Ni kipindi cha kuweka kando nywele bandia

Katika maeneo mengi nchini kwa sasa kilio ni joto, mgawo wa umeme na uhaba wa maji. Kulingana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) mikoa 14 imekuwa na ongezeko la joto, ikiongozwa na mkoa wa Kilimanjaro ambako imefikia nyuzi joto 35.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa hali ya hewa, Rose Senyengwa hali hii inaweza kuendelea hadi Machi, kwa kuwa ni kipindi ambacho jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia na Tanzania ni nchi mojawapo ambayo ina hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine.

Ufafanuzi huu wa mtaalamu unatufanya tujiweke katika nafasi ya kuangalia namna ya kuishi katika kipindi hiki tukiendana na hali ya hewa iliyopo bila kusahau changamoto nyingine za uhaba wa maji na mgawo wa umeme.

Changamoto hizi kwa namna moja au nyingine zinaweza kuathiri mfumo wa maisha ya watu, hasa wa mijini ambao huenda ili kupata riziki ya kila siku ni lazima watoke eneo moja kwenda lingine.

Suala la kutoka kwa hakika linahusisha muonekano, kwa wanaojipenda na kujijali, muonekano ni kipaumbele chao na changamoto zilizopo nchini kwa sasa kwa kiasi fulani zinaweza kuathiri hilo.

Hapo ndipo jarida la Familia katika makala haya ya mitindo inakuleta mbinu mbalimbali za kuishi katika kipindi hiki bila kuathiri mwonekano wako.

Pamoja na dondoo hizo, mitindo na urembo ni muhimu pia kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuhakikisha tunaendelea kuwa na afya njema, licha ya hali mbaya ya hewa inayoendelea kusumbua katika maeneo mengi nchini.

Kwenye upande huu wa mitindo na urembo, hiki ni kipindi cha kuwa makini mno na ngozi kwa kuwa upo uwezekano mkubwa wa ngozi kuathiriwa na joto, hasa kupata vipele na kutokwa na jasho jingi.

Hali hii inatukumbusha tusifikirie kuvaa nguo nzito katika kipindi hiki na mavazi yenye rangi nyeusi si rafiki, hasa kama unatembea au kufanya shughuli zako kwenye jua. Kwa asili rangi nyeusi huhifadhi joto hivyo unaweza kujikuta katika mazingira magumu.

Si mavazi tu, kipindi hiki inashauriwa kuepuka vipodozi vikali kwa kuwa vinaweza kuleta matokeo hasi kwenye ngozi na kumpa mtu mwonekano usiofaa.
Ni kipindi cha kuepuka kupaka mafuta yaliyoganda ambayo yanaweza kuyeyushwa na jua na kutiririka kutoka kichwani.

Mtaalamu wa masuala ya urembo, Dina Charles anasema katika kipindi hiki ni vyema watu wakapunguza matumizi ya vipodozi, hasa ‘makeup’ kwa kuwa joto linaweza kuwafanya wapate mwonekano usiopendeza usoni.

“Makeup inatakiwa kumfanya mtu apendeze, lakini kama utatumia isiyokuwa na ubora ukichanganya na hali hii ya joto ni vigumu kupata matokeo mazuri na pia inaweza isidumu kwa muda mrefu. Ushauri wangu mtu kama unaweza kubaki na ngozi yako ya asili ni heri ukafanya hivyo katika kipindi hiki,” anasema Dina.

Mbali na hilo, eneo lingine linaloshauriwa kuangaliwa kwa umakini ni mitindo ya nywele, hasa ile inayohusisha nywele za bandia, ikiwemo mawigi, weaving na rasta ambazo husukwa kwa kuunganishwa na nywele za mtu.

Dina anasema, “Kiukweli kama huna kikwazo chochote basi hiki ni kipindi cha kuwa na muonekano wako wa asili, kama unasuka hebu suka nywele zako bila kuunganisha na nywele bandia, hii itakuepushia adha za joto, ikiwemo kichwa kuwasha kutokana na ngozi kulowa jasho.

“Wale wenye nywele fupi ni wakati wao wa kujidai, hakuna sababu ya kuhangaika na mawigi au weaving. Hali ya hewa inataka kichwa kipumue.
Kama una asili ya jasho, usitumie manukato kukata harufu hiyo, viwili hivi vikichanganyika inaweza kuleta harufu kali zaidi.

Kuzuia hili hakikisha unatumia deodorant kukausha jasho makwapani kabla ya kupulizia manukato kiasi”.

Mtaalamu wa afya, Festo Ngadaya anasema katika kipindi hiki ni muhimu kunywa maji ya kutosha kulingana na mahitaji ya mwili.

Anashauri pia ni muhimu kuoga maji ya baridi kushusha joto la mwili na kuepuka kulala bila kuusafisha mwili na kunawa mikono mara kwa mara kuepusha magonjwa.

Suala lingine ni kutorudia nguo za ndani kutokana na kwamba wadudu wa magonjwa huzaliana kwenye joto, hivyo kukaa na nguo chafu ni kujitengenezea magonjwa mwilini.

“Tuangalie nguo wanazovaa watoto wachanga tusiwafunike sana tuwaache wapate hewa ya kutosha.Hata watu wazima epuka nguo nyeusi, nzito, suti, tai, acha kuvaa nguo nzito,” anasema