Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbege, kiburu vyatajwa kuimarisha kinga ya mwili

Muktasari:

  • Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba, KCMC wataja faida ya kiburu, mbege katika kuimarisha kinga ya mwili.

Dar/Moshi. Majaribio ya utafiti wa kisayansi, yamebaini mbege na vyakula vya asili, kikiwamo kiburu vina faida kubwa katika uimarishaji kinga ya mwili kwa mwanaume.

Kiburu ni chakula cha asili cha jamii ya Wachanga ambacho hupikwa kwenye chungu kwa kuchanganya maharage, ndizi na viungo kama nyanya na kitunguu. Mbege ni kinywaji kinachotengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu, ulezi na maji.

Mlo wa jadi wa Kiafrika uliojaa mbogamboga, nyuzi lishe, kiburu na vyakula vilivyochachushwa ikiwamo mbege unatajwa kuwa na athari chanya katika kuongeza kinga za mwili.

Uchachushaji ni mchakato wa kibaolojia unaofanywa na vijidudu kama vile bakteria au chachu (hamira), ambao hupunguza au kuvunja sukari (glucose) na kugeuza kuwa bidhaa kama vile pombe bila kutumia oksijeni.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba, KCMC uliochapishwa katika jarida la Nature Medicine Aprili 3, 2025 unaonyesha hayo.

Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Aprili 5, 2025 Mhadhiri na Mtafiti kutoka KCMC ambaye ni kiongozi wa utafiti huo, Dk Godfrey Temba anasema ulilenga  kuona athari za kinga na kimetaboliki za mlo wa asili ya Kiafrika dhidi ya mlo wa Kimagharibi kwa wanaume uliofanyika Aprili 22, 2021 mpaka Julai 3, 2021 na kurudiwa kwa vipimo Agosti 9, mwaka huohuo.

Anasema utafiti huo uliofanywa kwa wanaume 77, awali waliufanya kwa vijana wa miaka 20 hadi umri wa miaka 70 mijini na vijijini wakagundua wanaokula vyakula asili miili yao inatengeneza kinga zaidi.

Anasema utafiti huo uliwafanya kutaka kujua kinga inatengenezwaje na ni vipi inaweza kuboreshwa.

Dk Temba amesema walikwenda Kijiji cha Urushimbwe wilayani Moshi, wakaweka kambi. Anasema waliwachukua wanaume wa miaka 20 mpaka 40 wenye afya njema waliowafuatilia kwa wiki mbili kujua wanachokula asubuhi mpaka jioni, wakiendelea kufuata lishe zao za asili kisha walichukua sampuli.

Anafafanua kuwa baadaye waliwapatia vyakula vya watu wa mijini kama vile chai ya maziwa, soseji na mkate asubuhi, mchana chipsi yai na vyakula vilivyokaangwa na jioni nyama choma kwa wiki mbili.

Anasema walibaini kubadilishiwa mlo kutoka wa asili ya Kiafrika kwenda wa Kimagharibi kwa wiki mbili tu, kunaweza kusababisha uvimbe (inflammation), kupunguza mwitikio wa kinga dhidi ya vijidudu na kuchochea michakato inayohusiana na magonjwa ya mtindo wa maisha.

Dk Temba anasema kundi la pili lilikuwa la watu wa mijini, ambao walichukua sampuli kabla na baadaye waliwapatia vyakula asili yakiwamo magimbi na uji wa ulezi asubuhi, ugali wa mahindi na muhogo, mchicha na bamia mchana na jioni walikula kiburu na parachichi.

Anasema walibaini kinga zao ziliimarika kutokana na kula mlo wa asili ikilinganishwa na sampuli za awali.

Dk Temba anasema kundi la tatu lilikuwa la watu maalumu wenye umri mkubwa ambao walihojiwa kuhusu hali zao za afya, sababu ya kutozeeka na kuwa na afya njema.

Wengi anasema walieleza wamekuwa wakinywa mbege, akiwamo mzee wa miaka 82 mwenye nguvu.

"Tuliwachukua wanaume wanaoishi mijini na hawanywi mbege, tukawapatia kila siku lita moja ya mbege jioni, baada ya wiki moja tukabaini   kinga zao ziliimarika tofauti na walizokuwa nazo mwanzoni, zikaanza kupambana na vimelea vya magonjwa. Tulibaini kinga zao kupanda kwa kasi. Mbege ilionyesha matokeo makubwa kwa kuupa mwili kinga," anasema.

Kuhusu sababu ya mbege kuongeza kasi ya kinga mwilini Dk Temba anasema, "huu ni utafiti tunaoendelea nao kwa sasa, majibu yake yatatoka baadaye ila tayari tuko maabara kwa kazi hii."


