Kula kabichi uepuke magonjwa, upunguze unene

Kabichi ni mboga ya majani inayolimwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mboga hii inapatikana kwa wingi sokoni, karibu kipindi chote cha mwaka.
Katika mapishi, wengi hupenda kuchanganya kabichi na nyama, huku wengine wakiitumia kutengeneza saladi (wengi huita kachumbari) kwa kuchanganya na tango, nyanya na pilipili hoho.
Faida za Kabichi
Kabichi imeonekana kuwa na uwezo wa kipekee wa kupambana na magonjwa ya saratani kutokana na kuwa na aina tatu za virutubisho vya Antioxidant, Anti –inflammatory na Glucosinolates vyenye uwezo wa kuzuia magonjwa nyemelezi yanayosababisha saratani.
Takriban tafiti 475 zimefanyika kuhusu virutubisho hivyo vinavyopatikana kwenye kabichi na kuthibitisha kwamba, vina uwezo wa kuzuia saratani ya matiti, utumbo mpana na tezi dume.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Stanford unaonyesha kuwa wagonjwa 13 waliokuwa wanaugua vidonda vya tumbo walipona kwa kunywa juisi ya kabichi mara tano kwa siku kwa kipindi cha siku saba hadi 10.
Faida kubwa ambayo watu wengi wanaifahamu ni uwezo wa kupunguza uzito na unene kwa kuwa ina kiwango kidogo sana cha Kabohidreti na mtu anayetaka kupunguza unene na uzito anashauriwa kula saladi ya kabichi kwa wingi.
Imeandaliwa na Hadija Jumanne, Mwananchi