Watatu kortini wakidaiwa kujifanya maofisa usalama
Muktasari:
- Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa yao Mei 17, 2023 katika mtaa wa Zaramo na Jamhuri eneo la Posta jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Wakazi watatu wa Morogoro wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na manne likiwemo la unyang'anyi wa kutumia silaha na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa usalama.
Washtakiwa hao ni Sufian Kidevu (30) mkazi wa Kizuka, Celestini Kamuli (32) mkazi wa Kizuka na mfanyabiashara Husein Mwinyijuma (37) mkazi wa Gairo, wote wanatoka mkoani Morogoro.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Januari 18, 2024 na kusomewa kesi ya jinai namba 1447/2024 na wakili wa Serikali Pancrasia Protas, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.
Hii ni mara pili kwa washtakiwa hao kufikishwa katika Mahakamani hapo, kwani kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Mei 29, 2023 na kusomewa kesi ya jinai namba 85/2023 yenye shtaka moja la unyang'anyi wa kutumia silaha na kuteka.
Kabla ya kusomewa kesi mpya yenye mashtaka manne, washtakiwa hao, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) aliwafutia kesi ya zamani ambayo ni kesi ya jinai namba 85/2023, baada ya kuieleza Mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendea na shauri hilo.
Washtakiwa hao walifutiwa shtaka lao chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Hadi wanafutiwa kesi hiyo, tayari upande wa mashtaka ulikuwa umesikiliza mashahidi zaidi ya watatu na vielelezo kadhaa.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kufutiwa kesi hiyo, washtakiwa hao walikamatwa na askari waliokuwepo mahakamani na kisha kupandishwa kizimbani na kusomewa kesi mpya yenye mashtaka manne.
Akiwasomea mashtaka mapya leo, wakili Protas amedai katika staka la kwanza, ambalo ni unyanyanyi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 17, 2023 katika mtaa wa Zaramo na Jamhuri eneo la Posta jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuiba simu moja ya mkononi aina ya iPhone, mali ya Hussein Mohamed.
Kabla ya kutenda kosa hilo, washtakiwa wanadaiwa kumtishia Husein kwa bastola aina ya Luger yenye namba A712040 ili waweze kutekeleza wizi huo.
Shtaka la pili ni kujitambulisha kama watumishi wa Umma, ambapo washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa siku na eneo hilo, walijitambulisha kwa Hussein kuwa wao ni maofisa usalama, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Pia washtakiwa hao wakabiliwa na shtaka la kuteka kwa nia ya kumzuia mtu, ambapo siku na eneo hilo hilo, washtakiwa wanadaiwa kumteka Hussein kwa nia ya kumficha, jambo ambalo walijua kuwa ni kosa kisheria.
Shtaka la nne ni kujaribu kumtishia mlalamikaji, ambapo siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja walijaribu kumtishia Hussein ili waweze kujipatia vitu walivyokuwa wanavitaka.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, washtakiwa walikana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomewa maelezo ya awali.
Hakimu Mushi aliwaambia washtakiwa kuwa shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo washtakiwa wataendelea kubaki rumande.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 22, 2024 na washtakiwa wamerudishwa rumande.