Kichaa cha Mbwa: Ugonjwa unaowaathiri wakazi Dodoma

Aghalabu siku haiwezi kwisha bila kuona mbwa akikatisha katika mitaa ya katikati ya mji, wakati wa mchana bila kuwa chini ya uangalizi.
Muktasari:
- Baadhi ya wakazi wa Dodoma Mjini wamesema kuwa tatizo la mbwa kuzagaa ovyo limekuwa kero kubwa kwao.
Mbwa ni mnyama wa kufugwa mwenye manufaa chekwa. Anaisaidia jamii kwa mambo mbalimbali ikiwemo ulinzi, kazi za kiusalama na hata utunzaji wa mazingira.
Kwa sababu anaishi kwa ukaribu kabisa na wanajamii anahitaji kutunzwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanapata chanjo.
Hali katika Mkoa wa Dodoma, imekuwa kinyume kwa sababu kumekuwa na idadi kubwa ya mbwa wanaozurura mitaani jambo ambalo linahatarisha maisha ya wakazi.
Uchunguzi uliofanywa katika maeneo mbalimbali ulibaini kuwa kuna idadi kubwa ya mbwa wanaozurura ovyo kwenye maeneo ya Area A, Swaswa, Area D na hata katikati ya mji.
Aghalabu siku haiwezi kwisha bila kuona mbwa akikatisha katika mitaa ya katikati ya mji, wakati wa mchana bila kuwa chini ya uangalizi.
Ofisa Mfuatiliaji wa Mgonjwa yanayotokana na chanjo mkoni hapa, Paul Mgeni, anasema tatizo la watu kung’atwa na mbwa ni kubwa.
“Si chini ya watu 10 ambao wamekuwa wakiripoti katika hospitali yetu (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma) kuwa wameumwa na mbwa na hasa hasa wanaoathirika ni watoto wadogo,” anasema.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha kati ya Januari na Oktoba mwaka jana, jumla ya watoto 278 walio chini ya umri wa miaka mitano waling’atwa na mbwa mkoani hapa.
Kati ya hao watoto 165 walikuwa ni wa kiume wakati watoto 113 walikuwa ni wa kike. Kwa mujibu wa takwimu hizo watu zaidi ya umri wa miaka mitano waliong’atwa na mbwa katika kipindi hicho, walikuwa ni 1580 ambapo kati ya hao wanaume walikuwa 931 wakati wanawake walikuwa 649.
Mwaka juzi, watoto chini ya miaka mitano walikuwa ni 326 na waliojuu ya miaka mitano walikuwa ni 877.
Mageni anasema watu 16 walipoteza maisha mkoani hapa kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Hata hivyo anasema wengi wa watu wanaokuja kupata matibabu hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua chanjo.
Chanjo ya kichaa cha mbwa
Kwa mujibu wa Mageni, dozi moja (chupa moja) ya chanjo hiyo inayojulikana kama Anti-Robies, inauzwa Sh27,000 katika hospitali za Serikali wakati katika maduka ya dawa binafsi chupa moja huuzwa kwa kati ya Sh30,000 hadi Sh40,000 kwa chupa.
Anasema ili mgonjwa awe amekingika na kichaa cha mbwa, anatakiwa kuchanjwa chupa tatu kwa mara tatu.
“Anapokuja tunamchanja chupa moja, baada ya siku saba anachanjwa nyingine na baada ya siku 28 anamalizia dozi. Mtu akikatisha anakuwa hajapata kinga na hivyo kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa kichaa,” anasema Mageni.
Mageni ambaye pia ni Mratibu wa Huduma za Chanjo mkoani hapa, anasema wagonjwa ambao hawana uwezo wa kumudu gharama hizo wamekuwa wakiombewa kibali katika ofisi ya Ustawi wa Jamii ili waweze kuchanjwa bure.
“Kuna mwingine anakuja ukimwangalia wewe mwenyewe unaridhika kuwa hawezi kulipia huduma hiyo inabidi umpeleke katika kitengo cha msaada na wapo pia wenye uwezo kidogo hawa wote hupatiwa msaada baada ya majadiliano na uongozi,” anasema.
