Wenye kisukari wasiache vyakula hivi
Muktasari:
- Kwa watu wenye kisukari, vyakula hivi ni msaada mkubwa katika kudhibiti viwango vya sukari na kupanda na kushuka kwa sukari ghafla.
Dar es Salaam. Watu wenye kisukari mara nyingi wanadhani kudhibiti sukari ni kuacha kabisa kula vyakula vya wanga.
Hata hivyo, wasichojua ni kuwa kuna vyakula vya wanga vyenye kiasi kidogo sana cha sukari au low Glycemic Index, ambavyo vinaweza kuliwa bila hofu, bado husaidia kudhibiti viwango vya sukari
Vyakula kama mtama, ulezi, uji wa hafrahafi (oats), mchele wa kahawia, unga wa mahindi na ngano isiyokobolewa, ni vyanzo bora vya nishati vinavyofyonzwa taratibu vikiwa tumboni kwa sababu vina nyuzinyuzi nyingi, hivyo kumsaidia mtu kushiba muda mrefu na kuepuka ulaji wa mara kwa mara.
Kwa watu wenye kisukari, vyakula hivi ni msaada mkubwa katika kudhibiti viwango vya sukari na kupanda na kushuka kwa sukari ghafla. Kwa wale wasiokuwa na kisukari, vyakula hivi husaidia kudhibiti uzito na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa huo.
Mboga nyingi za majani zina kiasi kidogo sana cha Glycemic Index, ikiwemo mchicha, kabeji, broccoli, bilinganya na matango.
Mboga hizi hazina sukari ya kuweza kupandisha viwango vya sukari, zina vitamini na madini mengi, na ni muhimu katika kuimarisha kinga ya mwili.
Kwa wenye kisukari, mboga husaidia kuweka uwiano wa sukari na kuboresha mmeng’enyo. Kwa watu wasio na kisukari, ulaji wa mboga mara kwa mara hupunguza hatari ya kupata unene kupita kiasi na magonjwa ya moyo.
Mbegu za karanga, almonds, walnuts, mbegu za chia na mbegu za maboga zina Glycemic Index ndogo sana na zina mafuta mazuri yanaweza kuimarisha afya ya moyo. Zinasaidia kupunguza njaa na kuboresha viwango vya sukari.
Vyakula vyenye kiasi kidogo cha sukari au Glycemic Index ni muhimu kwa wenye kisukari kwa sababu husaidia kudhibiti sukari muda wote kwa kuepuka ongezeko la ghafla, hupunguza hatari ya madhara ya muda mrefu kama shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na uharibifu wa neva, husaidia kupunguza uzito, jambo muhimu katika udhibiti wa kisukari.
Hata watu wasio na kisukari wananufaika na vyakula hivi kwa sababu huzuia hatari ya kupata kisukari aina ya pili, husaidia kupunguza na kudhibiti uzito, huimarisha mfumo wa mmeng’enyo kutokana na nyuzinyuzi, hulinda moyo kwa kupunguza mafuta mabaya, huongeza kinga ya mwili
Vyakula vyenye kiasi kidogo cha glycemic index ni nguzo muhimu ya afya njema kwa watu wote. Kwa wenye kisukari, vyakula hivi ni msaada wa moja kwa moja katika kudhibiti viwango vya sukari na magonjwa mengine.
Watu wenye uzito mkubwa au wasiokuwa na kisukari, vyakula hivi husaidia kupunguza hatari ya magonjwa sugu na kuimarisha mwili kwa ujumla. Kila mtu anaweza kunufaika kwa kuongeza vyakula hivi kwenye lishe ya kila siku.