Unachomfikiria mwenza wako, ndicho anachokufikiria
Picha na Mtandao.
Wengi wa wanandoa, japo si wote, hujiona wao ni bora na sahihi kuliko wenzao. Hii si kweli na ni dhana potofu. Hakuna aliyemkamilifu wala sahihi.
Kujiona ni bora si ubora bali udhaifu usio na msingi. Wote tuna upungufu na ubora kadhalika. Na katika hili, hatuchekani wala kuzidiana bali tu binadamu. Hivyo, tunakosea kila siku. Na tutaendelea kukosea.
Kutokana na udhaifu na ukomo wa uelewa wa binadamu, maisha hasa ya ndoa ni darasa lisilo na mwisho. Mwenye kuwamo kwenye darasa hili, anapaswa kujua na kukubali kuwa ni mwanafunzi hadi atakapokufa.
Uzuri wa darasa hili, wote ni wanafunzi na pia ni walimu. Mnafundishana hata muwe mnatofautiana kiakili na kielimu kiasi gani. Hii ni kutokana na mambo kadhaa.
Mosi, kutotabirika kwa binadamu ambayo ni asili yake. Hii ni kutokana na uwezo mkubwa kiakili katika kuelewa na kushughulikia mambo.
Pili, kubadilika kwa binadamu. Binadamu anabadilika karibu kila sekunde.
Tatu, kutojua wala kuweza kila kitu. Bindamu wote wana ukomo wa uelewa. Wapo wanaoelewa mambo makubwa wakashindwa madogo na wanaoelewa mambo madogo wakashindwa makubwa.
Pamoja na umaarufu na kipaji kikubwa cha kuchora, mchoraji nguli, Leonardo da Vincci hakuwa na uwezo wa kutunza muda wala hakuoa maisha yake yote.
Tano, binadamu wote ni tegemezi. Hatuna uwezo wa kujitosheleza kwa kila kitu. Tunahitajiana iwe kwa kutaka au kulazimika. Jiulize swali dogo. Kuna binadamu anayejitosheleza? Jibu ni hakuna.
Wapo waliojaliwa akili vipaji na vipawa vikubwa tu. Bado wanahitaji wengine kuvifanikisha au kuvifaidi. Usishange profesa mzima kukumbushwa na mkewe kuwa soksi alizovaa ni chafu.
Tuone mfano
Usishangae daktari kukumbushwa kuwa amesahau kupeleka mtoto shule na vitu kama hivyo. Huu ni ushahidi wa kutegemeana na kutojitosheleza kama binadamu. Tutoe mfano wa mtoto wa rafiki yetu.
Huyu baba ni gwiji ya teknolojia ya mtandao. Ajabu, hawezi kuendesha gari. Wazazi wake walimlazimisha ajifunze kuendesha gari akakataa. Je, hapa tatizo ni nini?
Hivyo, unapomfikiria, kumhukumu, kumkosoa, hata kumtenza ndivyo siyo mwenzio, kumbuka. Naye ana uwezo wa kukuwazia na kukutenga hivyo hivyo.
Kimsingi, wanandoa ni sehemu mkabala ya wenzao. Tunajiona kupitia kwa wenzetu kama ambavyo nao, wanajiona kupitia kwetu.
Hivyo, kabla hujamhukumu, au kumuwazia lolote mwenza wako, jikumbushe. Unaweza kumsukuma naye kufanya hivyo hivyo hata kama hakuwa amepanga. Na hili haliepukiki.
Ni kwa sababu hakuna awezaye kutawala mawazo ya mwenzake achilia mbali kuyajua. Unachompa au kumnyima ndicho hicho hicho anachokupa au kukunyima.
Kimsingi, maisha ya ndoa ni sawa na barabara. Lazima iwe na njia mbili ili kuwezesha usafiri kufanyika. Au tuiweke hivi. Ni kama mikono miwili. Lazima inawishane.
Kitu kingine ambacho hakiepukiki ni kwamba, huwezi kumuepuka mwenzako kama ambavyo naye hawezi kukuepuka. Mnategemeana.
Ndiyo maana mlitafutana na kukubaliana kuishi pamoja na kuchangia maisha yenu. Ogopa mtu ambaye yuko karibu nawe muda mwingi kuliko yeyote awe mtoto au wazazi wako.
Sisi, kama wanandoa wakongwe, tunayo falsafa moja kuu. Mwenzako ni kama nyuki. Ukimkandamiza, anaweza kukung’ata na kukuumiza. Ukimruhusu atue kiganjani na kutomsumbua, atakulipa hivyo hivyo japo si wote. Ukimtenza nyuki, atakuachia asali.
Ukimtenza vibaya, atakung’ata na kukuachia maumivu hata msiba. Yote hutegemea namna mnavyoishi na sababu za kuwa kitu kimoja. Hii ni tofauti na wale wasaka ngawila waingao kwenye ndoa kuchuma na kuondoka.
Kwa mwenza wa kweli, utakachomfanyia au utakavyomtenza, tegemea malipo yale yale hata wakati mwingine zaidi. Kuna kitu kwa kimombo kinaitwa the rule of reciprocity, yaani kanuni ya kulipizana.
Ni kama shamba. Upandacho ndicho uvunacho japo wengine wanaweza wasivune chochote kama hawatafuata kanuni za upanzi.
Huwezi kuwa unamsonya, kumsimanga, kumnyanyasa hata kumpiga mwenzako ukategemea upate kicheko na upendo. Kanuni iko wapi. Lazima ulipie ulichopewa.
Ukitoa maumivu, tegemea maumivu. Kila unachotoa ni kama mwangwi. Lazima kikurudie. Kimsingi, kila umtendeacho au kumpa mwenzio, unajitendea mwenyewe.
Mwisho, kitu kikubwa ambacho wengi husahau nasi hupenda kukikumbushia, ni ukweli kuwa tunaishi mara moja. Hivyo, unapofanya makosa yasiyo na sababu, jua. Unazidi kuharibu bahati ambayo hutaipata tena. Hivyo, mnapoishi, tendeni wema kana kwamba mtaishi milele.