Mtu chake apendacho hakina ila machoni

Muktasari:

  • Watoto wa mjini wanaikumbuka Happy Photo Studio enzi hizo mitaa ya Kariakoo. Nje yake mabitozi walijazana kungoja zamu zao za kupiga picha kila wikiendi. Walivaa mashati ya kubana (slim fit), suruali za kumwaga (bugaluu) na viatu vya ghorofa (raizoni). 

Kwa wakati mgumu wa maombolezo baada ya kumpoteza mhafidhina wa Kiswahili, Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi. Kwa jinsi ninavyozielewa jitihada zake kuienzi lugha yetu adhimu, kila ninapolisikia jina lake akili yangu huligeuza kuwa “Ali hasa ni Mwinyi”. Leo nimekumbuka mbali sana baada ya kumkumbuka mzee wetu huyu.

Watoto wa mjini wanaikumbuka Happy Photo Studio enzi hizo mitaa ya Kariakoo. Nje yake mabitozi walijazana kungoja zamu zao za kupiga picha kila wikiendi. Walivaa mashati ya kubana (slim fit), suruali za kumwaga (bugaluu) na viatu vya ghorofa (raizoni). 

Pozi bora ya picha enzi hizo ilikuwa ni kuchuchumaa huku mkono mmoja ukiwa kiunoni na mwingine ukinyosha alama ya “V” pembeni ya mitungi ya maua.

Enzi hizo hakukuwa na ujanja wa “kujiselfii”. Watu hawakuwa na jeuri ya kurusha picha whatsap wala insta kuwaringishia wenzao jinsi wanavyofakamia michemsho na vichwa vya mbuzi klabu..

Tena wakati huo walikuwa bado hata kuwasha TV kuangalia ligi za Ulaya, Orijino Komedi wala Mizengwe. Kwenye mtandao ndio kabisaaaaa… hakuna aliyewahi kuota kurusha kigodoro chake Youtube. Uvumbuzi na ugunduzi ndio uliotufikisha hapa.

Uvumbuzi na ugunduzi ni vitu vinavyofanana, lakini naamini kuvumbua ndio kunakotangulia. Anayevumbua dawa ya kichwa huanza, kisha kufuatiwa na anayegundua kuwa dawa hiyo hutibu pia maumivu ya mwili.

Kuna mwanamuziki anayeheshimika sana katika visiwa vya Carribean alimkemea mgunduzi maarufu duniani kwa kujiita “mvumbuzi”. Mwanamuziki huyu mwenye heshima ya “Babu” aliimba kuwa Christopher Columbus ni mwongo na mzandiki anayeidanganya dunia.

Aliimba: “Eti anasema yeye ndiye mtu wa kwanza kuivumbua Jamaika. Je, Wahindi Wekundu (Arawak Indians) waliokuwa waasilia wa hapo walikuwa wapi”. Sijui kama jamaa zangu Wasukuma walishawahi kujiuliza juu ya “mvumbuzi wa Ziwa Victoria”. Nasikia wenyewe walilibatiza ziwa lao kwa jina la Nyanza, lakini akapita mzungu aliyeitwa Speke.

Akalishangaa ziwa kwa ukubwa wake ulioyazidi yote barani na la pili kwa ukubwa duniani kwa maziwa ya maji safi. Akaamua kumtunukia zawadi hiyo Malkia wake aliyeitwa Victoria. Kumbe basi yeye alikuwa ni Mwingereza wa kwanza kuliona kama Columbus alivyokuwa Mtaliano wa kwanza kuiona Jamaika. Kwani Mhehe wa kwanza kuliona soko la Kariakoo ndiye aliyelivumbua?

Historia inasema mara baada ya kugundua kuwa keshaumbwa na ndio keshafika hapa duniani, binadamu alikuwa akivumbua jambo kila baada ya muda fulani. Alivumbua chakula alipobanwa na njaa, akavumbua mavazi baada ya kugundua kuwa yu mtupu, na akaja kuvumbua malazi alipomenywa na baridi na mvua.

Baadaye alivumbua kilimo na ufugaji kuwa ni njia kuu ya kuzalisha chakula. Lakini changamoto walizokutana nazo (hasa baridi kali) zilimlazimisha kukusanya kuni na kugonga mawe hadi cheche zikaruka, moto ukavumbuliwa. Kwa kutumia moto aliweza kufua majembe ya kulimia, mashoka ya kukata kuni na mikuki ya kuwindia. Akaanza kutumia wanyama kama usafiri wa kubeba mizigo yake alipokwenda kubadilishana bidhaa na wezake wa mbali.

Hali ya kusafiri mwaka mzima kutoka Tanzania hadi Misri kwa ngamia na punda ikamchosha. Ilimlazimisha kuvumbua mashine iliyombebea mzigo mkubwa na mzito katika safari ya muda mfupi. Lakini pia binadamu alivumbua mashine ya kutunza kumbukumbu na kuhesabia bidhaa zake.

Alipofika kwenye kompyuta, binadamu sasa aliweza kuishi Tanzania lakini akafanya kazi kila siku Ujerumani kwa kutumia mtandao. Hakuishia hapo maana imesemwa kwamba binadamu hataacha kuvumbua na kugundua hadi mwisho wa uhai wake. Anapomaliza muda wake anapokewa na wengine, nao watapokewa na wengine hadi kitakapoeleweka.

Kwa mara ya kwanza sasa tuna kizazi kinachobomoa badala ya kuendeleza yale yaliyovumbuliwa. Wakati huu wa teknolojia watu wanadhani kila jambo limeshakuwapo, hivyo wanachokifanya ni kuangalia upande hasi: “kama hiki kisingekuwepo ingekuwaje?”
Au: “Kama nguo zingeonesha maungo ya mwili kungetokea nini?” Hii ndiyo ileile ya kubadilisha mtandao kutoka kupashana habari na kusambaza ngono, matusi na malumbano.

Nilimnasa kwa masikio yangu mtangazaji wa kituo kimoja cha redio akisema: “Mimi nirianza kuongea kwa ufasaa ruga ya Kiswairi na Kiingleza nikiwa shure ya chekechea”! Ingelikuwa nimesoma kwenye maandishi nisingelalamika sana kwani ningedhani ni makosa ya uchapaji. Lakini nilishtuka sana nilipogundua kuwa wapo wanaojifunza kupitia kwake. 

Nao wakiongezea makosa yao sijui tutapata matokeo yapi! Tukae tukijua wale akina babu waliokesha kutengeneza lugha hawakufanya kazi ya kitoto. Lugha ni sauti za nasibu zinazokubaliwa na jamii, lakini mpaka kupata muundo wake si kazi nyepesi. Baada yao wakaja akina Mzee Ruksa kuienzi na kuilinda lugha isipotee. Ajabu hivi sasa wanakuja mazombi kuiharibu.