Prime
Baba Levo, AG kidedea, mahakama yakataa nyaraka kukaguliwa
Muktasari:
- Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Victoria Nongwa, mahakama ilisema kiapo chao kilikuwa na maelezo ya kuambiwa na yasiyo ya kweli.
Kigoma. Mahakama Kuu Kigoma, imekataa maombi ya kukagua na kujiridhisha kuhusu nyaraka mbalimbali za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 katika jimbo la Kigoma Mjini.
Nyaraka hizo ni pamoja na kujiridhisha juu ya uwepo wa nakala halisi ya daftari la wapiga kura lililotumiwa katika kila kituo cha uchaguzi kuidhinisha mpigakura, fomu za matokeo kwa kila kituo na matokeo ya ubunge katika vituo vyote.
Uamuzi wa kuyakataa maombi hayo yaliyowasilishwa na wapigakura wanne wa jimbo la Kigoma Mjini--- Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, umetolewa jana, Machi 2, 2026 na Jaji Victoria Nongwa wa mahakama hiyo.
Maombi hayo yalifunguliwa na wapigakura hao, wanaowakilishwa na Wakili John Seka, dhidi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, mbunge wa jimbo hilo, Clayton Chipando maarufu “Baba Levo”, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Maombi hayo yaliambatana na kiapo cha pamoja cha waleta maombi, na walieleza kuwa wao ni walalamikaji katika shauri la uchaguzi namba 28949 la 2025.
Walidai hawakuridhishwa na utaratibu wa uhakiki thabiti wa mpigakura kupitia nakala ya daftari la kudumu la wapigakura, ubandikwaji wa matokeo katika ngazi ya vituo, na kwamba hakuna nakala halisi au durufu ya matokeo ya kila kituo na ya jimbo zima.
Walieleza kuwa nyaraka zinazohusiana na utaratibu mzima wa uchaguzi zimehifadhiwa na mjibu maombi wa kwanza, ambazo ni fomu namba 21B ya matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika kituo cha kupigia kura na jimbo zima.
Pia fomu namba 22B ya matokeo ya uchaguzi wa ubunge, fomu 23B ya matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika jimbo kwa kila chama na 24B ya matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika jimbo, hivyo waliomba wazikague na kupewa.
Wajibu maombi wa kwanza, ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi Kigoma Mjini, na AG walipinga maombi hayo kupitia kiapo kinzani cha David Rwazo, aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini.
Kwa upande wa mjibu maombi wa pili, ambaye ni Baba Levo, alipinga maombi hayo kwa kiapo cha wakili wake, Daniel Rumenyela.
Hoja za waleta maombi
Katika usikilizaji, waleta maombi waliwakilishwa na Wakili Seka, wakati mjibu maombi wa kwanza na wa tatu waliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Mark Mulwambo, Vivian Methodi na Lessi Majala, pamoja na mawakili waandamizi George Kalenda na Edwin Webiro.
Kwa upande wake, mjibu maombi wa pili, Baba Levo, aliwakilishwa na mawakili wa kujitegemea, Emmanuel Msasa na Daniel Rumenyela.
Katika hoja zake, Wakili Seka alisema maombi ya aina hiyo yanaruhusiwa kupitia Kanuni ya 18(1) ya Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge, na Kanuni ya 24 inaruhusu matumizi ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Wakili Seka, alieleza kuwa wajibu maombi wa kwanza na wa tatu, katika kiapo kinzani aya ya 8, wanakiri kuwa nyaraka zote wanazo na walishawapatia mawakala wote waliokuwepo kwenye vituo na kwenye majumuisho ya kura.
Wakili Seka alisema waleta maombi walikuwa wapigakura na hawakuwa sehemu ya watu waliopatiwa nyaraka hizo, na kwamba wajibu maombi hao katika kiapo chao walisema hawakuona haja ya kuambatanisha nyaraka hizo katika shauri la msingi.
Hivyo, aliiomba Mahakama itoe amri kwa mjibu maombi wa kwanza, ambaye ni msimamizi, ili waleta maombi waweze kupekua nyaraka hizo.
