Wanafunzi masomo ya ujuzi washindanishwa utatuzi changamoto kwa teknolojia
Baadhi ya washiriki wa Mashindano ya Ujuzi Kitaifa kutoka vyuo mbalimbali nchini wakionesha umahiri wao katika maeneo ya uhandisi mitambo na usanifu wa kihandisi wakati wa mashindano hayo yanayoendelea jijini Arusha.
Muktasari:
- Washindi ngazi ya kanda watapata fursa ya kushiriki ngazi ya Taifa Mwezi Agosti, 2026, ambapo washindi watapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Ujuzi ya Afrika.
Dar es Salaam. Wanafunzi wameshindanishwa kuonesha umahiri katika Uhandisi Mitambo na Usanifu wa Kihandisi kwa kutumia kompyuta.
Mashindano ya Ujuzi Kitaifa 2026 yanaendelea kufanyika nchini, ambapo wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali wameshiriki mchujo katika eneo la Uhandisi Mitambo na Usanifu wa Kihandisi kwa kutumia Kompyuta ngazi ya Kanda uliofanyika katika chuo Ufundi Arusha (ATC), mkoani Arusha.
Washiriki walichuana umahiri wao katika kubuni, kuchambua na kutatua changamoto za kiufundi kwa kutumia teknolojia za kisasa za usanifu wa kompyuta.
Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi, yalianza tarehe 8 Juni 2026 na yanalenga kuhamasisha maendeleo ya ujuzi miongoni mwa vijana kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Lengo ni kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira n akucnagia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Washindi ngazi ya kanda watapata fursa ya kushiriki ngazi ya Taifa Mwezi Agosti, 2026, ambapo washindi watapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Ujuzi ya Afrika.
Mashindano haya yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na ni ya kwanza kufanyika tangu Tanzania ijiunge na uanachama wa Worldskills Africa, hatua inayofungua fursa zaidi kwa vijana wa Kitanzania kushiriki na kushindana katika majukwaa ya kimataifa ya maendeleo ya ujuzi.