Mbinu kukabili msongo wa mawazo kwenye familia
Muktasari:
- Wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa msongo wa mawazo unapodumu kwa muda mrefu unaweza kuathiri afya ya mwili na akili, uhusiano wa kifamilia na hata maendeleo ya watoto.
Dar es Salaam. Katika maisha ya sasa yenye changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii na kiafya, familia nyingi zinakabiliwa na msongo wa mawazo bila hata kutambua.
Gharama za maisha zinazoongezeka, majukumu ya kulea watoto, migogoro ya kifamilia, magonjwa na hata ukosefu wa muda wa kuwa pamoja vinaweza kusababisha hali ya mfadhaiko na msongo wa mawazo kwa wanafamilia.
Wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa msongo wa mawazo unapodumu kwa muda mrefu unaweza kuathiri afya ya mwili na akili, uhusiano wa kifamilia na hata maendeleo ya watoto.
Msongo wa mawazo unaweza kuathiri afya ya akili na mwili kwa njia mbalimbali kutokana na mwili kuendelea kuzalisha homoni za mfadhaiko kama cortisol na adrenaline kwa kiwango kikubwa.
Mfano unaweza kuwa na wasiwasi wa kupindukia na hofu za mara kwa mara, kukosa usingizi au kupata usingizi usio wa kutosha, kushindwa kuzingatia kazi au masomo, kukosa hamasa ya kufanya shughuli za kawaida, kuwa na hasira za haraka, kuwa na huzuni ya muda mrefu ambayo inaweza kusababisha unyogovu (depression).
Kwa upande wa afya ya mwili, msongo wa mawazo unaweza kuchangia maumivu ya kichwa ya mara kwa mara, kuongezeka kwa shinikizo la damu, magonjwa ya moyo kutokana na presha ya muda mrefu, uchovu usioisha hata baada ya kupumzika, matatizo ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula kama vidonda vya tumbo, gesi au kuharisha.
Dalili za msongo wa mawazo
Hatua ya kwanza ni kutambua dalili zinazoweza kuashiria kuwa mmoja au zaidi ya wanafamilia wanapitia msongo wa mawazo. Dalili hizo zinaweza kujumuisha hasira za mara kwa mara, kukosa usingizi, uchovu usioelezeka, kukosa hamu ya kula au kula kupita kiasi, kujitenga na wengine, pamoja na kupoteza hamasa ya kufanya shughuli za kawaida.
Kwa watoto, dalili zinaweza kujitokeza kupitia mabadiliko ya tabia, kushuka kwa ufaulu shuleni, kulia mara kwa mara au kuwa wakorofi kupita kiasi.
Mawasiliano mazuri ni nguzo muhimu katika familia yenye afya. Wazazi na watoto wanapaswa kupewa nafasi ya kueleza hisia, changamoto na mawazo yao bila kuhukumiwa.
Mazungumzo ya mara kwa mara husaidia kutambua matatizo mapema na kutoa fursa ya kutafuta suluhisho kwa pamoja. Wataalamu wanashauri familia kutenga muda wa kukaa pamoja kila siku au angalau mara kadhaa kwa wiki ili kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu.
Wakati mwingine msongo wa mawazo hutokana na mzigo mkubwa wa majukumu kubebwa na mtu mmoja pekee. Kugawana kazi za nyumbani na majukumu ya malezi husaidia kupunguza uchovu na kuongeza ushirikiano.
Watoto wanaweza kupewa kazi ndogo zinazolingana na umri wao, huku wazazi wakisaidiana katika shughuli za kila siku. Hali hii hujenga mshikamano na kupunguza hisia za kubanwa na majukumu.
Tenga muda wa kupumzika na kufurahi pamoja. Familia nyingi hujikuta zikitumia muda mwingi katika kazi na masomo huku zikisahau umuhimu wa burudani.
Kutenga muda wa kufanya shughuli za pamoja kama kutembea, michezo, kusoma vitabu, kuangalia filamu au kula pamoja kunaweza kusaidia kupunguza msongo wa mawazo.
Shughuli hizi huimarisha uhusiano wa kifamilia na kuwapa wanafamilia nafasi ya kufurahia uwepo wa kila mmoja.
Pia, zingatia mtindo bora wa maisha; Afya ya akili ina uhusiano mkubwa na afya ya mwili. Kula lishe bora, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara na kupata usingizi wa kutosha husaidia mwili na akili kukabiliana na changamoto za kila siku.
Mazoezi huchochea mwili kutoa homoni zinazosaidia kuboresha hali ya moyo na kupunguza hisia za wasiwasi. Hata matembezi mafupi ya familia yanaweza kuwa na manufaa makubwa.
Aidha, epuka kutatua migogoro kwa hasira; Migogoro ni sehemu ya maisha ya familia, lakini namna inavyoshughulikiwa ndiyo huleta tofauti. Kutumia lugha ya ukali, matusi au vitisho huongeza msongo wa mawazo na kuharibu mahusiano.
Badala yake, wanafamilia wanapaswa kujifunza kusikilizana, kuheshimiana na kutafuta suluhisho kwa mazungumzo ya utulivu. Watoto wanaokulia katika mazingira ya amani huwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na afya nzuri ya akili.
Hata hivyo, kama msongo wa mawazo unaendelea kwa muda mrefu na kuathiri maisha ya kawaida ya familia, ni muhimu kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ya akili. Ushauri wa kisaikolojia unaweza kusaidia kutambua chanzo cha tatizo na kutoa mbinu sahihi za kukabiliana nalo.
Kutafuta msaada si ishara ya udhaifu, bali ni hatua muhimu ya kulinda afya na ustawi wa familia.
Msongo wa mawazo unaweza kuathiri familia yoyote, lakini kwa mawasiliano mazuri, ushirikiano, mtindo bora wa maisha na utayari wa kutafuta msaada inapohitajika, athari zake zinaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Familia yenye afya ya akili hujenga mazingira salama, yenye upendo na yanayowawezesha wanafamilia wote kustawi na kufikia malengo yao.