Sababu za utafiti

Anasema sababu za utafiti huo ni kuwapo kwa magonjwa ya moyo, kisukari na hali sugu za uvimbe yanaongezeka kwa kasi barani Afrika na kuleta changamoto kubwa kwa mifumo ya afya.

Ili kuelewa madhara ya mabadiliko ya lishe kiafya, anasema watafiti kutoka Chuo Kikuu cha KCMC na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (KCRI) nchini Tanzania wamechunguza athari za mabadiliko hayo kwa afya.

"Wanaume 77 wenye afya, kutoka maeneo ya mijini na vijijini, walishiriki katika utafiti huu,” anasema.

Dk Temba anasema watafiti walichunguza kwa kina utendaji wa mfumo wa kinga, alama za uvimbe katika damu na michakato ya kimetaboliki kabla ya mabadiliko ya lishe, baada ya wiki mbili na tena wiki nne baadaye.

Anasema washiriki waliobadilika kwenda kula mlo wa Kimagharibi walionyesha kuongezeka kwa protini za uvimbe kwenye damu na kuanzishwa kwa michakato ya kibaolojia inayohusiana na magonjwa ya mtindo wa maisha.

"Seli zao za kinga zilionyesha mwitikio mdogo dhidi ya vijidudu. Kwa upande mwingine, waliobadilika kula mlo wa asili ya Kiafrika au waliokunywa mbege walionyesha kupungua kwa viashiria vya uvimbe," anasema Dk Temba.

Anasema baadhi ya athari hizo ziliendelea hata baada ya wiki nne, jambo linaloonyesha kuwa hata mabadiliko ya muda mfupi ya lishe, yanaweza kuwa na athari za muda mrefu.

Kwa mujibu wa Dk Temba, huu ni utafiti wa kwanza kuchunguza kwa undani athari za kiafya za mlo wa jadi wa Kiafrika.

"Utafiti wa awali umekuwa ukilenga zaidi milo ya jadi ya Kijapani au ya Mediterranean. Hata hivyo, kuna mengi ya kujifunza kutoka kwenye milo ya Kiafrika, hasa sasa mitindo ya maisha inabadilika haraka na magonjwa kutokana na mitindo hiyo yanaongezeka. Tofauti kubwa ya milo ya jadi Afrika ni fursa ya kipekee ya kupata maarifa ya jinsi lishe inavyoathiri afya,” anasema.


Wasemavyo wananchi

Baadhi ya wananchi wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro wamesema mbege imekuwa ikitumiwa tangu enzi na wazee na imekuwa na faida mbalimbali mwilini.

Mbege inaheshimika kwa Wachaga kutokana na mila na desturi, ikitumika katika ibada za kimila na sherehe za kijamii.

Athanas Joseph, mmoja wa wazee wilayani humo anasema mbege ni utamaduni wa kila siku wa jamii ya Wachaga.

Anasema huitumia kama chakula hata wanapokwenda shambani.

"Mbege kwetu ni kama chakula, mtu akienda shambani huwa na kibuyu pembeni chenye mbege, akiwa shambani akinywa humpa nguvu akafanya kazi bila kuchoka," anasema.

Amedea Shayo anasema: "Sisi kina mama huku vijijini tuna shughuli nyingi, wakati mwingine ukiwa umechoka baada ya kutoka kwenye shughuli zako za utafutaji unatafuta kitu cha kukupa nguvu, kwa hiyo unakunywa mbege na unakaa sawa. Hata mama anayenyonyesha huitumia ili kupata maziwa.”


Mbege inavyotengenezwa

Christian Tesha, mmoja wa watengenezaji mbege anasema kinywaji hicho kina wateja na gharama zake ni kidogo ambazo 'bohora' moja huuzwa kati ya Sh500 na Sh1,000.

"Ili mbege iitwe mbege ni lazima uandae ndizi mbichi  kwa kuivundika kwa siku sita, baada ya hapo humenywa na  kuchemshwa na maji kwenye sufuria kubwa na inachemka kwa muda mrefu," anasema.

Anasema baadaye huwekwa kwenye pipa na baada ya siku moja hukamuliwa, kuchujwa na kisha huwekwa kwenye pipa. Kesho yake huwekwa unga wa ulezi.

"Unachukua ulezi unauosha na kuutoa maji, unauvundika kwa siku kadhaa ambapo huota majani, kisha unauanika juani ukikauka  unasagwa na kisha unga wake unatengenezea uji, ambapo ukishapoa unauchanganya na ule uji wa ndizi, ndipo kinywaji sasa kinakuwa tayari," anasema.