Wazazi wavamia shule wakidhani watoto wanachomwa chanjo ya corona

Muktasari:
Wazazi wageuka mbogo baada ya kuona magari katika Shule ya Msingi Imanga huku wakidhani watoto wanachomwa chanjo ya corona
Kigoma. Wazazi wa watoto wanaosoma Shule ya Msingi Imanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wamezuka shuleni hapo kwa madai ya kuhoji sababu za wanafunzi kupewa chanjo dhidi ya corona bila kupewa taarifa.
Hata hivyo, Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Carlos Mabula amesema leo Jumatano Agosti 11 kuwa wazazi hao waliandamana na kufika shuleni hapo huku wakiwa na hasira ya kudhani ugeni uliofika shuleni hapo ni kwa ajili ya kuchoma chanjo wanafunzi wa shule hiyo.
"Nilitembelewa na wageni ambao ni watalaamu kutoka Tari (Taasisi ya Kilimo Tanzania) waliofika shuleni kwenye shamba la michikichi ili kujionea hali halisi ya shamba hilo. Hali hiyo ilisababisha mtafaruku uliolazimisha walimu kuanza kuwatuliza wazazi na kutoa elimu ya chanjo ya virusi vya corona.” amesema Mabula.
Awali, shuleni hapo yalifika magari mawili ya watafiti kutoka Tari kuangalia maendeleo ya shamba la michikichi lenye mbegu bora aina ya Tenera iliyofanyiwa utafiti na Tari-Kihinga.
Mmoja wa wazazi hao, Fikiri Waziri amesema kwa kuwa chanjo ni hiari, walimu hawawapi nafasi ya kupata elimu itokananyo na chanjo.
Soma zaidi: Masharti ya chanjo yaanza kuwabana wasafiri
Amesema kitendo cha magari kufika shuleni hapo kimewasababisha wanafunzi kukimbia kurejea nyumbani kuogopa kuchomwa chanjo.