Maumivu ya mgongo; Tatizo kubwa linalosumbua wengi nchini

Mfanyakazi akiwa ameketi kwenye kiti ofisini. Maendeleo yamesababisha watu wengi kutumia muda mwingi kuketi.
Muktasari:
- Maumivu ya mgongo hujitokeza zaidi kwa watu wa umri wa miaka 20-40 na ndio mara nyingi wanaofika kwa ajili ya matibabu, hapo baadaye nusu ya wagonjwa hupata maumivu makali kuliko ilivyokuwa mwanzoni na ikitokea maumivu yakawa sugu huambatana na matatizo mengine kama vile kukosa usingizi, unajisikia kulala mara kwa mara, lakini usingizi huwa mfupi hii ni kutokana na kushtuka mara kwa mara nyakati za usiku.
Usione watu wakitania, lakini mgongo una umuhimu wake katika maisha.
Jiulize, wewe ambaye umelitumikia taifa lako kwa takriban miongo mitatu huku uwajibakaji wako kazini ukiwa hauna shaka na wenye tija katika eneo unalofanyia kazi hali itakuwa vipi baada ya kustaafu.
Ukiwa katika umri mkubwa na pengine kukaribia kustaafu unaanza kupata tatizo la maumivu ya mgongo ambayo hukomaa na kuwa sugu.
Hivi ndivyo ilivyomkuta Elida Miti mtumishi wa Serikali aliyestaafu kwa sasa (si jina lake) akiwa na umri wa miaka 58 alipatwa na tatizo la kuumwa mgongo kwa muda mrefu hali iliyomlazimu kuwa kitandani kwa siku nyingi.
Tatizo hili lilimfanya Miti kutoweza kuendelea na kazi kwa muda mrefu lakini baada ya mafanikio ya upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alipona na kurudi kazini kuendelea na kazi zake kwa kipindi kilichobakia mpaka kustaafu kwake.
Mama huyu mwenye watoto watano ana historia ya kuwa na uzito mkubwa na kutofanya mazoezi, kipindi akiwa kazini muda mwingi alikuwa kwenye kiti kilichosimama nyuzi 90 akifanya kazi ya kuandika na kuchapa kazi katika kompyuta yake akiwa ameinama muda mwingi huku akichambua majalada lukuki.
Historia zaidi inaeleza kuwa cheo alichonacho ilimbidi kwenda sehemu mbalimbali nchini kwa usafiri wa barabara.
Takribani kila miezi mitatu alikuwa ana safari zaidi ya nne. Hivyo, ilimfanya kuwa mtu wa kusafiri na huku akitumia muda mwingi kukaa katika kiti cha gari, huku akipita katika barabara zilizo na lami zenye matuta na zisizo na lami zenye mashimo.
Historia ya mgonjwa huyu imetumika ili angalau tuweze kupata picha na hali zetu za kiafya na kazi tunazofanya, aina za kazi tunazofanya, kusogea kwa umri, kutokuwa na muda wa mazoezi, kuzaa, yote haya yanachangia kuwa na maumivu ya mgongo, zaidi ya yote miili yetu na mienendo yetu kimaisha ikichangia kwa kiasi kikubwa.
Ukubwa wa tatizo kiafya
Maumivu ya mgongo ni moja ya matatizo ya kiafya yanayojitokeza mara kwa mara na huathiri zaidi misuli na mifupa ya mgongo.
Tatizo hili Iinawaathiri karibu asilimia 40 katika moja ya hatua za maisha yao. Maumivu ya mgongo yapo ya kawaida (chini ya wiki 6), yapo ya maumivu ya kati (wiki 6-12) na maumivu sugu ambayo ni zaidi ya wiki 12.
Maumivu haya yakiainishwa zaidi yanaweza kutokana na kupata majeraha ya kawaida au mambo yasiyo ya majeraha na chanzo cha maumivu haya kinaweza kuwa eneo husika au maumivu yalitokea mahali pengine mwilini.
Mara nyingi maumivu haya chanzo na sababu hasa hakigunduliki moja kwa moja na hakujitokezi mapema, lakini inaminika kuwa chanzo cha maumivu haya huenda yametokana na kujeruhiwa kwa misuli au mifupa ya mgongo.
Pale endapo itatokea maumivu hayo kutoisha baada ya matibabu ya kawaida ama kuambatana na viashiria hatari kama vile kupungua uzito kusikokuwa na sababu maalum, homa kali, kushindwa kuhisi chochote maeneo ya makalio au miguu na kushindwa kujongea vizuri, hali kama hizi lazima hatua za haraka zitahitajika kwa ajili ya uchunguzi kwani ni kawaida maumivu ya mgongo kupotea baada ya matibabu chini ya wiki 6 kwa asilimia 40-90 ya wagonjwa.
Usiyoyajua kuhusu mgongo
Umbile la mgongo ni kama vile herufi S likiwa na maeneo makuu matano, yaani cervical, thoracic, lumber, sacral na coxgeal.
Mgongo unaundwa na pingili za vifupa 24 vilivyoshikizwa na kutengeneza maungio, pia kuna vifupa tisa vilivyoshikamana katika mwishilio wake ndiyo unaona kama vile mkia, ndiyo inafanya jumla ya mifupa 33.
