Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uvaaji hatarishi wa nguo za ndani

Muktasari:

“Ikitokea nimeanguka ghafla, nikapoteza fahamu kitu cha aibu nitakachokipata ni kwenye hii sidiria niliyovaa. Sikumbuki mara ya mwisho kuifua, kila nikitaka kufua najikuta nimeivaa tena, sasa nikidondoka mkasema mnilegeze nguo zilizobana mwilini ikifika kwenye sidiria itakuwa shughuli.


Dar es Salaam. “Ikitokea nimeanguka ghafla, nikapoteza fahamu kitu cha aibu nitakachokipata ni kwenye hii sidiria niliyovaa. Sikumbuki mara ya mwisho kuifua, kila nikitaka kufua najikuta nimeivaa tena, sasa nikidondoka mkasema mnilegeze nguo zilizobana mwilini ikifika kwenye sidiria itakuwa shughuli.

“Naona kidogo mie ina nafuu, nilifua wiki iliyopita, ila yale maji niliyoloweka nilipoyaangalia niliishia kucheka, yaani yalikuwa mazito ilibidi nifue mapovu matatu, ili kuirudisha katika hali yake, kiukweli ni hatari.”

Hiyo ni sehemu ya mazungumzo kati ya wanawake wawili waliokuwa wakielezea namna ambavyo mazoea yanawafanya wasifue sidiria na kujikuta wakirudia kuvaa nguo hiyo ya ndani kwa muda mrefu.

Tabia hii inaonekana kuwa sugu kwa wanawake wengi, hasa wanaofanya kazi au biashara zinazowafanya muda mwingi wawe kwenye shughuli za uzalishaji.

Kulingana na maandiko mbalimbali ya wataalamu, angalau sidiria ifuliwe baada ya kuvaliwa mara mbili au kama inawezekana kila inapotoka mwilini kama ambavyo inapaswa kufanyika kwa nguo nyingine za ndani.

Hata hivyo, suala hili limeonekana kuwa gumu kwa wanawake wengi, kati ya wanawake sita waliohojiwa na gazeti hili, ni mmoja pekee ndiye aliyeeleza kuwa ana utaratibu wa kuvaa sidiria mara moja na kuifua.

Watano waliosalia walieleza wanavaa sidiria zaidi ya mara moja na wengi wao walikwenda mbele zaidi na kueleza sidiria ya rangi nyeusi inaweza kukaa mwilini hata kwa zaidi ya wiki bila kufuliwa.

Akizungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina, mmoja wa wanawake hao alieleza wakati wa joto ndiyo anaweza kuvaa sidiria mara nne hadi tano bila kufua, lakini msimu wa baridi anaivaa hadi wiki tatu.

Suala la kupendelea kuvaa sidiria moja liligusiwa pia na Salome Machaga, anayeeleza licha ya kuwa na sidiria kadhaa, ipo moja anaipenda zaidi na anaamini inamkaa vizuri mwilini, hivyo analazimika kuivaa mara nyingi.

“Nafanya kazi kwenye mgahawa, naondoka nyumbani asubuhi narudi usiku. Nikiivua usiku nikiamka asubuhi ninayo. Matokeo yake naivaa kwa muda mrefu bila kuifua,” anasema.


Hali ikoje kwa wanaume?

Wakati sidiria ikiwa donda sugu kwa wanawake, hali iko hivyo pia kwa wanaume kwa upande wa nguo za ndani, kwa maana ya boksa na singlendi zinazovaliwa kabla ya kuvaa shati au fulana.

Ripoti moja ya utafiti uliofanyika nchini Marekani inaonyesha asilimia 45 ya wanaume nchini humo wanavaa nguo za ndani zaidi ya mara mbili, huku asilimia 13 wakikiri kuvaa boksa kwa zaidi ya wiki moja kabla ya kuisafisha.

Tofauti na ilivyo kwa wanawake kwamba anaweza kupendelea zaidi kuvaa sidiria moja, wanaume kwao haiko hivyo, chanzo kikubwa cha kuvaa nguo ya ndani zaidi ya mara moja ni uvivu na tabia ya uchafu aliyonayo mtu husika.

Emmanuel Jangua anasema anaweza kuvaa kwa wiki moja lakini anawafahamu rafiki zake ambao wanaweza kuvaa boksa kwa wiki mbili hadi tatu bila kufua.

“Kinachofanyika ni kwamba mtu anaivaa wiki halafu anaiweka sehemu inayoruhusu kupigwa na upepo, hapo katikati anaweza kubadilisha akavaa nyingine, wiki ikiisha anairudia ile yaani mwendo unakuwa huo,” anasema Jangua.

Kwa upande wake, Hassan Njenga anasema tabia hiyo huwakumba zaidi wavulana au wanaume wanaoishi wenyewe.

“Nimesoma shule ya bweni, haya masuala ya boksa kurudiwa ni kitu cha kawaida kabisa. Mwamba anapiga hata siku sita sio ajabu kabisa,” anasema.


Kiafya inakuwaje

Inaelezwa hali hii inaweza isiwe na athari za moja kwa moja kiafya kwa kila mtu, bali kulingana na aina ya ngozi ya mhusika na uwezo wake katika kuhimili mashambulio yanapotokea.

Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka kutajwa jina anasema si rahisi kwa ngozi kuathirika ndani ya muda mfupi baada ya kuvaa nguo chafu.

“Kwa ngozi kuathirika kwa sababu ya nguo chafu haiwezi kuwa kwa ndani ya muda mfupi, labda kutoa harufu na ikitokea mwili umechubuka kuna uwezekano wa wale bakteria waliokuwa kwenye nguo wakaingia mwilini, hivyo ni muhimu kufanya usafi wa nguo zote si sidiria au boksa,” anasema daktari huyo.

Kulingana na andiko la daktari wa magonjwa wa ngozi, Alok Vij nguo ya ndani inapovaliwa mwilini inabeba mafuta, losheni na vitu vyote vinavyopakwa kwenye ngozi, endapo itaendelea kuvaliwa bila kufanyiwa usafi ni rahisi kutengeneza fangasi ambao wanaweza kuwa tatizo kwenye ngozi.

“Ikifikia hatua hii upo uwezekano mkubwa wa sidiria kutoa harufu maana mrundikano wa mafuta na jasho kwenye nguo ni chanzo kikubwa cha harufu mbaya.

“Upo uwekezano pia wa kupata miwasho na vipele vidogo vidogo endapo ngozi yako ni rahisi kushambuliwa na fangasi na bakteria wanaotokana na uchafu, hili linaweza lisimtokee kila mtu, wapo wale ambao ngozi zao ni rahisi kupata maambukizi au kushambuliwa, hivyo wanapaswa kuongeza umakini,” anasema Dk Vij.