Mtaalamu: Ukipiga mswaki usisukutue na maji

Muktasari:
- Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa maonyesho ya kimataifa ya matibabu ya kinywa na meno Mei 30 na 31 mwaka huu, wakati takwimu zikionyesha kuwa asilimia 76.5 ya watu walio na umri wa miaka 15 na kuendelea wana tatizo la kuoza kwa meno, huku asilimia 33.1 ya watoto wakiwa na tatizo hilo.
Dar es Salaam. Ili kulinda afya ya kinywa na meno wataalamu wa afya wanasema mtu hatakiwi kusukutua na maji baada ya kupiga mswaki na kutema povu la dawa, kwani kufanya hivyo unapungiza ulinzi.
Pia, mtu anatakiwa kupiga mswaki baada ya kunywa chai asubuhi na si kabla ya kunywa cha na jioni kabla ya kulala.
Hayo yamesemwa na wataalamu walipozungumza na vyombo vya habari leo Aprili 2, 2025 wakati wakitangaza maonyesho ya kimataifa ya matibabu ya kinywa na meno yanayotarajiwa kufanyika Mei 30 na 31 mwaka huu jijini hapa.
Maonyesho hayo yatakutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo nchi wazalishaji wa bidhaa za matibabu ya meno.
Akizungumza leo Mkurugenzi Msaidizi huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo amesema kutosukutua na maji baada ya kupiga mswaki kunaiwezesha dawa kufanya kazi yake ipasavyo.
“Ndiyo maana tunasema upige mswaki walau mara mbili kwa siku, asubuhi baada ya kunywa chai na usiku kabla ya kwenda kulala. Tunasema baada ya kunywa chai kwa sababu tunaamini kuwa ulilala na kinywa kisafi,” amesema Dk Nzobo.
Amesema ili kulinda meno, mtoto anapaswa kutumia dawa ya meno ambayo madini yake ya floride ni ‘1000 ppm’ na watu wazima kiwango cha floride ni ‘1450 hadi 1500 PPM’ na baada ya kupiga mswaki mtu atatakiwa kutema povu peke yake na atakuwa amemaliza.
“Ukitema povu usisukutue na maji ili floride iweze kuzunguka ndani ya kinywa chako kwa saa 12 ili kutoa ulinzi wa jino lako, na usiku unapokwenda kulala si unapiga tena unatema povu hadi asubuhi unapopiga mswaki tena unakuwa na ulinzi wa ile dawa, hivyo bakteria watashindwa kulishambulia jino lako,” amesema.
Hatua hizi za kufuatwa kulinda meno zinatolewa wakati ambao takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 76.5 ya watu walio na miaka 15 na kuendelea wana tatizo la kuoza kwa meno huku asilimia 33.1 ya watoto wakiwa na tatizo hilo.
“Magonjwa ya fizi asilimia 67 ya watu wazima Tanzania wana ugonjwa huo na asilimia 58 ya watoto wanashambuliwa na ugonjwa huo huku asilimia 36 ya Watanzania wakiwa na mpangilio mbaya wa meno,” amesema.

Licha ya kuwapo kwa changamoto hii, lakini Dk Nzobo anasema mtaalamu mmoja wa meno Tanzania anahudumia watu 100,000 ikiwa ni zaidi ya kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutaka mtaalamu mmoja kuhudumia watu 10,000.
“Hivyo, bado tuna idadi ndogo sana ya wataalamu wa meno,” amesema Dk Nzobo.
Hayo yanasemwa wakati ambao pia Tanzania inatajwa kuwa na changamoto mbalimbali kuelekea utoaji wa huduma bora za meno ikiwemo kukosekana kwa vifaa vya kisasa, miundombinu, teknolojia na fedha za kutosha jambo ambalo linafanya watu wengi kushindwa kufikia huduma za afya ya meno.
Kutokana na hili, tayari Tanzania imelenga kuhakikisha utoaji wa huduma za meno unafikia asilimia 20 katika vituo vya afya ifikapo mwaka 2030.
Changamoto zilizopo katika sekta hiyo unaifanya dunia kuendelea kutumia fedha nyingi katika kutibia magonjwa ya meno ambapo kiasi cha Sh94.01 trilioni kilitumika mwaka 2023 ambapo kiliongezeka hadi kufikia Sh103.49 trilioni mwaka 2024 na ikitarajiwa kufikia Sh253.42 trilioni mwaka 2030.
Kwa upande wa Afrika mwaka 2022, Sh1.43 trilioni ambayo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia Sh2.63 trilioni mwaka 2030.
Akizungumzia mkutano utakaofanyika baadaye mwezi huu, Dk Nzobo amesema wanategemea uwepo wa watengenezaji wa vifaatiba kutoka nchi mbalimbali kushiriki katika maonyesho hayo, huku wadau wengine kutoka nchi mbalimbali za Afrika kuleta wataalamu watakaotoa mafunzo mbalimbali.
“Itakuwa na maonyesho watu wataona maendeleo ya teknolojia ya kinywa na meno, kutakuwa na utoaji elimu kutoka kwa madaktari kutoka hospitali mbalimbali kutakuwa na madarasa yanayofundisha utumiaji wa vifaa, mbinu za matibabu na ukuaji wa teknolojia,” amesema.
Pia, kupitia maonyesho hayo wananchi wataona bidhaa mbalimbali na kujifunza namna ya kutunza kinywa na meno aina za meno za watoto na watu wazima, miswaki inayopaswa kutumika jambo ambalo litaenda sambamba na uchunguzi kutoka kwa wataalamu wa kinywa na meno.
“Pia, hi itakuwa fursa kwa kliniki mbalimbali kujinunulia vifaatiba na dawa ambazo wanaweza kutumia kwa mwaka mzima,” amesema Dk Nzobo.
Rais Mteule wa Chama cha wataalamu wa meno, Dk Anold Agustino amesema maonyesho hayo ni eneo muhimu kwa wataalamu kujifunza teknolojia mpya ambazo zimegunduliwa katika eneo hilo sambamba kujifunza vitu vipya.