Faida ya tunda hili kwa mwenye kisukari

Inawezekana ukajiuliza matunda yapi yanafaa kuliwa na mgonjwa wa kisukari.

Kuna matunda mengi ambayo wagonjwa wa kisukari huwa na hofu ya kula pasipo kujua kuwa yana faida tele, hasa katika kudhibiti viwango vya sukari mwilini, kuongeza kinga za mwli na kuboresha afya ya mwili kiujumla.

Tunda kama komamanga, lina kalori kidogo sana na ni tunda lenye nyuzinyuzi nyingi, vitamin na madini.

Komamanga lina molekuli ijulikanayo kama ‘antioxidants’ za kutosha, hulinda na kuimarisha afya ya moyo, na husaidia kulinda seli za mwili zinazoweza kuharibiwa na magonjwa sugu kama kisukari au saratani.

Antioxidants kutoka kwa matunda kama vile makomamanga, ni njia nzuri ya kusaidia afya kwa jumla na kuzuia magonjwa.

Si tunda tu, bali ni chakula chenye vitamini, madini pamoja na virutubisho vingine vingi vinavyoweza kufanya miili yetu kuwa na afya na nguvu tele.

Virutubisho vinavyopatikana katika komamanga ni vitamin C kwa wingi, vitamin B5, vitamin A, vitamin E, Madini ya Potassium na Iron.

Wataalamu wa lishe wanasema kuwa matunda yenye kirutubisho cha polyphenolic, kama vile komamanga, yanaweza kuimarisha na kuboresha afya ya moyo. Juisi ya komamanga hupunguza ukali wa maumivu ya kifua, hatari ya maradhi ya moyo na shinikizo la damu.

Juisi ya mbegu za komamanga husaidia kuepuka saratani na kusaidia mtiririko wa damu kwenda vizuri katika mishipa ya damu, hivyo kupunguza hatari sio tu ya magonjwa ya moyo, shinikizo la damu pekee ila huepusha kiharusi.

Baadhi ya tafiti zinaonyesha komamanga lina kirutubisho kiitwacho ellagitannins kinachoweza kusaidia kulinda afya ya ubongo dhidi ya ugonjwa wa Alzeima na Parkinson.

Faida nyingine ya ulaji wa komamanga ni katika kuboresha afya ya figo. Hata hivyo, vyakula vilivyo na ellagitannins na potassium nyingi vinaweza kutoa faida kwa mwili mzima, ikiwa ni pamoja na figo.

Ikiwa unaishi na ugonjwa wa figo, ni muhimu kujadili na daktari kuhusu ulaji wa makomamanga pasipo kuleta athari yoyote.

Wagonjwa wa kisukari wenye tatizo la mafuta kwenye damu ‘cholesterol’, wakila komamanga mara kwa mara wanaweza kuepuka au kumaliza tatizo la mafuta kwenye damu, husaidia kurekebisha presha ikae sawa.

Husaidia kuimarisha mfumo wa meno kinywani, kwa wale wenye tatizo huwa linaondoka kwa kula sana tunda hilo.

Komamanga husaidia pia kutokomeza ugonjwa wa kuharisha, kwa mtu anayeharisha akitumia juisi yake anapata nafuu. Husaidia kupunguza uzito na kukuweka sawa.

Licha ya faida hizo, pia huongeza hamu ya kula. Husaidia usagaji wa chakula mwilini.

Angalizo kwa wagonjwa, komamanga sio tiba au dawa ya magonjwa tajwa, isipokuwa ni tunda lenye virutubisho vinavyoweza kuboresha kinga za mwili.