Waombolezaji waanza kuwasili Karimjee kumuaga Profesa Sarungi

Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakiwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga mwili wa Profesa Philemon Sarungi. Picha na Sunday George
Muktasari:
- Makundi mbalimbali ya wananchi na viongozi wastaafu yameanza kuwasili katika Uwanja wa Karimjee kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Profesa Philemon Sarungi.
Dar es Salaam. Viongozi wastaafu wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndio waliofika hadi sasa katika Uwanja wa Karimjee, Dar es Salaam kutoa heshima za mwisho kwa daktari, mwanasiasa, na waziri wa zamani, Profesa Philemon Sarungi.
Mwili wa Profesa Sarungi aliyefariki dunia jioni ya Machi 5, 2025 unatarajiwa kuagwa na kuzikwa leo Jumatatu, Machi 10, 2025 jijini hapa.

Waombolezaji wakiwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga mwili wa Profesa Philemon Sarungi. Picha na Sunday George
Sambamba na viongozi hao, kundi lingine lililowasili mapema hadi saa 4 asubuhi katika eneo hilo ni madaktari wakiongozwa na Chama cha Madaktari wa Mifupa Tanzania (TOA).
Pia, kulikuwepo waombolezaji wengine waliofika kutoka makundi mengine mbalimbali, akiwemo Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu.
Katika orodha ya viongozi waliofika viwanjani hapo, yumo Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba na Katibu wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku.
Pia, amefika Katibu Mkuu na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana na Balozi Christopher Liundi.
Kwa upande wa Chadema, waliofika ni Mwenyekiti, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, huku ACT Wazalendo aliwasili Kiongozi wake mstaafu, Zitto Kabwe
Hadi saa 3:52 asubuhi ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ndiye kiongozi wa Serikali aliyefika katika eneo hilo, huku kwaya ya Kanisa la Waadventista wa Sabato ikiendelea kuimba.
Profesa Sarungi alifariki dunia jioni ya Machi 5, mwaka huu kwa maradhi ya moyo kwa mujibu wa familia akiwa na umri wa miaka 89.
Enzi za uhai wake, amewahi kuwa Mbunge wa Rorya, Waziri wa Afya, Waziri wa Elimu, Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, pia alitumikia sekta ya afya kwa nafasi ya Daktari Bingwa wa Mifupa.
Watu mbalimbali wamemuenzi kwa utumishi wake usio na mawaa, wakimtaja kuwa mzalendo aliyewapenda Watanzania katika nafasi yoyote walivyowahi kuishika.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu (kushoto) akisalimiana na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana walipokutana leo Jumatatu Machi 10, 2025 katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kumuaga Profesa Philemon Sarungi.
Hata hivyo, hapa Karimjee waombolezaji mbalimbali wameendelea kuwasili kutoa heshima za mwisho, wakati mwili ukisubiriwa kuwasili kutoka Hospitali ya Lugalo.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali