Misingi ya sifa za wanamuziki imebadilika sana zama hizi

Muktasari:

  • Hali hii imetokana na kubadilika kwa mfumo wa utayarishaji wa muziki. Katika zama hizi sauti za vyombo vinavyo msindikiza muimbaji, havilazimiki kupigwa na binadamu tena, bali hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta kwa akili ya mtayarishaji wa muziki.

Dar es Salaam. Sababu ambazo zinafanya mwanamuziki awe maarufu, zimebadilika sana katika zama hizi, kiasi cha kwamba asilimia kubwa ya wasanii walio maarufu katika muziki ni waimbaji.

Hali hii imetokana na kubadilika kwa mfumo wa utayarishaji wa muziki. Katika zama hizi sauti za vyombo vinavyo msindikiza muimbaji, havilazimiki kupigwa na binadamu tena, bali hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta kwa akili ya mtayarishaji wa muziki.

Katika kutambulisha au kutangaza muziki, video za muziki huonesha muimbaji  pekee akiwa ndiye nyota wa wimbo, hivyo kuishia kuwa ndiye pekee anayepata umaarufu.

Hebu turudi nyuma, hapo kale hali ilikuwaje? Kwanza kabisa mfumo wa muziki ulikuwa tofauti, mwanamuziki ilikuwa lazima awe katika kundi la wanamuziki ili kukamilisha wimbo, katika kundi kila mwanamuziki ana nafasi yake ambayo ni muhimu sana katika kukamilisha wimbo.

Katika bendi kulikuwa na waimbaji kadhaa ambao walikuwa na sauti zenye nafasi mbalimbali, kama vile sauti ya kwanza, ya pili na ya tatu, na hao wote mara nyingine walikuwa wakishirikiana katika kuimba wimbo mmoja.

Katika bendi kulikuwa na wanamuziki waliokuwa wakipiga vyombo mbalimbali, vinanda, vyombo vya kupuliza, magitaa ya aina mbalimbali kama vile gitaa la solo, gitaa la ridhim, gitaa la bezi na mara nyingine kulikuwa na gitaa lililoitwa ‘second solo’.

Katika bendi pia kulikuwa na wapiga ngoma za aina mbalimbali kama vile  drums na tumba au wengine huziita conga, na wote hao kwa pamoja walishiriki kikamilifu kutengeneza na hatimaye kupiga wimbo.

Katika mazingira hayo, umaarufu ulienda  kwa wanamuziki wa nafasi mbalimbali katika bendi. Kuna wanamuziki wengi sana ambao hawakuwahi kuwa waimbaji, lakini walikuwa maarufu na wengine bado maarufu sana katika jamii ya wapenzi wa muziki wa dansi, hebu niwataje wachache.

Hakika nitakaowataja ni sehemu ndogo sana ya waliokuwa maarufu, lakini wao ni mfano tu wa hali ilivyokuwa.  Nianze na wapiga tumba, zile ngoma mbili ndefu, ambazo pia huitwa conga, kati ya waliokuwa maarufu kutokana na chombo hicho ni marehemu Siddy Morris, aliyejulikana pia kwa jina la ‘Tanzania One’, marehemu Haruna Lwali, mkongwe Ally Jamwaka ambaye bado yupo jukwaani katika bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Katika upande wa wapiga drums, alikuwepo marehemu Chipembele Said aliyejulikana kwa rafiki zake kama  ‘Bob Chipe’, marehemu Abuu Semhando ambaye aliwahi pia kuwa na jina la utani la ‘Lokasa’ na katika siku zake za mwisho alipenda kuitwa ‘Baba Diana’, marehemu Johnny Rocks aliyekuwa mpiga drum wa bendi ya The Sunburst.

Upande wa wapuliza tarumbeta, walikuweko, marehemu Kulwa Salum wa Morogoro Jazz band, Kanku Kelly, mkongwe wa bendi za OSS, Maquis du Zaire na Kilimanjaro Connection, marehemu Joseph Lusungu wa Msondo, marehemu Machaku Salum wa Mlimani Park.

Kati ya wapiga saksafon maarufu, walikuweko marehemu Ahmad Kipande wa Kilwa Jazz Band, marehemu  Mafumu Bilali Bombenga aliyejulikana pia kama Super Sax, Rashid Pembe wa Vijana Jazz Band, marehemu Joseph Bernard, marehemu Juma Town, Mnenge Ramadhani, Ally Rashid, marehemu Michael Enoch ambaye pia alisifika sana enzi zake alipokuwa mpiga gitaa la solo wa Dar es Salaam Jazz Band.

 Upande wa gitaa la bezi, alikuweko Selemani Mwanyiro ‘Computer’, Banza Mchafu wa Maquis na Mustafa Ngosha, aliyejulikana awali kwa jina la Charles Ngosha.

Kwenye gitaa la rhythm umaarufu ulikuwa wa Kassim Kaluwona, aliyejulikana pia kama Kassim Rhythm wakati akiwa Tabora Jazz Band,  Jamhuri Jazz Band ilikuwa na Harrison ‘Satchmo’ Siwale, Morogoro Jazz Band ikawa na  Charles Kasembe, wakati Urafiki Jazz Band ikawa na  Mohamed Bakari Churchil.

Gitaa la solo na second solo kulikuwa na wapigaji wengi waliopata umaarufu, mfano Mohamed Hanzuruni, Wema Abdallah, Kassim Mponda, Nguza Viking, Ndala Kasheba, Shem Karenga, Mbaraka Mwinshehe, Rizwan Pangamawe,  Shaaban Yohana Mwanasande (Shaaban Wanted), Kassim Rashid na wengine wengi.

Wako pia wanamuziki wengi waliokuwa maarufu kutokana na kupiga vinanda, Hassan Shaw, Waziri Ally, Abdul Salvador na wengine wengi.

Kama inavyoonekana hapo juu, kulikuwa na wanamuziki wengi maarufu ambao sauti zao hazikuwahi kusikika, lakini walikuwa wakithaminiwa na wapenzi wa muziki kutokana na upigaji wao wa ala.

Moja kati ya vitu vilivyowafanya magwiji hawa kuwa maarufu, kila mmoja alihakikisha ana staili yake ya upigaji, kitu ambacho kilifanya kila bendi kuwa tofauti na nyingine na mashabiki walipokuwa wakisifia bendi yao walikuwa na sababu za kimuziki kwa nini walipenda bendi fulani, upigaji wa Ndala Kasheba ukijumlisha na ubunifu wake wa kutumia gitaa la nyuzi 12 ulifanya awe tofauti na upigaji wa Hamza Kalala au Kassim Mponda, japo kila mmoja wao alikuwa bingwa.

Siku hizi si ajabu kabisa kuingia bendi nne au tano ukakuta upigaji wa gitaa la solo au drums au kinanda ni ule ule kama vile wote walifundishwa na mwalimu mmoja. Na hivyo sasa hata sifa zinakuwa kwa waimbaji tu kama ilivyo muziki wa kutengenezwa studio.