Watoto wataka mwarobaini wa vitendo vya ukatili dhidi yao

Baadhi ya watoto wakiwa kwenye maandamano ya kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika jijini Arusha. Picha na Bertha Ismail

Muktasari:

  • Wamesema kuwa vitendo hivyo vinawaathiri Katika makuzi yao ya kimwili, kiakili na kiafya.

Arusha. Watoto wameitaka Serikali na wadau wa maendeleo ya jamii kutafakari na kutathimini upya mwarobaini wa kutokomeza vitendo vya ukatili wanavyokumbana navyo.

Wamesema vitendo hivyo vinawaathiri makuzi yao ya kimwili, kiakili na kiafya na ni hatari kwa hatma ya Taifa la kesho linalowategemea kuja kuendeleza nchi katika nyanja za kisiasa, kidini, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.

Watoto wameyasema hayo Leo Jumapili Juni 16, 2024 jijini Arusha kwenye maadhimisho ya kilele cha Mtoto wa Afrika.

Akisoma risala kwenye maadhimisho hayo, Felister Nicolaus (14) amesema watoto wengi nchini hivi sasa wameendelea kuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili.

Amesema vitendo hivyo ni pamoja na kutelekezwa, vipigo, ubakaji na ulawiti sambamba na utumikishwaji wa kazi ngumu.

“Tunaingizwa kwenye ndoa za utotoni, mambo yote haya yanaathiri malezi na makuzi yetu, kimwili na  kifikra na yanakatisha ndoto zetu za maisha,” amesema Felister.

Amesema mara nyingi vitendo hivyo vinavyofanywa na ndugu wa karibu, jamaa hata wazazi.

Hivyo, amesema Serikali na wadau wa watoto wajue kwamba huu ni wakati mwafaka wa kulitafakari hilo kwa kina na kutafuta mbinu na njia zitakazoweza kusaidia kutokomeza vitendo hivyo.

“Kama mbinu hizi haziwezi, basi iwe ni wakati muafaka wa kutumia siku ya maadhimisho ya Mtoto wa Afrika  katika kutafakari na kutathimini hatua zinazoweza kuchukuliwa na Serikali, wadau wa maendeleo na wazazi ili kuweza kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto endapo mnahitaji Taifa salama la baadaye,” amesema Felister.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengewa amesema kukua kwa teknolojia na baadhi ya wazazi kupwaya kwenye malezi na makuzi ya watoto ni miongoni mwa sababu kubwa ya mmomonyoko wa maadili ambao Taifa linapitia.

Kutokana na hayo, amepiga marufuku baadhi ya shule na walimu kupokea misaada ya vitabu au vitendea kazi vyovyote bila kupata idhini ya ofisi yake ,akidai kuwa baadhi vimekuwa vikihamasisha vitendo vya mmomonyoko wa maadili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Iyanna foundation, Prisca Lema amesema wameendelea kutoa elimu juu ya makuzi na malezi ya watoto hasa katika kukabiliana na vitendo vya ukatili.

“Wazazi tumekuwa tukiwaambia wawe karibu na watoto wao, wasiwakaripie hovyo wala kuwapiga kipigo kikali kama adhabu pekee ya kosa lakini wawasikilize Ili kama kuna changamoto anapitia aweze kusema na kupata msaada wa haraka,” amesema Lema.

Ofisa ustawi wa jamii wa kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, Sara Ndaba amesema changamoto kwa sasa ni jinsi ya kuwaepusha watoto hasa wa mitaani dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Amesema katika kukabiliana na hilo, wanashirikiana na vituo vya malezi na makuzi ya mtoto ikiwemo Amani center Ili kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya, lakini pia kuwashawishi ili wakubali kurudi  kwenye familia zao au  kulelewa kwenye vituo.