Pombe, sigara chanzo watoto kukosa ubongo, mimba kuharibika

Muktasari:
- Watoto kuzaliwa wakiwa na hawana ubongo ‘alcoholic syndrome’, tundu kwenye moyo na mimba kuharibika hujitokeza mimba ikiwa chini ya miezi mitano hali ambayo huleta madhara kwa mama na mtoto aliye tumboni.
Mbeya. Wajawazito wanaotumia vilevi na sigara kupita kiasi, wako hatarini kupata watoto wasio na ubongo ‘alcoholic syndrome’ tatizo linalosababisha ubongo wa mtoto kutofanya kazi, kutokomaa maumbile na tundu kwenye moyo.
Madhara mengine ni kujifungua watoto wenye changamoto mbalimbali wakiwepo njiti, kuzaliwa na changamoto ya vichwa vikubwa, mgongo wazi hususani kwa mjamzito mimba kuharibika ikiwa chini ya wiki 28 sawa na miezi saba.
Daktari Bingwa wa masuala ya wanawake katika Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dk George Lweyemamu ameliambia Mwananchi Digital leo Jumatano, Aprili 9, 2025, alipohojiwa kuhusiana na sababu za watoto kuzaliwa wakiwa na changamoto hizo.
"Kama mjamzito anapenda kutumia vilevi miezi mitatu ya mwanzo, yuko kwenye hatari ya kupata mtoto asiye na ubongo kwa maana anao ila haufanyi kazi yoyote, upungufu wa damu, mimba kuharibika na kusababisha dawa kushindwa kufanya kazi kutokana na mvutano wa kemikali za pombe mwilini, amesema Dk Lweyemamu.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na kinamama kutoka Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge.
“Tunaita mtoto ambaye hana ubongo kitaalamu ‘alcoholic syndrome’ kama ni mnywaji wa pombe anazaa mtoto mwenye shida. Ubongo ni moja ya ogani muhimu katika mwili wa binadamu, tatizo hili mtoto anazaliwa kama mtu mwenye kiharusi, kunakuwa hakuna mawasiliano sababu ubongo haifanyi kazi, atashindwa kukua vizuri, kutembea au kuongea,” amesema Dk Mkeyenge.
Dk Mkeyenge amesema tatizo hilo lina hatua wapo wanaoathirika kwa kiasi kidogo pia.
Dk Lweyemamu ametaja madhara mengine ni kupasuka kwa chupa kabla ya muda wa kujifungua na kupata maambukizi ya bakteria kwenye viungo vya uzazi na kuzaa watoto wa ajabu.
Dk Lweyemamu amesema licha ya Tanzania takwimu za matumizi ya vilevi na sigara kwa wajawazito kutokuwa juu, hivyo tunashauri kama kuna ulazima wa kunywa siyo kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito, bali kuanzia miezi mitano na kuendelea.
"Kuna tatizo haswa kwa mabinti wanaiga mikumbo na kujiingiza kwenye matumizi ya sigara na pombe pasipo kujua wana ujauzito, hali ambayo huleta athari kwa kiumbe kilichopo tumboni baada ya kujigundua," amesema.
Amesema hali hiyo husababisha baadhi yao kujikuta wamepata magonjwa ya kuambukizwa hususani maambukizi mapya ya VVU kutokana na ubebaji holela wa mimba zisizo tarajiwa.
Nini kifanyike
Dk Lweyemamu ametaka wajawazito kubadili mifumo ya maisha pale wanapo kuwa kwenye mipango na wenza wao kutafuta mtoto kwa kujiweka mbali na matumizi ya sigara na vilevi ili kuwa salama na mtoto anayezaliwa.
"Nitoe ushauri kwa wanaume na wenza wao kama ni watumiaji wa vilevi wanapo hitaji kupata familia wakae chini wajadiliane ili kupata watoto wenye afya bora hususani wanawake kuwa na kasumba ya kupima afya mara kwa mara ili kukwepa mimba zisizo tarajiwa," amesema.
Mbali na wajawazito Dk Lweyemamu, ameshauri jamii kubadili mifumo ya maisha na kutoweka matumizi ya pombe kama sehemu ya kupoteza mawazo ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
"Tunaona mifumo ya sasa ya maisha kwa jamii kwani idadi kubwa wanabainika kupata matatizo ya figo na ini chanzo ni matumizi makubwa ya pombe na kujikuta wakiingia gharama kubwa za matibabu," amesema.
Kauli za wajawazito
Mjamzito, Ndimyake Fredy amesema kutokana na ukubwa wa tatizo kuna haja wataalamu wa afya kurejea kutoa elimu kwa jamii ya madhara ya pombe na sigara ambayo yamekuwa makubwa kwa kundi hilo.
"Kwa sasa ni kama fasheni kwa mabinti walio na ujauzito kuwa wafuasi wakubwa wa sigara na pombe kwa kisingizio mtoto tumboni anapenda pasipo kujua athari kiafya," amesema.
Mjamzito ambaye hakutaka jina lake kuandikwa, amesema binafsi ni mfuasi mkubwa na kwamba mifumo ya maisha na mimba zisizotarajiwa na changamoto kwao.
"Unajua kwa mfano mimi hii mimba ya pili wanaume wamenikataa sina maisha, naona njia pekee ni kwenda vilabu vya pombe za kienyeji kupoteza muda na marafiki wa karibu waliopo wanatumia viburudisho hivyo," amesema.
Kuhusu madhara, amekiri kujua na kuomba Serikali kuwa na mpango mkakati kutoa elimu kupitia wataalamu wa afya ngazi ya jamii ili kunusuru kundi kubwa la vijana ambao ni taifa la kesho.