Namna ya kukabiliana na tatizo la kuziba mishipa ya damu ya vena

Muktasari:
Baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuchangia tatizo ni kuishi bila kufanya mazoezi, uzito kupita kiasi na kusimama muda mrefu
Wiki iliyopita, miongoni mwa Makala tulizochapisha, ilikuwapo ya binti wa miaka 22, Theresia Costantine ambaye alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya mishipa inayosafirisha damu miguuni. Tatizo hilo lilisababisha kidonda alichopata mguuni kutopona na kuongezeka siku hadi siku jambo ambalo alielezea linahatarisha mguu wake kukatwa hivyo kuomba wasamaria wema wamsaidie.
Wasomaji wengi walipiga simu wakitaka ufafanuzi zaidi juu ya ugonjwa huo. Kwa kifupi huu ni ugonjwa unaotokana na kuziba kwa mishipa ya vena, hivyo kusababisha damu kushindwa kuingia na kutoka.
Kutokana na shauku hiyo, leo tunauelezea kwa undani namna unavyoanza, athari zake na jinsi ya kukabiliana nao.
Kuziba kwa mishipa ya vena
Vena ni mishipa inayosafirisha damu kutoka kwenye misuli na kuirudisha kwenye moyo. Moyo unapopokea damu ambayo ina upungufu wa hewa ya oksijeni, huisukuma kwenda kwenye mapafu ili isafishwe na kuongezewa hewa safi ya oksijeni.
Baada ya hapo moyo husukuma damu yenye oksijeni kwenda sehemu mbalimbali za mwili kwa ajili ya kuendeleza afya na uhai.
Mishipa ya vena hasa inayotoa damu miguuni inapoathirika kwa kuvimba, kujikunja, kupoteza uwezo wa kuvutika na kuziba, inasababisha damu kuganda ndani yake.
Mishipa ya vena inafikia hatua hii, baada ya valvu zake kudhoofika na kusababisha damu kurudi nyuma na kurundikana ndani ya mishipa badala ya kurudishwa kwenye moyo.
Maradhi haya ya mishipa yanaweza kusababisha maumivu, kuathirika kwa ngozi na kusababisha vidonda miguuni.
Nini kinasababisha tatizo
Baadhi ya mambo yanayochangia kutokea kwa maradhi haya ni pamoja na kuishi maisha ya kubweteka bila mazoezi, kusimama au kukaa kwa muda mrefu huku ukiwa umekunja miguu, maarufu kama kukunja nne au kuvaa mavazi yanayobana sana kiunoni au kwenye mapaja.
Mambo mengine yanayochangia ni pamoja na ujauzito kwa wanawake, uzee, majeraha kwenye miguu na kunenepa kupita kiasi.
Wanawake wenye uwiano wa uzito kwa urefu (BMI) kati ya 25 hadi 29.9, wana hatari zaidi ya kupata maradhi haya kwa asilimia 50 ikilinganishwa na wanawake wenye uzito wa wastani.
Hali hii kwa kiasi kikubwa huwapata wanawake zaidi ikilinganishwa na wanaume. Katika nchi zilizoendelea, inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wanawake na asilimia 10 ya wanaume wanaokwenda hospitalini, wanakabiliwa na maradhi haya.
Mabadiliko ya vichocheo vya jinsi na homoni hasa wakati wa kubalehe, wakati wa ujauzito hasa wa watoto pacha, wakati wa komahedhi au pale mwanamke anapotumia vidonge vya kupanga uzazi, huongeza hatari ya kupata maradhi ya kuvimba kwa vena.
Swala la urithi pia linachangia kutokea kwa hali hii. Pale na wazazi wote wawili wanapokabiliwa na tatizo hili, uwezekano wa mtoto wao kupata maradhi haya unaweza kufika asilimia 90.
