanisi.
Anachokisema Lisu ni sawia na kile kilichotokea kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi Juni 2024 ambapo viongozi waliokuwa kwenye msafara huo walimpongeza Kingu kwa kazi kubwa.
"Tumepita maeneo mengi, hapa kuna kazi kubwa imefanyika, sasa kama kuna mtu anataka kuja hapa anapaswa kujipanga kwelikweli na hii inaonesha jinsi mbunge alivyo karibu na wananchi wake," alisema mmoja aa wajumbe wa kamati kuu.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Sepuka ambao uliitishwa na Kingu jana Alhamisi, Februari 27, 2025, Lisu alikuwa miongoni mwa wahudhuriaji wa mkutano huo ambapo alisema kazi kubwa imefanyika chini ya utawala wa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.

"Sikuwahi kuhudhuria mkutano wa Kingu tangu apate ubunge, nafikiria mnaweza mkajua sababu ni nini, lakini leo Mungu ameniambia ebu nenda. Nashukuru mbunge kwa kuniita hapa, lakini nilivyoona vumbi lilivyotimka, nikajiuliza nina ubavu kweli," amehoji huku akishangiliwa na wananchi.
"Ubavu wa kupambana na huyu bwana (Kingu) ninao kweli? Ninawaomba wale waliokuwa wananishawishi nichukue fomu washindwe na walegee," amesema Lisu huku vicheko na makofi yakiibuka uwanjani hapo.
Hata hivyo, Lisu amesema wakati Kingu anahutubia alijiuliza au awanie udiwani kwa sababu siasa ipo kwenye damu.
"Nimefanya uamuzi wenye busara kutokana na mambo makubwa yaliyofanywa na viongozi wetu, pamoja na upendo wao," amesema Lisu.
Kwa upande wake, Kingu amesema kwa sasa anaendelea kufanya kazi kwa bidii ya kuwatumikia wananchi wake kama alivyoahidi wakati anapewa ridhaa ya kuwa mbunge mwaka 2020.
“Wananchi wangu wanataka maendeleo na kuona natekeleza kwa mafanikio kila nilichoahidi na zaidi, najua huu ni mwaka wa uchaguzi na muda ukifika mambo yatajulikana. Kwa sasa chama bado hakijapuliza kipenga, “ amesema Kingu.