Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali, wadau wa afya wasisitiza kuongeza juhudi kutokomeza malaria

Mkurugenzi wa Idara ya afya ya uzazi mama na mtoto kutoka wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani akizungumza kwenye jukwaa la Malaria lililoandaliwa na Ifakara Health Institute (IHI) Jijini Dodoma leo April 23, 2026

Muktasari:

  • Serikali na wadau wa sekta ya afya wamesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji, ubunifu na ushirikiano katika kuharakisha mapambano dhidi ya malaria, huku changamoto za usugu wa dawa na upatikanaji wa huduma zikiendelea kujitokeza.

Dodoma. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya nchini imesema Tanzania ipo katika hatua muhimu ya kuelekea kutokomeza malaria, ikisisitiza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado juhudi zaidi zinahitajika ili kufikia lengo hilo kwa haraka na ufanisi.

Akizungumza katika Jukwaa la Malaria la Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) lililofanyika leo, Alhamisi, Aprili 23, 2026, jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk Ahmed Makuwani amesema uwepo wa zana mpya unatoa fursa kubwa ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Ametaja zana hizo kuwa ni pamoja na vyandarua vilivyoboreshwa vyenye dawa, chanjo za malaria, mbinu bunifu za kudhibiti mbu, pamoja na tafiti zinazoongozwa na wataalamu wa Afrika.

Hata hivyo, Dk Makuwani ameonya kuwa mafanikio hayo yanaweza kudhoofika iwapo uwekezaji utapungua au dhamira ya kisiasa italegalega.

“Historia inaonesha kuwa mafanikio yanaweza kurudi nyuma pale uwekezaji unapopungua, afua zinapodhoofika au umakini wa kisiasa unapopungua,” amesema.

Baadhi ya washiriki wa jukwaa la malaria lililoandaliwa na Ifakara Health Institute (IHI) Jijini Dodoma leo Aprili 23, 2026

Ameongeza kuwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 70, Taasisi ya Afya ya Ifakara imekuwa na mchango mkubwa katika tafiti za malaria, ikiwemo tafiti za ikolojia ya mbu, ubunifu wa mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo, pamoja na maendeleo ya chanjo na dawa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa IHI, Dk Nicodemus Govella amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, malaria bado ni changamoto kubwa kwa afya ya umma na maendeleo ya nchi.

Amebainisha changamoto zinazoendelea kuwa ni pamoja na maambukizi yaliyosalia katika baadhi ya maeneo, mzigo mkubwa wa ugonjwa katika maeneo mengine, kuongezeka kwa usugu wa viuatilifu na dawa, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, amesema kuna fursa mpya zinazotokana na maendeleo ya teknolojia na tafiti bunifu zinazoweza kuharakisha juhudi za kutokomeza malaria.

“Swali si kama malaria inaweza kutokomezwa, bali ni kwa kasi na ufanisi gani tunaweza kufikia lengo hilo,” amesema.

Baadhi ya washiriki wa jukwaa la malaria lililoandaliwa na Ifakara Health Institute (IHI) Jijini Dodoma leo Aprili 23, 2026

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maeneo manne muhimu, ambayo ni kuharakisha ubunifu, kuimarisha mifumo ya afya, kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa huduma na kudumisha dhamira ya kisiasa.

Naye, Dk Magreth Sawe kutoka Hospitali ya Mvumi Mission amesema kutokomeza malaria kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, watafiti, washirika wa maendeleo na jamii kwa ujumla.

“Tunayo maarifa, tunazo zana na tunayo ushirikiano. Kinachohitajika sasa ni dhamira mpya na hatua za pamoja,” amesema.

Ameongeza kuwa jukwaa hilo linatarajiwa kutoa mapendekezo ya vitendo yatakayosaidia kuongoza sera na kuimarisha juhudi za kutokomeza malaria nchini.