Katikati ya pingili hizi huwa na sahani kama plastiki, pia huwa na matundu ya pembeni na kati, na kutengeneza mfereji maalum unaopita uti wa mgongo. Uti wa mgongo ndio chanzo cha maelfu ya mishipa ya fahamu inayopeleka na kuleta taarifa za mfumo wa fahamu toka sehemu mbalimbali mwilini na kuzipeleka katika ubongo kwa ajili ya tafsiri.
Kifupa cha kwanza na cha pili ndivyo vinavyoweza kwenda mijongea mbalimbali kama vile unaposema ndiyo na hapana kwa mwitiko wa kichwa, vile vile mifupa 12 ya mbavu hukutana na pingili za mifupa ya mgongo na kutengeneza ungio.
Kazi kuu ya mgongo ni kuuwezesha mwili kuwa na umbile maalumu linalowezesha mwili kusimama, kuulinda uti wa mgongo ambao ni rahisi kudhurika, ni kiunganishi cha kichwa na kiwiliwili na vilevile mwishilio wa mgongo ndiyo kwa kiasi kikubwa unatusaidia kutembea.
Dalili za maumivu ya mgongo
Mara nyingi mtu huweza kuhisi maumivu pale panakuwepo na mjongeo yaani kunyanyua kitu, kunyanyuka na kupiga hatua, kujipinda au kujinyoosha.
Mtu hujigundua kuwa na maumivu pale anapoamka asubuhi. Ukali wa maumivu hutegemeana na hutofautina na eneo la mgongo na yanaweza yakachokozwa au yakawa tuli na kutokana na aina ya mkao unaotumia.
Mfano, kukaa au kusimama, kunyanyua mguu na wakati mwingine maumivu hushuka mpaka miguuni.
Maumivu ya mgongo hujitokeza zaidi kwa watu wa umri wa miaka 20-40 na ndio mara nyingi wanaofika kwa ajili ya matibabu, hapo baadaye nusu ya wagonjwa hupata maumivu makali kuliko ilivyokuwa mwanzoni na ikitokea maumivu yakawa sugu huambatana na matatizo mengine kama vile kukosa usingizi, unajisikia kulala mara kwa mara, lakini usingizi huwa mfupi hii ni kutokana na kushtuka mara kwa mara nyakati za usiku.
Katika hatua za baadaye wengi wa wagonjwa wenye tatizo hili hupata magonjwa ya akili kama vile msongo wa mawazo, sonona na woga uliopitiliza.
Sababu za maumivu ya mgongo
Huwa si tatizo linalosababiswa na ugonjwa fulani pekee bali huwa na sababu nyingi zinazoleta tatizo hilo, hakuna uhakika wa moja kwa moja sababu hasa inaleta maumivu haya, lakini inaaminika kuwa ni matokeo yaliyotokana na majeraha ya kawaida ya misuli na mifupa.
Uzito uliokithiri, uvutaji tumbaku, kuongezeka uzito kipindi cha ujauzito, shinikizo la kimwili, kutofanya kazi, mkao wa ovyo, ulalaji usioendana kimwili, haya ni mambo yanayoambatana na maumivu ya mara kwa mara ya mgongo.
Kwa upande wa magonjwa mwilini kama vile baridi yabisi ya mifupa, shambulizi la maungio, kunywea na kuchoropoka kwa sahani za mgongo, sahani za mgongo kujipenyeza katika uti wa mgongo, kuvunjika kwa vifupa vya mgongo mfano kumomonyoka kwa vifupa, yapo mambo mengine yanayosababisha ingawa ni nadra ni saratani au uvimbe au uambukizi.
Pia, yapo matatizo ya kinamama yanayoambatana na maumivu ya mgongo, kama vile kujipandikiza kusiko kwa kawaida kwa tishu za mfuko wa uzazi, saratani ya mirija ya uzazi, saratani ya ovary, uvimbe wa mfuko wa uzazi.
Karibu nusu ya wanawake waliowahi kuwa wajawazito hupata tatizo la maumivu ya chini ya kiuno wakati wa ujauzito hii ni kutokana na mabadiliko ya ujauzito yanayosababisha kuwa na mkao usio wa kawaida na mgandamizo wa misuli na nyuzi zinazoshika mifupa ya kiuno na mgongo.
Viashiria vya hatari
Endapo utaumwa mgongo na uzito ukipungua huku ukiwa na historia ya kuugua saratani hiyo ni dalili inayoweza kuashiria uwepo wa saratani iliyosambaa.
Kushindwa kudhibiti haja kubwa na ndogo, kukosa hisia za mihemko ya kimwili, misuli kudhoofika, kukosa hisia katika maeneo ya makalio, hii ni dalili inayoambatana na ugonjwa wa mfumo wa fahamu uitwao kitaalamu, cauida equine syndrome.
Ajali zilizoambatana na umri mkubwa na matumizi ya mda mrefu ya dawa jamii ya corticosteroidi hii huashiria kuvunjika kwa pingili za mifupa ya mgongo.
Kuwa na maumivu makali sana ya chini ya mgongo kwa mtu aliyewahi kufanyiwa upasuaji mwaka uliopita.
Uwepo wa homa kali, uambukizi njia ya mkojo, upungufu wa kinga mwilini, utumiaji wa dawa kwa njia ya mshipa, ni viashiria vya uwepo wa maumbukizi mwilini. Mambo haya ni viashiria hatari kuwa mwilini kuna tatizo kubwa hivyo hatua za haraka zinahitajika kwa ajili ya uchunguzi wa kina na matibabu.