Chanjo ya kichaa cha mbwa
Mageni anasema kwa miaka ya nyuma Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilikuwa ikileta chanjo ya kichaa cha mbwa sawa sawa na za magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo.
Lakini mwaka jana, Serikali ilisitisha kuleta chanjo hiyo kwa sababu inagharama kubwa na kuzitataka wilaya kuingiza katika mipango yao madhubuti ya afya.
“Mwaka jana wizara ilisitisha kuleta hizo dawa kutokana na kupanda kwa gharama, kwamba Serikali haiwezi tena ku-manage (kumudu), kununua chanjo hiyo,” anasema Mageni.
Anasema wao walipokea maelekezo yanayoziagiza wilaya kuingiza manunuzi ya chanjo hiyo katika mipango yao madhubuti ya afya ambapo waliwapelekea wilayani.
“Tumeagiza pia wilaya ziwe na dirisha maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa waliong’atwa na mbwa ili kupunguza usumbufu kwa wananchi, baadhi ya wilaya zimeanza utekelezaji wa agizo hilo,” anasema Mageni.
Aidha, anasema wanapokutana katika vikao vya kutokomeza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano wamekuwa wakihamasisha wilaya ziweke gharama ya chanzo hizo katika mpango kazi wao.
Anapoulizwa kwa nini baadhi ya wagonjwa wanafuata chanjo hiyo mjini, Mageni anasema chanjo hiyo huhifadhiwa katika mnyororo baridi kwenye hospitali hiyo ya Mkoa.
“Hapo zamani chanjo hizi zilikuwa zikipatikana katika Hospitali ya Mkoa tu, tulikuwa hatuja decentralize (hawajasambaza), huduma hiyo na ndiyo hapo wagonjwa kutoka wilayani walikuwa wakilazimika kuja kufuata huduma hapa,” anasema.
Huduma ya kwanza kwa mgonjwa
Anasema jambo la kwanza ni kuchukua maji na kuosha vyema kidonda na kwa wale wa vijijini (kwenye shida ya maji safi na salama), wanatakiwa kuchemsha maji na kuweka chumvi kidogo ndipo wamuoshe mtu aliyeng’atwa na mbwa.
“Kidonda cha kung’atwa na mbwa hakitakiwi kufungwa, kinaachwa wazi maana mbwa anapomng’ata huwa anaacha wadudu pale. Unakiacha wazi ili wakati uchafu unapotoka na wadudu watoke,” anasema Mageni.
Anasema hata anapofika hospitali wanachokifanya ni kukifanyia usafi wa hali ya juu kidonda na kisha kukiacha wazi.
Mageni anasema katika viwango vya kimataifa mtu ambaye amen’gatwa na mbwa mwenye kichaa, anatakiwa awe amemaliza chanjo yake ndani ya siku 50.
“Kwa kifupi kila anayeng’atwa na mbwa anatakiwa kuanza matibabu mapema ingawa tunasema kuwa uwezekano wa kupona unakuwa ni mdogo kama mgonjwa atakuja kuanza matibabu baada ya siku 50,” anasema.
Dalili za kichaa cha mbwa
Anasema dalili za kichaa cha mbwa zipo nyingi inategemea ni nini kimetangulia lakini dalili ya kwanza kubwa ni mgonjwa kuogopa maji.
“Ukifungulia maji mgonjwa huogopa na kama ukimwonyesha kikombe cha maji anaweza kukitupia mbali,” anasema.
Anabainisha dalili nyingine ni mgonjwa kushindwa kula chakula na wakati mwingine katika hatua za mwisho mgonjwa hutoka udenda uliochanganisha na damu mdomoni.
Aidha, anasema mgonjwa huwa kichaa na kama anayemhudumia hawi makini basi anaweza kumuuma na kumweka katika hatari ya kumwambukiza kichaa cha mbwa.
“Ugonjwa huu hautibiki. Kwa mujibu wa taarifa za kimataifa inasemekana ni mgonjwa mmoja tu aliwahi kupona duniani,” anasema.