Wasiorejesha mikopo elimu ya juu kubanwa kila kona

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu (HESLB), Bill Kiwia (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya uchakataji wa taarifa za wakopaji (CREDITINFO), Edwin Urasa wakikabiziana hati ya ushirikiano kati ya Bodi hiyo na Taasisi hiyo, katika hafla ya kubadilishana hati za ushirikiano kati ya HESLB na wadau wa kimkakati,jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- HESLB imeungana na Nida, Rita na Credit Info kwa ajili ya kuwafikia wanufaika wenye kipato lakini hawajaanza kurejesha mikopo wanayodaiwa na bodi hiyo.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imeunganisha mifumo ya kimkakati kwa ajili ya kuwafikia wanufaika wenye kipato lakini hawajaanza kurejesha mikopo ya elimu.
Katika hilo HESLB imeingia makubaliano ya ushirikiano na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Taasisi ya Kuchakata Taarifa za Wakopaji Credit Info.
Akizungumza katika hafla ya kubadilishana hati za ushirikiano kati ya HESLB na wadau hao jijini Dar es Salaam leo, Jumatano, Septemba 11, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia amesema hadi sasa mikopo inayopaswa kurejeshwa ni Sh600 bilioni.
"Mikopo ambayo imeshaiva ni Sh2.1 trilioni na hadi sasa zimerejeshwa Sh1.5 trilioni, kuna kama Sh600 bilioni bado hazijarejeshwa, hivyo kama ilivyo katika kampeni za urejeshwaji mikopo, tumeamua kuunganisha mifumo ili kuwafikia wanufaika wenye kipato waanze urejeshaji," amesema Kiwia.
Vilevile, Kiwia amesema muungano na taasisi hizo unaboresha huduma na urahisi huku Bodi ikitekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo Desemba, 2024 mifumo yote ndani ya Serikali iwe inasomana.
"Kama ilivyo majukumu yetu ya kukopesha na kukusanya mikopo, hivyo hatua hii itaongeza tija kuwafuatilia na kuwafikia wanufaika wote nchi nzima," amesema.
Akitaja majukumu ya taasisi hizo walizoungana nazo akianza na Credit Info ambayo inajukumu la kutunza taarifa za wanufaika wa mikopo kwenye taasisi za kifedha hapa Tanzania.
Amesema, hivyo wameshirikiana nayo ili iweze kukusanya na kutunza taarifa za wadaiwa na wanufaika wa mikopo ya HESLB ambapo itasaidia bodi kuwafikia wanufaika hao.
"Kwa upande wa Rita, watahakikisha uhalali wa vyeti vya kuzaliwa na vifo na uombaji wa mikopo, hivyo itaongeza tija katika kazi zetu," amesema.
Kwa, Nida amesema watarahisisha kupata taarifa za makazi na mawasiliano ya wanufaika ambao hawajaanza kulipa madeni, hasa wale wenye kipato na wapo kwenye sekta binafsi.
Amesema ushirikiano na wadau hao umelenga kukuza uchumi kwa kubadilishana taarifa pamoja na kuwafatilia na kuwafikia wanufaika wote.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Deusdedit Buberwa amesema: "Nida jukumu lake ni kushirikiana na HESLB ili kuirahisishia kuwafikia wateja wake na kuwafikia wanufaika ambao hawajaanza kurejesha mikopo ili waanze kulipa.
"Pia, nitoe wito kwa Watanzania wote ambao waliwahi kukopeshwa na Serikali, wawe wazalendo wajitokeze wenyewe waanze kurejesha," amesema Buberwa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Credit Info Tanzania, Edwin Urasa amesema wako tayari kushirikiana na HESLB katika kufanikisha mchakato mzima wa ukopaji na urejeshwaji mikopo hiyo unafanikiwa.
Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Frank Kanyusi amesema katika muunganiko huo Rita itajikita katika jukumu la vizazi na vifo.
"Katika kuhakikisha wenzetu wa HESLB wanatoa mikopo kwa wakati basi Rita tumetengeneza mfumo wa kieletroniki ambao unaunganisha kati yetu na bodi kurahisisha wanafunzi kufanya mchakato wa mikopo kwa ujumla," amesema.