Watoto wawili wa familia moja wafa katika mazingira ya kutatanisha

Muktasari:
- Watoto wawili wa familia moja wa kitongoji cha Nyamiturumwa wilayani Serengeti wamekufa katika mazingira ya kutatanisha.
Serengeti. Watoto wawili wa familia moja wa kitongoji cha Nyamiturumwa wilayani Serengeti wamekufa katika mazingira ya kutatanisha.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara akiziungumza Mwananchi kwa njia ya simu amekiri kutokea kwa vifo hivyo Julai 28 jioni na polisi wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha vifo hivyo.
Mang'ora Wang'enyi baba mdogo wa watoto aliwataja waliokufa kuwa ni Edita Samson (11) mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Nyamakendo na mdogo wake Alphonce Samson (6) anayesoma chekechekea katika shule hiyo.
"Jana walikuwa shuleni wamerudi saa 10 jioni wakawa hapo nyumbani, mama yao alipotoka kwenye kikundi akawakuta wamelala wakiwa wanatoka mapovu puani na mdomoni, hawaongei ikabidi apige kelele kuomba msaada," amesema.
Amesema pamoja na juhudi za kuwapa huduma ya kwanza bila mafanikio waliamua kuwapeleka zahanati lakini walifia njiani.
"Alianza mkubwa kufa na baada ya dakika mbili mdogo naye akafa, tukaamua kutoa taarifa polisi na kwa viongozi wa kijiji,"amesema.
Kuhusu chakula amesema walikula mchana kisha wakarudi shuleni hivyo wanashindwa kuelewa kilichowakuta wanasubiri taarifa za uchunguzi wa kitabibu kujua chanzo cha vifo vyao.
Kwa mjibu wa katibu tawala wilaya miili ya watoto hao iko katika hospitali ya wilaya kwa ajili ya uchunguzi.