Aliendelea kueleza kuwa mashauri ya uchaguzi, kama yalivyo mashauri mengine ya madai, si mashauri ya kushtukizana bali yanaendeshwa kwa uwazi bila kuficha karata, ndiyo maana kanuni ya 18(1) imeruhusu kupatiwa nyaraka.
Kwa mujibu wa Wakili Seka, aliongeza kusema kuwa maombi ya kuomba nyaraka si jambo linalobanwa na taratibu za kiufundi, mahakama inatakiwa kuangalia haki ya msingi bila kufungwa na mambo ya kiufundi ya kisheria.
Kulingana na wakili huyo, sheria imeweka sharti kuwa kama nyaraka hizo zitasaidia kumaliza shauri kwa haki, na endapo mahakama itaona nyaraka hizo zikitolewa katika hatua za awali zitaondoa gharama na muda wa kusikiliza shauri, itaruhusu.
Majibu ya wajibu maombi
Katika hoja zake, Wakili Webiro, anayemwakilisha Msimamizi na AG, aliibua hoja kuwa kiapo cha waleta maombi kina uongo, kwani wakati wa maswali ya dodoso walikiri kuwa maelezo yaliyopo kwenye kiapo ni ya kuambiwa.
“Wamekiri kuwa maelezo yaliyopo kwenye kiapo ni ya kuambiwa, kama ambavyo mleta maombi wa nne aliwataja watu waliompa hizo taarifa. Ili kujua kuwa maelezo ya kiapo ni ya uongo, tunaangalia uthibitisho na waleta maombi wanathibitisha kwamba yote waliyoyasema yapo ndani ya uelewa wao binafsi.”
Wakili alitaja aya ya 6 ya kiapo cha waleta maombi kuwa kimesheheni uongo, kwa waleta maombi kukataa kwamba hawajawahi kuona au kupata nakala halisi au durufu ya matokeo ya vituo vyote ndani ya jimbo la Kigoma Mjini.
Lakini wakili huyo alisema, wakati wa maswali ya dodoso, mleta maombi wa kwanza alikiri mahakamani kuwa wana nakala za matokeo na waliona hazikujazwa kwa kufuata matakwa ya sheria.
Alisema mleta maombi wa pili naye alikiri kuwa wana nakala za matokeo karibu nusu ya jimbo zima, na hiyo iliwasaidia kuona kuwa ujazaji wa hizo fomu una upungufu, hivyo kusababisha wafike mahakamani kuleta malalamiko yao.
Wakili aliendelea kueleza kuwa pale panapokuwa na ushahidi wa uongo kwenye kiapo, kama ilivyo katika shauri la Ignazio Messina dhidi ya Willow Investments SPRL, si kiapo na hakiwezi kutumika kama ushahidi.
Kuhusu nini kifanyike inapogundulika kiapo kina uongo, wakili huyo alirejea mashauri ambayo mahakama ilisema pale ambapo kiapo kina uongo hakiwezi kufanyiwa kazi, na kiapo chenye aya za uongo kinaathiriwa chote.
Kuhusiana na maombi yenyewe, Wakili Webiro alikiri kuwa umuhimu wa nyaraka ndicho kigezo kikuu cha mahakama kuzingatia kwenye maombi ya aina hiyo, lakini aliona waleta maombi hawakukidhi sharti hilo, kwani hawakueleza umuhimu wa kila nyaraka inayoombwa na namna itakavyowasaidia.
Kwa upande wa mjibu maombi wa pili, Wakili Msasa alianza kwa kuasili kiapo kinzani walichowasilisha na kusema maombi dhidi ya mjibu maombi wa pili hayakuwa na msingi wowote, kwani hakuna nyaraka inayoombwa kutoka kwake.
Wakili Rumenyela alisema neno “hatukumbuki” linaonesha ukamilifu wa dhana ya kutafuta ushahidi kwa waleta maombi, hivyo wanataka upande wa pili uwakumbushe, wakati wao ndio waliofungua shauri.
