Watu wanne wakamatwa Biharamulo kwa tuhuma za ujangili

Wa pili kutoka kushoto ni Kamishna msaidizi wa uhifadhi, hifadhi ya Taifa Ibanda -Kyerwa Fredirick Mofuli kulia kwake ni Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera William Mwampaghale na kushoto kwake ni Kamishna msaidizi wa uhifadhi, Hifadhi ya Taifa Rumanyika -Karagwe Charles Ngendo
Muktasari:
- Watuhumiwa wanne wa ujangili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kukutwa na nyara za Serikali pamoja na silaha mbili aina ya gobore na risasi tatu za kienyeji aina ya goroli.
Bukoba. Jeshi la Polisi mkoani Kagera linawashikiria watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majangiri kwa tuhuma za wizi wa nyara za Serikali katika Hifadhi ya Taifa ya Ibanda - Kyerwa na bunduki mbili aina ya gobore na risasi tatu za kienyeji aina ya goroli.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Februari 19, 2023, Kamishna msaidizi wa uhifadhi, hifadhi ya Taifa Ibanda – Kyerwa, Frederick Mofuli amesema watu hao walikamatwa na nyara za Taifa Februari 13, 2023 majira ya saa 3 usiku katika vijiji vya Muungano na Lusahunga wilaya ya Biharamulo mkoani hapa.
Amesema ukamataji ulipangwa na kufanikiwa baada ya kupata taarifa za kiinterijensia za uwepo wa mtandao wa watu wanaojihusisha na ujangili wa wanyamapori pamoja na biashara ya nyara za Serikali ambazo ni meno mawili ya tembo, ngozi ya fisi, kichwa cha fisi, vipande vitatu vya ngozi ya nyati, mkia wa nyati, ngozi ya swala aina ya pala na siraha mbili aina ya gobore na risasi tatu za kienyeji aina ya goroli.
“Meno yote mawili ya tembo yana uzito wa kilogram 9.15 na kati ya meno ya hayo, jino moja lenye alama ya A lina uzito wa kilogram 4.75 wakati jino la pili lenye alama A1 likiwa na uzito wa kilogram 4.40,” amesema Mofuli.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera, Wiliam Mwampaghale amesema jeshi hilo linawashikiria watu wanne kwa tuhuma za ujangili ambao ni Raphael Lugaira (44), Fikiri Rugaira ( 43), Majaliwa Charles (42) na Warwa Rupilya (45), wote wakazi wa wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera na kuwa watuhumiwa wote watafikishwa Mahakamani upelelezi ukikamilika.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, hifadhi ya Taifa Rumanyika – Karagwe, Charles Ngendo ametoa rai kwa Watanzania wote kutojihusisha na vitendo vya ujangili dhidi ya maliasili kwani jeshi liko imara na kwamba yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.