Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hatari mwenza kupenda bila mipaka

Muktasari:

  • Upendo wa kweli hauui, hauharibu wala haulazimishi. Upendo wa kweli hujenga, huacha nafasi ya utu binafsi, na hukubali kuwa maisha yanaweza kuendelea hata baada ya mapenzi kuisha.

Dar es Salaam. Mapenzi yamekuwa yakisifiwa kama chanzo cha furaha, faraja na maana ya maisha. Nyimbo, filamu na hadithi nyingi zimejengwa juu ya wazo la kumpenda mtu kwa moyo wote bila kipimo. 

Hata hivyo, nyuma ya simulizi hizi nzuri kuna ukweli mchungu unaojitokeza kila siku katika jamii. Mapenzi yanapokosa mipaka na maandalizi ya kiakili, hugeuka chanzo cha migogoro mikubwa, vurugu, mauaji ya kimapenzi na hata kujiua. 

Kumekuwa na ongezeko la visa vya watu kuumizana au kujiua kufuatia kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi. Wengi wao walikuwa wamewekeza kila kitu katika uhusiano mmoja.

Furaha yao, heshima yao na sababu ya kuishi ilikuwa mtu mwingine. Mapenzi yalipoyumba, maisha yao yote yaliporomoka. Hali hii inaonesha wazi kuwa tatizo si kupenda, bali ni kupenda bila mipaka na bila uelewa kuwa mapenzi ni uamuzi unaobeba hatari zake.

Mtaalamu wa uhusiano na mwanasaikolojia, Esther Perel anasema kuwa binadamu wa kisasa anatarajia kupokea kila kitu kutoka kwa mpenzi mmoja, kitu ambacho hapo zamani kilikuwa kikitolewa na jamii nzima. Anaeleza kuwa pale mtu anapomfanya mpenzi wake kuwa kila kitu katika maisha yake, anaunda mzigo mkubwa usiobebeka. 

Hapo ndipo mapenzi yanapogeuka kuwa utegemezi wa kihisia badala ya ushirika wa hiari.

Mapenzi yasiyo na mipaka humfanya mtu kupoteza uwezo wa kujitambua. Anaanza kuishi kupitia macho ya mpenzi wake, kuamua kwa niaba ya hisia za mwingine na kupima thamani yake kwa kiwango cha mapenzi anachopewa. Katika mazingira haya, wivu huongezeka, hofu ya kuachwa hutawala, na migogoro midogo hugeuka vita vikubwa. Pale uhusiano unapovunjika, mtu hujihisi kama amepoteza kila kitu.

Hali hii imechangia matukio mengi ya mauaji ya wapenzi, hasa pale mtu mmoja anapohisi kuwa hawezi kuishi bila mwenzake au hawezi kumwona mwenzake akiendelea na maisha bila yeye.

 Kukosa mipaka kunamfanya mtu aamue kuwa bora afe au aue kuliko kukubali kuachwa. Huu ni ushahidi wa wazi kuwa mapenzi yasiyo na mipaka ni hatari kwa maisha ya binadamu.


Usizame bila maandalizi

Kinyume na dhana maarufu kuwa mapenzi ni hisia zisizodhibitika, wataalamu wengi wa kisasa wanasisitiza kuwa mapenzi ni uamuzi unaofanywa kwa hiari na unaohitaji uwajibikaji. 

Jay Shetty anaeleza kuwa hisia za kuvutiwa zinaweza kujitokeza bila mpango, lakini kuamua kubaki na mtu, kuwekeza na kujitoa ni uamuzi unaopaswa kufanywa kwa akili timamu.

Kuzama sana katika mapenzi bila kujiandaa ni kosa linalofanywa na watu wengi. Wanaingia kwenye uhusiano wakiwa na matumaini makubwa lakini bila kujiuliza maswali muhimu kuhusu uwezo wao wa kukabiliana na mabadiliko. 

Hawajiandai kwa uwezekano wa mapenzi kupungua, migogoro kutokea au hata uhusiano kuvunjika. Matokeo yake ni mshtuko mkubwa wa kihisia pale hali inapobadilika.

Mwandishi Alain de Botton, anaeleza kuwa tatizo kubwa katika mapenzi si maumivu yanayotokea, bali ni matarajio yasiyo halisia tunayojenga. 

Anasema watu wengi hupenda wakiamini kuwa watapendwa milele kwa namna ile ile, bila mabadiliko. Wanapokutana na uhalisia wa kibinadamu, ambapo hisia hubadilika na watu hukosea, wanashindwa kuhimili.

Kujiandaa katika mapenzi kunahitaji mtu ajitambue kwanza. Ajue thamani yake haitegemei kupendwa na mtu mwingine. Ajue kuwa anaweza kupoteza uhusiano bila kupoteza maisha. Hii ndiyo maana halisi ya kuweka mpaka wa moyo katika kupenda.


Kusalitiwa, mapenzi kuchuja 

Hakuna uhusiano ulio salama kabisa dhidi ya changamoto. Kusalitiwa, kupungua kwa hisia au kuachana ni sehemu ya hali halisi ya mapenzi. 

Tatizo kubwa ni kwamba watu wengi hawajiandai kukabiliana na hali hizi. Wanapokutana nazo, huingia katika msongo mkubwa wa mawazo, hasira kali au huzuni isiyodhibitiwa.

Mtaalamu wa saikolojia ya uhusiano, Alexandra Solomon anaeleza kuwa maumivu makubwa ya kimapenzi hutokana zaidi na tafsiri tunazotoa kuliko tukio lenyewe. 

Mtu anapojisemea kuwa kusalitiwa kunamaanisha yeye si wa thamani, maumivu huongezeka maradufu. Kama angekuwa amejiandaa kisaikolojia, angeona tukio hilo kama kosa la binadamu mwingine, si hukumu juu ya utu wake.

Mapenzi yanapochuja, watu wengi hujihisi wameshindwa au wameachwa bila thamani. Hali hii husababisha baadhi yao kufanya uamuzi wa haraka na wenye madhara makubwa. 

Vienna Pharaon anaeleza kuwa uhusiano mzuri hauji kujaza mapengo ya utu wa mtu, bali hukutana na mtu aliyejitosheleza kihisia. Mtu ambaye hajajiandaa kihisia huweka mzigo mkubwa kwa mpenzi wake, na pale mzigo huo unaposhindwa kubebwa, maumivu huwa makubwa.

Kuweka mipaka katika mapenzi humsaidia mtu kukubali kuwa hata kama uhusiano umeisha, maisha yanaendelea. Humsaidia kuona kuwa maumivu ni sehemu ya safari, si mwisho wa safari. Huu ndiyo uelewa unaopunguza hatari ya migogoro mikubwa na uamuzi wa kujiumiza.

Mapenzi ni uamuzi unaohitaji maandalizi, uelewa na ujasiri wa kukubali uhalisia wa maisha. Mtu anayependa kwa mipaka hujua kuwa anaweza kuumizwa bila kuangamia, anaweza kuachwa bila kupotea, na anaweza kupenda bila kujisahau.

Katika dunia ambayo mapenzi yamekuwa chanzo cha migogoro mikubwa na hata vifo, ni muhimu kujifunza kupenda kwa akili pamoja na moyo. 

Upendo wa kweli hauui, hauharibu wala haulazimishi. Upendo wa kweli hujenga, huacha nafasi ya utu binafsi, na hukubali kuwa maisha yanaweza kuendelea hata baada ya mapenzi kuisha. Makala haya kwa hisani ya mitandao mbalimbali