Wizara ya fedha Tanzania yasema haitoi mikopo

Muktasari:
Wizara ya fedha nchini Tanzania imekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa imeungana na Benki ya Dunia (WB) na taasisi binafsi kutoa mikopo ya biashara na kilimo bila riba.
Dar es Salaam. Wizara ya Fedha na Mipango nchini Tanzania, imekanusha habari inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo Facebook kuwa inatoa mikopo bila riba ya kilimo na biashara.
Kanusho hilo limetolewa leo Ijumaa Juni 28, 2019 na Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja baada ya kusambaa taarifa inayoonyesha wizara hiyo imeungana na taasissi nyingine kutoa mikopo kwa wakulima na wafanyabiashara bila riba.
Taarifa hiyo iliyopo kwenye mfumo wa picha inaeleza wizara ya fedha imeungana na taasisi binafsi iitwayo Global Entrepreneurship Forum na benki ya dunia kutoa mikopo hiyo.
"Hii taarifa ni ya uongo tunaomba muwafahamishe Watanzania kuwa haijatoka kwetu wala hakuna suala kama hilo. Inawezekana ni mbinu mpya za matapeli wanataka kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu" amesema Mwaipaja.