Uamuzi wa jaji
Katika uamuzi wake, Jaji alisema wakati wa mawasilisho hoja mbili zimejitokeza, moja, kuwa kiapo cha waleta maombi kimejaa uongo na hakipaswi kuzingatiwa na pili kama maombi hayo yamekidhi sifa za amri zilizoombwa kutolewa.
“Kwenye mawasilisho, Wakili Webiro alirejea kiapo cha waleta maombi na katika maswali ya dodoso, ambapo waleta maombi walisema kuna baadhi ya maelezo waliambiwa, lakini kwenye uthibitisho wanasema yote ni kwa ufahamu wao.
“Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi, viapo vinapaswa kujikita katika ukweli ambao muapaji anaweza kuthibitisha kwa maarifa yake binafsi, isipokuwa katika maombi ya amri ya mpito, ambapo taarifa za imani yake zinaweza kukubaliwa,” alisema Jaji Nongwa.
“Hivyo, kuna mapungufu ya aina tofauti ambayo yanaweza kujitokeza kwenye kiapo, na hatua za kuchukuliwa nazo pia zinatofautiana. Kwa mfano, moja, kiapo ambacho mapungufu yapo kwenye uthibitisho, Mahakama inaweza kuruhusu kasoro hiyo ikarekebishwe,” alieleza Jaji na kuongeza kuwa;
“Pili, kiapo ambacho kina hoja, uvumi, hitimisho na maelezo ya kuambiwa; aya ambazo zitaonekana kuwa na kasoro hizo zitaondolewa, na Mahakama itaangalia kama aya zinazobaki ni ushahidi tosha.”
“Tatu, kiapo chenye taarifa za uongo; hapo ndipo hoja za wajibu maombi zilijengwa. Sheria iko wazi kuwa kiapo ambacho kimesheheni taarifa za uongo hakiwezi kukubaliwa na Mahakama na kutumika katika shauri kama ushahidi.”
Kutokana na sheria, Jaji alisema ni wazi kuwa watu pekee wanaoruhusiwa kuwepo kwenye eneo la kuhesabu kura, pamoja na wengine waliotajwa na sheria, ni mgombea pamoja na wakala wa chama cha siasa kilichoshiriki uchaguzi.
“Waleta maombi, tofauti na kituo walichopiga kura, wasingeweza kujua nini kilikuwa kinaendelea katika vituo vingine na jimbo zima la Kigoma Mjini kwa ujumla, isipokuwa tu chama cha siasa, mgombea ubunge au wakala,” alisema.
“Baada ya kupitia kiapo cha waleta maombi, hasa aya ya 4, 7 na 8, ni wazi baadhi ya maelezo kama kunakili matokeo ya uchaguzi wa ubunge na kutobandikwa kwa matokeo katika ngazi za vituo katika jimbo hayakuwa kwenye ufahamu wa waleta maombi, hivyo kufanya maelezo ya ukiukwaji wa utaratibu wa kuhesabu kura katika vituo vyote vya jimbo kuwa maelezo ya kuambiwa.”
“Mkanganyiko wa ushahidi wa waleta maombi, kwanza kusema hawana fomu wanazoomba na baadaye kubadilika kusema wanazo baadhi ya vituo, unaathiri uaminifu wa ushahidi wao juu ya kile wanachokisema, kwani Mahakama itashindwa kuchagua upi ni ukweli wa muapaji,” alisisitiza Jaji Nongwa.
“Nakubaliana na wajibu maombi kuwa kiapo cha waleta maombi kimejaa maelezo yasiyo ya kweli, kwa sababu maombi ya kuomba kupekua nyaraka za uchaguzi hayajaungwa mkono na ushahidi wa mgombea, mawakala wa chama au mtu mwingine anayeruhusiwa kuwepo wakati wa kuhesabu kura, kujaza fomu na kubandika matokeo.”
Jaji alisema, baada ya kuhitimisha kuwa kiapo kina maelezo yasiyo na ukweli, ni wazi kuwa hakuna ushahidi wa kuiwezesha mahakama hii kusikiliza na kutoa amri ambazo zimeombwa na waleta maombi, hivyo maombi yao yanatupiliwa mbali.