Watoto watatu waliopotea Lindi wakutwa porini wamenyongwa, wakatwa viungo
Muktasari:
- Kamati ya Ulinzi Mkoa wa Lindi inaendelea na uchunguzi kubaini waliohusika na mauaji ya watoto hao wakiwemo wawili wa familia moja.
Lindi. Watoto watatu wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Kilimahewa wa Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi waliopotea Juni 8, 2026 wakiwa njiani kwenda madrasa wamekutwa wamefariki dunia kwa kunyongwa.
Watoto hao ni Kulwa Mohamed (7) na Doto Mohamed (7), wanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mitopitopi pamoja na Rehema Mohamed (6), mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mpanyu.
Miili ya watoto hao ilipatikana kwa nyakati tofauti ambapo miwili ilipatikana Juni 13, 2026 na mmoja ulipatikana asubuhi ya jana Jumapili Juni 14, 2026 yote katika Pori la Kijiji cha Kilimawe.
Jana Jumapili, Juni 14, 2026, miili ya watoto hao ilizikwa ambapo viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi (RC), Zainab Telack walishiriki.
Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori alisema watoto hao walitoka nyumbani kwao Juni 8 kwenda madrasa ambako taarifa walizonazo hawakufika na kupotelea njiani ambapo walianza msako kuwatafuta.
“Ilipofika Juni 13, tuliwapata watoto wawili wakiwa wamekufa kwa kunyongwa ambapo ni Kulwa na Rehema ambaye huyu ameuawa kwa kunyongwa kwa kutumia kitambaa alichokuwa amejifunga akienda msikitini,” alisema Kamanda Imori.
Kamanda huyo alisema asubuhi ya jana katika pori hilohilo: “Tulimkuta mtoto wa tatu Doto Mohamed, yeye uchunguzi wa awali unaonyesha amekufa kwa kunyongwa shingoni hadi kufa na vilevile mtoto huyu amekatwa vidole gumba vya mikono yote miwili na sikio moja.”
“Sisi kama Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi kutulia, tukio hili si la kawaida na tunaomba mtupe fursa ya kuendelea kuwatafuta watuhumiwa waliotekeleza tukio hili la kinyama na tuendelee kuwalinda watoto wetu,” amesema Kamanda Imori.
Kamanda huyo amewahakikishia wananchi wa kijiji hicho kwamba hao waliohusika na unyama huo wanatoa mbaroni na sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kwa upande wake, RC Telack alilaani kitendo hicho na kuwataka wananchi kuwa na ushirikiano katika jamii katika kulinda usalama wa watoto.
"Tukio hili ni la kusikitisha na la kuhuzunisha sana. Natoa pole familia zilizopoteza watoto wao pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Lindi," amesema Telack.
Ametoa wito kwa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kuongeza umakini katika kuwafuatilia na kuwalinda watoto wakati wote ili kuzuia matukio kama haya yasijitokeze tena.