Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zigo la takataka linavyoitesa Kinondoni

Rundo la takataka zikiwa zimetupwa kando kando ya Barabara ya Kigogo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam licha ya eneo hilo kutoruhusiwi kutupwa takataka. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Katika mkakati wa kukabiliana na ongezeko la takataka mitaani, wilaya ya Kinondoni imeanzisha utaratibu mpya ambako wakandarasi sasa wanalipwa na manispaa, tofauti na ilivyokuwa awali

Dar es Salaam. Je, tatizo la mrundikano wa takataka katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam itakuwa historia? Maofisa wa halmashauri ya manispaa ya Kinondoni, moja ya manispaa tano jijini hapa, wanadhani hivyo kufuatia utekelezaji wa utaratibu mpya wa ukusanyaji takataka mitaani.
Utaratibu mpya wa halmashauri hiyo umebadili utaratibu wa awali wa ukusanyaji mapato yatokanayo na ukusanyaji takataka. Awali  wakandarasi walikuwa wanakusanya takataka na kuzitupa kwenye jalala la Pugu Kinyamwezi lilipo katika viunga vya jiji la Dar es Salaam na lile la Mapinga, wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani.
Pia walikuwa wakilipwa hapo hapo baada ya kukusanya takataka kutoka kwa wenye nyumba au majengo ya kibiashara lakini halmashauri ilikuwa ikilia, iliachwa gizani haikujua lolote juu ya fedha zinazokusanywa. Si tu kiwango kinachokusanywa, bali pia nani anapata nini na kwa taratibu zipi.
Mbaya zaidi, manispaa ilikuwa haipati hata shilingi kutoka kwenye fedha zilizokusanywa.

Ukusanyaji mdogo
Halmashauri ya Kinondoni inakadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha takataka takribani tani 1,223 kwa siku lakini uwezo wa kuzikusanya ni mdogo, ukikisiwa kuwa kati ya asilimia 51 na 67.6.
Hali hii iliilazimisha manispaa kubuni mbinu mpya. Katika barua ya Septemba 13, 2018  kwenda kwa watendaji wa serikali za mitaa, mkurugenzi wa halmashauri hiyo Aron Kagurumjuli, aliandika, “kwa kipindi kirefu sasa Kinondoni imeweka kipaumbele kwenye suala la usafi bila mafanikio.”
Ndipo Oktoba, 2018, manispaa ya Kinondoni iliamua kubadilisha rasmi utaratibu wa kukusanya takataka.
Katika utaratibu mpya, wakandarasi ambao walikusanya takataka na tozo wakaachwa na kazi ya kukusanya takataka, tu tozo zikakusanywa na  manispaa kwa kutumia watu maalum.

Wakandarasi waja juu
Utaratibu mpya haukuwafurahisha  baadhi ya wakandarasi wakidai umepunguza kipato chao na hata malipo kutoka halmashauri huchukua muda mrefu kuyapata. Mmoja wa wakandarasi hao ni Kyalo Mbatha wa kampuni ya K.J Cashpoint aliyehamishia huduma yake manisapaa ya Ubungo. “Nadhani halmashauri ina tamaa isiyozingatia hali halisi. Inadhani tunafaidika sana kwa kukusanya takataka na tozo zake,” amesema Kyalo.
Stephano Lukinga wa kampuni ya Lunyani Enterprise pia amehamishia huduma yake Ubungo akidai mtaji wake mdogo hautomuwezesha kutoa huduma chini ya utaratibu huo mpya.
Si wakandarasi wote wana maoni haya. Muganyizi Ernest wa Brifu Afrika, hana tatizo. “Mimi napata kipato changu na manispaa chake,” anasema Muganyizi anayetoa huduma Tandale. “Changamoto zipo lakini za kawaida zilizopo katika kila shughuli ya utoaji wa huduma.”
Abilu Peter ni ofisa usafi na mazingira wa halmashauri ya Kinondoni ambaye anasema utaratibu huo mpya umetokana na utafiti uliofanywa na idara yake ambao matokeo yake ndiyo yaliweka msingi wa mabadiliko ya utaratibu wa ukusanyaji wa mapato.
“Utaratibu huu umelenga kuimarisha usafi katika halmashauri yetu. Naweza sema hadi sasa tuna mwelekeo mzuri,” amesema Abilu.
“Kwa upande wa mapato, kwa mfano, mpaka sasa tumekusanya jumla ya Sh2.35 bilioni tangu utaratibu huu uanze kutumika.”