Maradhi haya yakiwa katika hatua za mwanzo, yanaweza kutibiwa kwa kurekebisha mtindo wa maisha kulingana na ushauri wa kitabibu.
Mgonjwa anashauriwa kula vyakula vinavyoimarisha afya ya mishipa ya damu na kufanya damu kuwa nyepesi. Jamii inapaswa kuzingatia ulaji wa matunda na mboga kwa wingi na kuepuka mafuta yanoyoganda na nyama zenye mafuta. Mgonjwa pia anashauriwa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuepuka kukaa au kusimama kwa muda mrefu.
Kupunguza unene wa mwili na kuepuka mavazi yanayobana sehemu za kiuno pia ni njia zinazosaidia.
Inashauriwa pia kukaa na kuinua miguu juu ya usawa wa moyo angalau kwa dakika 15 mara kadhaa kwa siku ili kurahisisha urudishaji wa damu kwenye moyo. Lakini hali inapozidi kuwa mbaya, ikiambatana na maumivu makali pamoja na damu kuganda ndani ya mishipa, daktari anaweza kupendekeza matibabu ya kuvisha miguuni vifaa maalumu vinavyojulikana kama compression stockings. Vifaa hivi husaidia damu isirundikane katika vena za miguuni.
Hali ikizidi kuwa mbaya, matibabu ya upasuaji yanaweza kufanyika. Kwa njia hii mishipa yenye matatizo inafungwa au inaondolewa. Ikifungwa inatoa nafasi ile mipya ifanye kazi.
Matibabu haya yanaifanya damu irudishwe kwenye moyo kupitia kwenye vena zingine ambazo hazijaathirika.
Ili kukabiliana na hali, madaktari pia wanaweza kutumia tiba ya kuingiza kemikali maalumu kwa njia ya kudunga sindano ndani ya mishipa ya vena na kusababisha makovu ndani yake. Makovu haya huifanya vena izibe na kuzuia damu kuingia ndani yake. Njia hii kwa lugha ya kitabibu hujulikana kama Sclerotherapy.
Katika hospitali kubwa, madaktari wanaweza kufanya upasuaji kwa kutumia kamera maalumu ya video. Aina hii ya upasuaji hujulikana kama Endoscopic Vein Surgery.
Katika upasuaji huu daktari anachana sehemu ndogo kwenye ngozi karibu na mshipa ulioathirika, kisha kwa kuongozwa na kamera, anaingiza kitu ndani ya mshipa na kuuziba. Mara nyingi upasuaji wa aina hii unafanyika pale maradhi haya yanaposababisha vidonda visiyopona kwenye ngozi, hasa miguuni.
Wataalamu wengine hupendekeza tiba ya upasuaji kwa kutumia mionzi maalumu ijulikanayo kama Laser Surgery. Hii ni njia ya kisasa ya upasuaji ambayo haihitaji kuchana ngozi wala kumchoma mtu sindano ya aina yoyote. Utafiti uliofanywa mwaka 2014 na Taasisi ya Taifa ya Tafiti za Afya ya Uingereza (NIHR) na kuchapishwa katika jarida la New England Journal of Medicine, ulibaini kuwa matibabu ya upasuaji kwa kutumia mionzi maalumu ijulikanayo kama Laser Surgery, ni bora zaidi.
Mtafiti mkuu wa utafiti huo, Profesa Julie Brittenden, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Mishipa katika Chuo Kikuu cha Aberdeen anasema: “Kile ambacho utafiti huu umetuonesha ni kwamba, kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji, ulio bora zaidi ni wa njia ya laser.”
Watafiti hao walifikia hitimisho hilo baada ya kulinganisha njia tatu za matibabu ya maradhi haya kwa njia ya upasuaji. Utafiti huo ulihusisha wagonjwa wapatao 798 kutoka katika vituo 11 vya tiba za maradhi haya nchini Uingereza.
Wale waliofanyiwa wa laser walionekana kutatua tatizo kwa haraka zaidi.