Utaratibu mpya wazaa matunda
Mbali na mfumo holela wa ukusanyaji wa mapato, hoja nyingine ya manispaa ya kuleta utaratibu huu mpya ni kwamba wakandarasi katika halmashauri ya Kinondoni wameshindwa kupunguza idadi ya takataka zinazozalishwa katika manispaa hiyo.
Takwimu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zinaonyesha kuwa wakandarasi waliweza kukusanya takataka tani 8,170, 8,375 na 7,913 kwa miezi ya Julai, Agosti na Septemba mwaka 2018.
Lakini baada ya utaratibu mpya kuanza, kiwango kilichokusanywa katika halmashauri hiyo kinaonekana kuongezeka kwa kiasi fulani. Mfano, kuanzia Oktoba hadi Novemba tani 9,190 na 9,190 za takataka zilikusanywa. Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo lakini kwa kuzingatia tani ambazo halmashauri hiyo inazalisha kwa siku ni wazi kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

Mgawanyo wa mapato
Utaratibu huu mpya unalenga kuongeza kiwango cha takataka kinachokusanywa kutoka asilimia 67.6 ya sasa hadi asilimia 85 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Tofauti na ilivyokuwa zamani, wakandarasi sasa wanapaswa kuingia mkataba na manispaa ambapo watakuwa wanalipwa kwa huduma watakayokuwa wanatoa.
Wakandarasi wanalipwa kulingana na idadi ya safari wanazofanya za kupeleka takataka kwenye majalala yaliyotengwa kwa kuzingatia uwezo wa magari yao ya kubebea.
Chini ya utaratibu huu mpya, asilimia 20 ya mapato yatokanayo na takataka hubaki katika ngazi ya serikali ya mtaa kwa ajili ya kusimamia zoezi lenyewe (asilimia 5) na asilimia iliyobaki inabaki katika hazina ya serikali ya mtaa husika.
Diwani wa Kata ya Kinondoni Mustafa Muro (Chadema) ameupongeza utaratibu huo mpya akisema kwamba utasaidia kutimiza ahadi yake ya kampeni.
“Wapiga kura walinichaguwa kwa kuwaahidi kwamba nitahakikisha mazingira yao kuwa safi. Hii isingewezekana chini ya utaratibu wa zamani,” amesema Muro.


Safari bado ndefu
Wakati mchakato wa kufuatilia habari hii umeanza mwezi uliopita, miezi sita baada ya utaratibu mpya kuanzishwa, Mwananchi iliweza kushuhudia mrundikano wa takataka katika mitaa kadhaa ndani ya halmashauri ya Kinondoni inayoonekana kutelekezwa na wakandarasi.
Mmoja kati ya wananchi katika mitaa hii, Reginald Mlingi, 35, kutoka mtaa wa Kanazi, Kinondoni, alisema kwamba hakumbuki ni lini ilikuwa mara ya mwisho kuona gari la taka linapita mtaani kwake.
“Pengine wanaweza kuja mara moja kwa mwezi, kama nitakuwa nipo sahihi,” anasema Mlingi huku akionyesha mrundikano wa taka pembezoni mwa barabara, karibu na kibanda cha wauza ‘chips.’
Kanazi ni moja tu kati ya mitaa kadhaa ya Kinondoni ambako kuna mrundikano wa takataka kitu ambacho kinaashiria safari ndefu inayoikabili halmashauri hiyo katika mpango wake wa kudumisha usafi katika viunga vyake.